Haleluya, nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, habari za kutwa nzima. Bila shaka umekuwa mshindi wa leo, maana umeimaliza siku ukiwa mzima.

Kuna mambo tunaweza kujiendea katika maisha yetu, tukajikuta tunakwama kwa sababu hatuna Mungu ndani yetu. Kama yupo basi ni jina tu ila matendo yetu yanamkataa Kristo.

Wakati mwingine tumeshindwa kusogea kihuduma kwa sababu ya kutotii na kutulia mbele za Mungu, tumejikuta tunatumia muda mwingi kutumia akili zetu pasipo Mungu ndani yake.

Wakati mwingine tumesubiri mambo yaende vibaya ndipo tunamkumbuka Mungu wetu, wakati kulikuwa na uwezekano wa kutosubiri mambo yaharibike ndio uanze kuchukua hatua.

Wengi wetu tukiambiwa tusome NENO LA MUNGU, hatutaki kusikia, ila yakishatukuta ya kutukuta ndio tunaanza kukumbuka yale maneno tuliyoambiwa.

Tunapaswa kuelewa kwamba, ili maisha yetu yawe bora na si bora maisha yaende, tunapaswa kumtafuta Mungu kwa bidii na kumjua yeye vizuri. Ili maisha yetu kiroho na kimwili yawe salama siku zote.

Tunajifunza zaidi kwa mfalme Daudi akiwa anamwachia mwanaye Suleiman madaraka ya kiti chake. Kuwa amshike sana Mungu ndipo mambo yake yataenda vizuri.

Rejea: Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa BWANA hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele. 1 NYA. 28:9 SUV.

Anayejua mawazo yetu ni Mungu, hakuna jambo unaloliwaza halijui Mungu, ikiwa ni hivyo kwanini tusishikamane naye kwa bidii zote.

Pamoja na kushikamana na Mungu, hatuwezi kuwa na hasara, maana tukimtafuta kwa bidii anapatikana. Mbaya zaidi ni pale tunapomwacha naye anatuacha milele, ndivyo NENO LA MUNGU linavyotuthibitishia haya.

Ipi bora kuendelea kutangatanga na dunia au kushikamana na Mungu kwa moyo wako wote, mi naona bora kukaa sehem ambayo napata msaada wa kweli usio na kikomo.

Yafaa nini kumtafuta mungu anayetuingiza kwenye madhara ya maisha yetu ya sasa na ya umilele? Itafaa sana kumfuata Mungu wa kweli anayetimiliza ahadi zake za kweli kwa wamchao katika roho na kweli.

Unaweza kuamua leo kujitoa katika roho na kweli ili umwone Mungu katika maisha yako ya sasa. Hebu tamani kumwona Mungu huyu anayesema haya maandiko Matakatifu.

SOMA: Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa BWANA hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta,u ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele. 1 NYA. 28:9 SUV.

Nakusihi sana endelea kumjua Mungu kupitia NENO lake takatifu, litokalo ndani ya biblia, na kusikiliza mafundisho ya watumishi wake wa kweli. Hakika utaona nguvu za MUNGU zikiwa juu yako.

Usiache kuwa mtu wa maombi, maombi yatakuwezesha kudai haki zako za msingi, na kuzungumza na Mungu aweze kukupa sawasawa na ahad zake.

Unavyoendelea kumjua Mungu vizuri, ndivyo uhusiano wake na wako unazidi kuwa imara zaidi. Haitokei ukamjua Mungu alafu ukaanza kuishi maisha ya mazoea mbele zake. Labda hapo tutasema huyu mtu amerudi nyuma kiimani, maana Mungu wetu anatufanya upya utu wetu wa ndani kila wakati.

Bila shaka kupitia maneno haya umepata kitu cha kukusaidia kujimarisha katika imani yako. Uwe hodari katika kumjua Mungu, nawe utafanikiwa katika maisha yako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com