“Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe”, Rum 15:1 SUV.

Mtume Paulo anafundisha jambo la msingi sana kwa kanisa, hasa wale waliokomaa katika imani na wale ambao bado wachanga kiroho.

Sura 14 tuliona mtume Paulo akiwafundisha Warumi kuhusu siku na vyakula, vile watu walikuwa wanahukumiana katika hayo. Akawaweka sawa kuhusu hilo.

Leo anaendelea katika sura 15, namna ya kuwabeba wale walio dhaifu katika imani, yale ambayo wanahitaji kusaidiwa na wale walio imara katika imani.

Kuna vitu kwa mwamini mchanga ukiviona akiwa anavifanya unaweza kuchukizwa au kukerwa sana.

Tunapogundua kuwa anafanya kwa sababu ya uchanga wake wa kiroho, tunapaswa kumsaidia kwa upendo ili asipotee.

Mtu aliyekomaa kiroho anapaswa kujua namna ya kumlea aliye mchanga, hii sio ngumu kwa kila mmoja wetu tuliokomaa kwa sababu tumewahi kupitia hiyo hali.

Hatupaswi kuwatenga wale walio dhaifu katika imani, hatupaswi kuwashambulia na kuwaambia maneno ya kuwavunja moyo.

Mtu kutokana na uchanga wake anaweza kudanganywa akafanya jambo ambalo ni chukizo mbele za Bwana.

Mtu huyo anapaswa kusaidiwa katika upole na upendo ikiwa anakubali kurejeshwa katika njia sahihi.

Tunapaswa kuondoa ule ubinafsi, kila mmoja anapaswa kumwona mwenzake ni wa thamani mbele za Mungu.

Tunapaswa kujitoa mhanga kukubali madhifu yao na kuwasaidia wale washirika au waumini au waongofu walio wachanga kiroho.

“Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani”, Warumi 15:2 NEN.

Paulo ananukuu Zaburi 69:9, kutetea hoja hii ya msingi ikisema hivi; “Maana wivu wa nyumba yako umenila, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata”.

Paulo anaonesha wazi kwamba Mkristo anapaswa kujitoa na kukubali kuteseka kwa ajili ya watu wengine, hii ni sehemu mojawapo muhimu ya umisheni.

Tukilielewa hili tutawasaidia wale waliompokea na watakaompokea Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao, watakua vyema katika imani waliyoiamini katika maisha yao.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081