Leo unamwona fulani ni mwaminifu sana, kesho shetani anaweza kumwingia na mtu huyo akaacha kuwa mwaminifu kabisa.

Leo unamwona mtu ana bidii sana kwa mambo ya Mungu, mtu huyo asipokuwa makini, ile bidii yake inaweza kutoweka na akabaki mtu wa kawaida asiyependa mambo ya Mungu.

Leo unamwona mtu ni mwaminifu sana kwa mke/mume wake, mtu huyo asipojibidiisha kuendelea kuliweka Neno la Mungu moyoni mwake. Kuna mahali atafika atajikwaa, alafu ule uaminifu wake ukawa haupo kwake tena.

Leo unamwona mtu ni kahaba/malaya sana, siku huyo mtu akikutana na Yesu Kristo, hutomjua kama ni yeye alikuwa na tabia hizo chafu.

Leo hii unamwona mtu ni mlevi sana, pombe ni kama maji ya kunywa kwake, siku mtu huyo akikutana na Yesu Kristo kisawasawa. Unaweza kuanza kujiuliza unaona sawasawa au unamfananisha.

Tabia ya mtu iwe nzuri au iwe mbaya, inaweza kubadilika muda wowote, kutegemeana na mtu atakavyofanya. Kosa moja linaweza kumpelekea mtu yule kupoteza sifa ya kuwa mtoto wa Yesu au mtoto wa shetani.

Mfano, mtu anaweza kupanga njama mbaya kwenda kuharibu mkutano mahali fulani kwa kutumiwa na shetani. Kosa hilo la kutaka kwenda kuharibu mkutano wa injili, linaweza kumfanya aokoke siku hiyo hiyo mkutanoni.

Haijalishi mtu amesumbua sana na kufanya vituko vingi sana vya kutisha jamii, siku Mungu akiingilia kati, mtu huyo anaweza kugeuka tena mshangao kwa watu waliokuwa wanamfahamu tabia zake.

Rejea: Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. MDO 9:13‭-‬15 SUV.

Sauli aliogopwa na kila mtu, ila saa ya Bwana ilivyofika, aligeuzwa kuwa mtu mzuri, hakuna aliyeamini hicho kitu. Ila huo ndio ulikuwa ukweli, ukweli ambao kila mmoja aliuthibisha kwa matendo makuu aliyoyatenda kupitia jina la Yesu Kristo.

Ndio nikasema mtu anaweza kubadilika muda wowote, awe mtu mbaya sana anaweza kubadilika, ama awe mtu mwema sana anaweza kubadilika pia. Cha msingi ukiwa mtu mwema unapaswa kulinda sana hicho kitu kisijekukuponyoka kwenye mikono yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com