“Yesu alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,” Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani kwake”, Yohana 19:26‭-‬27 NEN.

Wakati Yesu yupo katika maumivu makali pale msalabani, hakuacha kuangalia usalama wa mama yake aliyekuwa eneo hilo la mateso. Alimteua mwanafunzi yule aliyekuwa anampenda na aliyekuwa hapo wakati huo ambaye anasemekana ni Yohana, alimwambia amwangilie au amtunze mama yake.

Katika maisha kuna watu tunawaamini kutokana na mahusiano ambayo tumekuwa nayo kwa muda mrefu tukiwa hai, unaweza ukamwamini mtu kuliko hata ndugu zako wa damu kutokana na uhusiano wenu.

Inapotokea shida hasa kifo, watu hawa wa karibu mara nyingi hutuachia maagizo ya kuangalia familia zao, usifikiri huwa wanaongea tu ni jambo ambalo lipo kibiblia kabisa kama tulivyoona hapa kwa Yesu.

Agizo hili aliloachiwa mwanafunzi wa Yesu kuhusu kumwangalia mama yake Yesu, inatukumbusha kuwasaidia wale wanaoachwa au wanaofiwa na wapendwa wao.

Ukikuta mtoto/watoto wadogo wameachwa na mama au baba yao, inawezekana ulikuwa rafiki wa karibu wa familia ile, usiache kusimama kama mzazi kuhakikisha watoto hao wanatunzwa na kufikia malengo yao.

Huo ni upande wa watoto unaweza kuachiwa hata mzazi wa mwingine umlee kutokana na hali yake kimaisha na umri wake, usiache kufanya hivyo maana kuna baraka nyingi katika kufanya hayo.

Usimtese mtoto uliyeachiwa umlee, hakikisha anakuwa salama na kutoona tofauti kubwa ya wazazi wake walioondoka duniani, mfanye ajione ni sehemu ya familia yako.

Watu wengi huwa hatujui kuwa huwa tunajitafutia laana pasipo kujua, unaachiwa mtoto umlee wewe unaanza kumtesa kwa kumfanyisha kazi ngumu kupita umri na uwezo wake, kumnyima chakula, kumnyima mavazi, kula chakula kisichofaa, kumtukana matusi mabaya.

Mtoto kukumbuka wazazi wake

Usiongeze majeraha mengine kwa mtoto aliyeondokewa na wazazi wake au mzazi wake, hakuna faida utakayopata kwa kumtesa zaidi utajitafutia dhambi ambazo zitakugharimu maisha yako.

Mungu akusaidie uweze kuelewa jukumu hili la kuwalea wale ulioachiwa uwalee, unaweza kuwa hukuachiwa kwa maagizo maalumu ila angalia uhusiano uliokuwa nao na marehemu, maana wapo watu huachwa na wategemezi wao.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081