Haleluya mwana wa Mungu, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, habari za leo, bila shaka siku yako inaenda vyema. Na kama kuna changamoto unapitia Mungu akutie nguvu uvuke salama.

Katika maisha kupo kushinda kwingi na kupo kushindwa kwingi, yote hayo yapo na yanatokea mara kwa mara katika maisha yetu.

Unaweza kuanzisha biashara yako vizuri ukitegemea kufanikiwa katika biashara hiyo, lakini ikatokea ukaanguka, na mwingine akafanikiwa katika bishara ile ile.

Unaweza kuanza masomo yako vizuri, ukafika siku ya kufanya mtihani wa mwisho ukaanguka vibaya, na wenzako wakafanikiwa katika mtihani huohuo.

Unaweza ukaanza mahusiano ya ndoa, yakakuletea shida mpaka ukamua kutengana na mwenzako. Ila yupo mwenzako anaishi na mke/mume kama mapacha waliozaliwa tumbo moja.

Unaweza kuanzisha mahusiano ya uchumba, yakakuvuruga mpaka ukafika wakati huna hamu tena ya kuanzisha mahusiano mengine mapya ya kuelekea ndoa. Ila yupo mwenzako katika mahusiano hayohayo ya uchumba anayafurahia kiasi kwamba anatamani kesho wawe mwili mmoja.

Labda umeanza kujiuliza nakupeleka wapi sasa huko, uwe na subira ngoja nikupitishe kidogo kwenye andiko hili uone jinsi Mungu anaweza kukupa kushinda.

Rejea; Hata aliposikia Tou, mfalme wa Hamathi, ya kuwa Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, mfalme wa Soba, akampeleka mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi, ili kumsalimia, na kumbarikia, kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou; naye akaleta vyombo vya dhahabu, na fedha, na shaba, vya namna zote. 1 Nya 18 :9_10.

Nazungumzia mshindi na mshindwa, hapa tunaona mfalme Tou alishindwa vita na jeshi la Hadadezeri. Ila pamoja na Tou kushindwa kwake, yupo mtu aliyeshinda pale aliposhindwa yeye.

Mtu huyo aliyeshinda si mwingine bali ni mfalme Daudi, huyu ndiye aliyewapiga maadui wote. Maana Mungu alikuwa upande wake na alimpa kibali cha kuwapiga madui zake, na kushinda.

Rejea; Akaweka ngome katika Edomu; na Waedomi wote wakawa watumwa wa Daudi. Naye Bwana akampa Daudi kushinda, kila alikokwenda. 1 Nya18 :13.

Wanaoshinda vita vya rohoni ni wale wanaofuata kanuni za KiMUNGU, na wanaoshindwa vita vya kiroho ni wale wasiofuata kanuni za kiMungu.

Wanaoshinda katika biashara zao ni wale wanaofuata kanuni za kibiashara, na wanaoshindwa ni wale wasiofuata kanuni za kibiashara.

Wanaoshindwa katika mahusiano ya ndoa, ni wale wasiomcha na kumtegemea Mungu. Na wanaoshinda katika ndoa ni wale wanaomtanguliza Mungu kabla na baada ya safari ya mahusiano.

Kila eneo lina kanuni zake, ila kanuni iliyokuu ni kumtengemea Mungu kwa kila jambo, na kulishika neno lake.

Mungu anapaswa kuwa kipaombele kwa kila hatua za maisha yako, iwe katika ndoa, biashara, Kazi, huduma/utumishi na familia. Mungu anapaswa kuwa sehemu yako na kiongozi wako.

Daudi alishinda vita hii kubwa kwa sababu alimwomba Mungu kabla ya kuingia vitani, hili tunaliona katika andiko lifuatalo;

Rejea; Daudi akamwuliza Mungu, kusema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye Bwana akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako. 1 Nya 14 :10.

Kumbe jambo lolote linapofanikiwa msingi wake huanzia katika maombi, na jambo kushindwa msingi wake hukuwekwa vizuri katika maombi.

Tunaweza kuomba Mungu kuhusu jambo fulani akaturuhusu, na vilevile tunaweza kuomba Mungu kuhusu jambo fulani akatuzuia kulifanya.

Haya yote ni kwa wale wanaotii NENO LA MUNGU, na kulifuata. Ndio watakaofanikiwa.

Mungu akuwezesha upate kuyatenda mapenzi yake ili upate kushinda.

Samson Ernest.
+255759808081.