Haleluya,

Sijui tuna nini inayotusumbua sana wanadamu, sijui ni kukosa imani mioyoni mwetu au sijui ni kuona alichotutendea Mungu hakiwezekani tena kututendea jambo lingine kubwa zaidi.

Sijui tuna shida gani ambayo inatufanya tufike wakati tunaona matendo makuu maishani mwetu anayotutendea Mungu. Pale pale tunapata ujasiri wa kumtenda Mungu dhambi, huenda tukasaidiana kufikiri hili.

Nimeanza na kama maswali ya kufikirika, ila napenda tuwe pamoja katika ujumbe huu. Nina imani mpaka kushusha kalamu yangu, nitakuwa nimesema nawe jambo moja kupitia ujumbe huu.

Kabla hutajaendelea, naomba ukumbuke muujiza mmoja tu aliowahi kukutendea Mungu. Labda kwa haraka haraka unaweza kupata shida kidogo kujua ni nini Mungu amewahi kukufanyia ambacho hutokuja kukisahau.

Nikurahishie hilo, kufikia siku ya leo na saa hii, na ukapata nafasi ya kusoma hapa, bila kukuficha wala kukupita pembeni. Huu ni muujiza mkubwa sana, kwanini ni muujiza mkubwa sana kuna mtoto amezaliwa leo na kufa saa hiyo hiyo baada ya kuzaliwa.

Lakini wewe huenda ulizaliwa katika mazingira fulani matata sana, ila Mungu amekukuza mpaka leo upo hapo ulipo. Huenda kuna wakati mzazi alihangaika sana kwa kuugua kwako kila mara, huenda kuna ugonjwa ulipita ukaua sana watoto, lakini wewe hujafa upo mpaka leo.

Usije ukafikiri ni jambo la kawaida sana, huu ni muujiza mkubwa sana ambao ukikaa ukatafakari vizuri utaelewa ninachosema hapa. Unaweza ukainuka tena na usiweze kukata tamaa tena, maana utajenga picha nzuri sana kwako.

Nirudi sasa Kwenye moyo wa somo hili, pamoja na mambo yote hayo mazuri Mungu kututendea katika maisha yetu. Bado imani yetu inayumbayumba sana, maana yake hatuna uhakika na ukuu wa Mungu wetu.

Jana nilifanikiwa kukaa na ndugu yangu mmoja tunayetoka kijiji kimoja na alinipita madarasa kadhaa mbele. Baada ya maongezi kuendelea nilikuja kujua alishabadilisha dini yaani akawa sio mkristo tena, tena mbaya zaidi lile jina lake la awali akawa halitaki hata kulisikia. Maana aliniambia nalichukia sana hili jina ila sina namna ilishatokea.

Huyu mtu alikuwa mkristo ila akaamua kuachana na ukristo akahamia kwenye uislamu, yale matendo ya Mungu maishani mwake hakuyakumbuka tena. Alichoona yeye ni cha maana sana kwake na sasa anajivunia kuacha kuamini jina la Yesu Kristo.

Nisiende mbali sana, nirudi kwetu waamini ambao bado tunasema Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wetu. Pamoja na Mungu kututendea mambo makuu katika maisha yetu, bado tunakuja kuona Mungu hawezi kutusaidia baadhi ya maeneo.

Leo kijana anasema haiwezekani kuacha dhambi ya uasherati ukiwa hujaoa/hujaolewa. Anaamua kuhalalisha kile ameona kwake kinamfaa kufanya wakati huo, amesahau aliyekataza hilo tendo ni Mungu aliyemwokoa na ile ajali, amesahau anayekataza uasherati ndiye aliyemponya ule ugonjwa baada ya madaktari kushindwa.

Binti anakaa kanisani vizuri, anaona anachelewa kuolewa na ameomba sana Mungu wake. Anamua kujiachia kwa mwanaume yeyote yule ili aoelewe, matokeo yake anajazwa mimba na kuharibu ushuhuda wake.

Mungu atufanyie nini wanadamu, mtu upo ndani ya ndoa bado una vimada vingine nje. Mtu unafanya huduma lakini unatembea na wadada/wamama wa kanisani kwa siri. Mungu akupe nini uweze kujua ya kwamba huyu ni Mungu asiyependa michanganyo.

Rejea: Aliipasua bahari akawavusha; Aliyasimamisha maji mfano wa chungu. Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto. Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi. Akatokeza na vijito gengeni, Akatelemsha maji kama mito. ZAB. 78:13‭-‬16 SUV.

Pamoja na Mungu kuwatendea mambo makuu wana wa Israel, na kuona waziwazi uweza wake mkuu. Lakini bado walimtenda Mungu dhambi mbaya sana.

Rejea: Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye juu katika nchi ya kiu. Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao. ZAB. 78:17‭-‬18 SUV.

Unajua dhambi gani unamtenda Mungu wako, nikuombe uchukue hatua za kutubu sasa. Ifike mahali useme imetosha sasa, wengine wanaweza vipi kuishi maisha bila ngono na wewe ushindwe, wengine wameweza vipi kuvumilia mpaka wakapata kile Mungu aliwaandalia wakipate na wewe ushindwe una nini.

Rejea: Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, Wakamwambia uongo kwa ndimi zao. Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema, Husamehe uovu wala haangamizi. Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake, Wala haiwashi hasira yake yote. ZAB. 78:36‭-‬38 SUV.

Haijalishi ulimdanganya Mungu kiasi gani mbele ya kanisa lake, ingia magotini sasa utubie uovu wako, naye Mungu atakusamehe dhambi zako zote.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
www.chapeotz.com
+255759808081.