
Mungu hawezi kukushtukiza kwaajili ya kumtumikia, ni lazima ataweka mazingira ya wewe kwanza kutambua kile alichoweka ndani yako.
Ukishajua sasa hapo ndipo huanza kufanya maandalizi ndani yako, na kwanza kabisa anabadilisha mtazamo wako kwa habari ya utumishi.
Huenda ulikuwa ukifikiri kazi ya Mungu ni mzigo na kamwe hautaweza kufanya hiyo kazi, hivyo Mungu anaanza kubadilisha mtazamo wako, na ndani yako anaweka utayari na moyo wa kupenda kumtumikia.
Tunapotafakari sura hii ya kutoka 28 tunaona ni jinsi gani Haruni alianza kuandaliwa kwaajili ya ukuhani, na mpaka watoto wake waliingizwa kwenye hayo maandalizi maana nao ni uzao wa kikuhani.
Hivyo wasingeweza kuwa tu kama watoto wengine, iliwapasa pia kuwa watakatifu na kuwa na mtazamo kama wa baba yao wanapoingia kwenye huo utumishi pamoja.
Nawe umlete Haruni ndugu yako karibu nami, na wanawe pamoja naye, miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haruni, na Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari, wana wa Haruni. 2 Nawe utamfanyia Haruni ndugu yako mavazi matakatifu, kwa utukufu na kwa uzuri. KUT. 28:1-2 SUV.
Katika mstari wa pili tunaona kwamba, kumbe Mungu anapomuandaa mtumishi wake, anabadilisha hata kuvaa kwake.
Kuvaa kwa mtumishi wa Mungu kunapaswa kuwe katika utaratibu, kwanza yawe ni mavazi yakumpa Mungu utukufu, lakini pia yawe ni mavazi mazuri yenye kupendeza.
Musa aliagizwa kumfanyia Haruni mavazi, sio kwamba Haruni hakuwa na mavazi, bali Mungu ndiye alitaka aingie katika huduma akiwa na mavazi mapya yenye utukufu na uzuri pia.
Hivyo tunaweza kuona kwamba si kila vazi linafaa kwa mtumishi wa Mungu, na si kila vazi mtumishi wa Mungu anaweza kupanda nalo madhabahuni, ni lazima atazame pia ni vazi gani zuri na lenye utukufu.
Hebu tusome huu mstari pia;
Na Haruni atayachukua majina ya wana wa Israeli katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu juu ya moyo wake, hapo atakapoingia ndani ya mahali patakatifu, kuwa ukumbusho mbele ya BWANA daima.KUT. 28:29 SUV.
Lakini pia tunaona jinsi gani Watumishi wa Mungu anavyopaswa kuwabeba watu wote wanaowaongoza mbele za Mungu, katika kuwaombea.
Mtumishi wa Mungu analo jukumu kubwa sana kuomba kwaajili ya kundi analoliongoza, wapo watu wenye mizigo mbali mbali na wengine hawajui nini cha kufanya.
Kama Kuhani ambaye Mungu amekupa nafasi ya kupaingia pale patakatifu pa patakatifu, ambapo Mungu anasema na wewe, hivyo unapaswa kuwabeba watu hao ili Mungu aweze kuwatazama katika shida zao.
Mungu anapokuchagua kumtumikia kwaajili ya watu wake, jiulize kwamba wewe ni nani kati ya wengi ambao wameachwa, tambua kwamba ni neema tu ya Mungu ambayo ameiachilia juu yako, na ili akuinua juu ya adui zako na za watu wako pia uwe wokovu kwao.
Kama Mungu alimfanya Haruni kuwa kuhani, ni ili watu wake wapata mhudumu katika madhabahu yake, na watu wapate msaada wa haraka pale wanapohitaji msaada wa Mungu.
Badilisha mtazamo wako, usemi wako, kuvaa kwako, na maisha yako kwa ujumla, ili Roho Mtakatifu apate nafasi yakutosha kuweza kufanya kazi pamoja na wewe.
Unapenda kusoma Biblia yako kila siku lakini watu wa kusoma nao au hujui utaanzaje, karibu sana kwenye kundi la wasap la kusoma Biblia kila siku. Tuma neno CHAPEO YA WOKOVU kwenda wasap +255759808081, karibu sana.
Mungu wa mbinguni akubariki.
Rebecca Ernest.