Dunia ya leo imemeza wengi katika maeneo mbalimbali ya maisha yao, wapo wamemezwa muda wao, hawawezi tena kumpa Mungu nafasi katika maisha yao. Wapo wamemezwa na magonjwa hawana tena uwezo wa kwenda kumtumikia Mungu wao, wamebaki kulala tu.
Wapo wamemezwa kwenye shughuli mbalimbali za kidunia, hawana tena muda wa kumwomba Mungu wao. Hawana muda wa ibada na Mungu, hadi siku za ibada wao wanafanya kazi zao.
Wapo wamemezwa na waume/wake zao, hawawezi tena kuomba Mungu, hawana tena muda wa kwenda kumtumikia Mungu wao. Zile huduma alizoweka/alizowapa Mungu, wameziacha kwa sababu ya mke/mume wake.
Mke amekuwa kikwazo cha huduma ya mume wake, na mume amekuwa kikwazo cha huduma ya mke wake. Kila akijaribu kutoka kumtumikia Mungu wake, mume/mke wake anamzuia.
Wapo watu wamemezwa kwenye matumbo ya ulevi, kila wakijaribu kuacha ulevi wanajikuta wanarudia lile lile wanalolikataa. Wanajaribu kutafuta washauri wazuri wa kuweza kuwasaidia ili waondokane na hiyo shida ya ulevi, imeshindikana.
Wapo watu wamemezwa kwenye tumbo la madawa ya kulevya, wamejaribu kwenda kwenye vituo vya kutibiwa ili waache hiyo tabia. Lakini badala yake, baada ya kuruhusiwa kutoka walirudia tena kutumia yale yale madawa.
Wapo watu wamemezwa kwenye tumbo la uasherati/uzinzi, kila wakijaribu kuacha kwa akili zao. Wanajaribu kwenda kanisani kabisa, baada ya siku mbili tatu, wanajikuta wameanguka tena kwenye dhambi ile ile ya uasherati/uzinzi.
Wapo watu wamemezwa kwenye tumbo la kutoa mimba, kazi yao ni kufanya ngono na wakishajazwa mimba wanazitoa. Hawapo tayari kuzaa ila wapo tayari kuzini ovyo, wakisema kuanzia sasa naacha ila baada ya muda fulani wanarudia tena yale yale.
Wapo watu wamemezwa kwenye tumbo la uvivu wa kusoma Neno la Mungu, wanajikakamua leo na kesho. Siku ya tatu au ya tano unamwona anarudi kule kule, akisema kuanzia sasa sitaki tena uvivu, utamkuta muda wa kusoma Neno la Mungu yeye yupo mitandao ya kijamii anadhurura tu, wala hana la kufanya zaidi ya kuchati tu.
Kwa akili zako hutoweza kuacha, hutoweza kushinda hizo hali zilizokukaba au zinazokusumbua, unamhitaji huyu Yesu Kristo aliye hai. Unahitaji utakaso wa damu ya Yesu Kristo, damu ya Yesu Kristo inahuhisha, inasafisha, ina ulinzi, na inaokoa.
Rudi kwa Yesu Kristo akutoe kwenye tumbo hilo lililokumeza, unajua ndani ya moyo wako ni tumbo la namna gani limekumeza katika maisha yako. Mwambie Yesu Kristo naja kwako, mimi mwenye dhambi, naomba unisamehe kwa yote niliyokutenda, naomba unitakase kwa damu yako takatifu. Nisaidie nisije nikarudi nyuma tena.
Kama umedhamiria kweli kuacha na kugeuka, utaona badiliko ndani yako, utaona kiu ya ulevi ikikata kabisa, utaona hujisikii tena kufanya umalaya/ukahaba, utaona ile hali ya kukataa ibada ikitoweka kabisa. Maana Yesu Kristo ameshaingia ndani ya moyo wako, umekuwa kiumbe kipya kabisa mbele za Bwana.
Hili tunajifunza kwa Yona, Yona alikuwa kwenye tumbo la samaki, tunaweza kusema alikuwa kwenye gereza zito. Ambalo tumelifananisha na uzinzi, uasherati, ulevi, madawa ya kulevya na mengine yanayofanana na hayo.
Rejea: BWANA akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani. YON. 2:10 SUV.
Yona baada ya kumlilia Mungu katika shida yake, Mungu alimwamru samaki amtapike Yona ufukweni(pwani) naye Yona akawa huru.
Rejea: Ndipo Yona akamwomba BWANA, Mungu wake, katika tumbo la yule samaki, Akasema, Nalimlilia BWANA kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu naliomba, Nawe ukasikia sauti yangu. YON. 2:1-2 SUV.
Hata wewe unaweza ukawa huru sasa kwenye kifungo ulichofungwa na shetani, ili usitimize kusudi la Mungu alilokuitia Duniani. Mwambie Yesu Kristo akutoe kwenye tumbo hilo ulilomezwa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.