Wazazi wanapitia changamoto ya watoto wao kutoolewa na kutooa kwa wakati waliotarajia wao, vijana wa kiume wakiulizwa kuhusu hili wana sababu nyingi juu ya hili.

Wapo watakuambia bado hawajaona wa kumuoa, wengine watasema wasichana wanachagua sana wanaume wa kuwaoa, wengine watakuambia muda bado, na wengine wanauguza maumivu ya kuachwa kipindi kilichopita.

Wengine wana hofu kutokana na walivyoona ndoa zingine zikiwaumiza watu wengine, na kuwaacha na makovu mabaya. Wengine ni wazazi wao, wengine ni dada zao, kaka zao, ndugu zao, marafiki zao, na wengine ni majirani zao.

Wasichana wakiulizwa wanadai wanawasubiri wanaume waje kuwaoa, wengine hawaoni sababu ya kuolewa kutokana na yale mambo mabaya waliyofanyiwa huko nyuma.

Wengine wanatamani kweli kuolewa ila hawana imani na wanaume kabisa wanapokuja kwao kuletea ombi la kuwaoa, wanaowaona ni wale wale waliowaumiza kipindi cha nyuma au waliowaumiza ndugu zao au marafiki zao.

Wazazi au ndugu au marafiki wanapoweka msisitizo mkubwa kwao, huona usumbufu na kuamua kujitupia kwa mwanamke/mwanaume yeyote anayejitokeza mbele yake au yule ambaye ndugu zake au wazazi wake wanamtaka wao.

Wanafanya hivyo kuepusha makelele wanayopigiwa kila siku kuhusu kuoa/kuolewa bila kufahamu hayo ni maisha yao wenyewe. Pamoja na msisitizo mkubwa kutoka kwa wazazi/mzazi wanapaswa kuwa makini na kumwomba Mungu awasaidie kumpata mtu sahihi.

Wazazi wengine hutaka matarajio yao yatimie kwa mtoto wao, yule mwanaume/mwanamke wanayemtaka wao awe mume/mke wa mtoto wao. Wanataka iwe hivyo, bila kujalisha anampenda au hampendi, wao hutaka awe mume/mke wake.

Wanasahau ikiwa mtoto wao hatampenda huyo wanayemwona wao anafaa, watakuwa wamempa mzigo mzito kwenye maisha yake ya ndoa, pili watakuwa wamempa shida yule anayeolewa au anayeoa.

Tufanye nini wazazi? Tunapaswa kuwaeleza watoto wetu umuhimu wa kuoa na kuolewa kwa upendo, lingine tunapaswa kuwaombea sana, upo uzito usio wa kawaida ndani yao. Uzito ambao huwezi kuondolewa kwa nguvu na hekima za kibinadamu.

Mambo wanayokutana nayo na kuyaona kwa macho yao ni mengi sana, yapo mafundisho mengine mabaya yanawafanya wasione umhimu wa kuwa na ndoa ya mke na mume wa jinsia tofauti na yake.

Kazi yetu kuu iwe kuwafundisha na kuwaombea sana, Shetani asipate nafasi kwenye eneo hili, tutaona wakioa na kuolewa na watu wazuri na matamanio yetu kama wazazi yatakuwa yametimia kwa mapenzi ya Mungu.

Waoaji na waolewaji wanapaswa kumwomba Mungu na kuhakikisha yule anayeingia naye kwenye ndoa anakuwa amempenda kweli na sio msukumo tu wa mzazi au ndugu au rafiki umemfanya amkubali huyo mwanaume/mwanamke.

Wazazi au ndugu wanaweza kutusaidia kuona umuhimu wa kuoa na kuolewa ila tunapaswa kuwa makini kuhakikisha wale tunaoingia nao kwenye ndoa ni watu sahihi ambao tunawapenda kutoka ndani ya mioyo yetu.

Ukiyafahamu haya kama kijana hutaingia kwenye ndoa usiyoipenda, hata kama wazazi watakuwa na msukumo wa kutaka umuoe/uolewe na fulani, utakuwa unajua namna ya kuzungumza na mzazi na kukuelewa.

Mungu asaidie kizazi chetu

Samson Ernest

+255759808081