Imezoeleka kwa watu wengi sana wakisema usioe mwanamke mzuri sana atakutesa maana wengi sio waaminifu katika ndoa. Hii imewafanya wanaume wengi akitaka kuoa anatafuta mdada yeyote ambaye moyoni mwake sio chaguo lake halisi, ila amefanya hivyo kujiepusha na zile kauli za watu.
Ukweli ni kwamba idadi ya wadada wengi wanaonekana wana sura nzuri, huwa wanapata shida sana kuolewa kutokana na mitazamo ya watu/jamii. Hasahasa ukute dada yule hajiheshimu yaani kila anayekuja anamkubalia kufanya naye uasherati, kwake inaondoa heshima na kuonekana ni malaya.
Shida sio uzuri wa mwanamke, ni vile mwanamke yule anavyojiweka, mwanamke mzuri wa sura na umbo akiwa hana Yesu moyoni ujue hilo ni jipu litakusumbua. Hii ni kwa mwanamke yeyote yule, awe mzuri sana au wa kawaida kwa jinsi unavyomwona wewe, kama hana Yesu moyoni ujue atakusumbua tu.
Mwanamke kuwa mzuri wa sura na kuwa na umbo namba nane, haaminishi kuwa sio mwaminifu wala haimanishi mwanamke yule ni wa kuogopwa. Mungu ndivyo alivyomuumba, wala hajasema ukiona mwanamke mzuri wa sura na umbo ujue ni kahaba/malaya.
Mwili wake na sura yake visikutishe, unachopaswa kuangalia wewe ni uhusiano wake na Mungu, unachopaswa kuangalia moyoni mwako unasikia amani juu yake. Ikiwa una mashaka juu yake ni bora usihangaike kupoteza muda wako na mtu ambaye huna imani naye.
Lakini suala la kusema wanawake wazuri sio wa kuoa na kuweka ndani, huo ni mtazamo hasi ambao haupo kibiblia. Ila upo kimazingira ya kimwili ambayo Labda umeona watu wakisema vibaya au limekutokea mwenyewe umeumizwa. Hapo unapaswa kuelewa kilichokuumiza sio sura na umbo lake, kilichokuumiza ni tabia mbaya iliyo ndani yake.
Wakati mwingine hawa dada zetu wameharibika kwa zile sifa wanazopata, sasa asipokuwa na mahusiano mazuri na Mungu anajikuta zile sifa zinamharibu. Na siku zote sifa zimeharibu wengi kwa kuwajaza viburi, na wengine kujiona wao ndio wao hakuna mwingine zaidi yao.
Kitu kingine kinachoweza kuwatia watu mashaka wanapoona mwanamke mzuri wa sura na umbo, ni pale mwanamke huyu anapovaa mavazi yasiyo na heshima mbele ya jamii inayomzunguka. Hapa ndipo lipo tatizo la wengi sana, mavazi yana mchango mkubwa sana kumtafsiri mtu alivyo ndani yake.
Wabaya wachache hawawezi kuondoa sifa ya wanawake wazuri wa sura na umbo kuonekana wote ni malaya, au kuonekana wana matumizi mabaya ya pesa. Hiyo ni tabia ya mtu mwenyewe, yeyote anaweza kuwa na matumizi mabaya ya pesa kama atakuwa ameruhusu kuendeshwa na hiyo hali. Lakini wapo wana nidhamu katika matumizi na uzuri wao umebaki palepale.
Biblia imeweka wazi kabisa wapo wanawake/wadada wazuri wa sura na umbo, hili tumelithibitisha kwa Ester binti aliyekuwa na bikira safi kabisa pamoja na uzuri wake wote hakuharibu sifa yake. Bali aliendelea kuwa mwaminifu mbele za Mungu bila kujiona yeye ndio yeye.
Rejea; *Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo mzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake yeye. EST. 2:7 SUV.*
Haleluya, umeona Biblia ilivyowazi kabisa, unaweza kuona ni kiasi gani unaweza kulishwa uongo na wewe ukaukubali. Pata kitu moyo unapenda, sio unajing’ang’aniza kwa mtu ambaye huwezi hata kumpa neno zuri la kumsifia, kumbe huna ile furaha ya kutoka ndani moyo wako.
Hebu tufute mitazamo hasi isiyo na ukweli wowote juu ya mahusiano yetu na Mungu, biblia imebeba majibu ya maswali yetu. Umeona mwenyewe jinsi Ester alivyomwagiwa sifa zake za uzuri, biblia haijasema tu huo uzuri ulikuwa wa rohoni la hasha ulikuwa uzuri wa uso na umbo.
Mungu akubariki sana kwa kuchagua kuijua kweli, hivi vitu usipokuwa msomaji wa Neno la Mungu huwezi kuvipata. Lakini wewe unavipata kwa sababu unatoa muda wako kusoma Neno la Mungu.
Unahitaji kujiunga na group la whatsApp la kusoma Neno la Mungu kila siku? Tuandikie ujumbe wenye majina yako kamili kwenda hizo namba nilizotoa hapo chini.
Nakutakia wakati mwema wa kuendelea kutafakari ukuu wa Mungu.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
www.chapeotz.com