Kila mmoja ana njaa na kiu yake katika maisha, yupo mtu ana njaa na kiu ya kufaulu mitihani yake shuleni/chuoni, yupo mtu ana kiu ya kufanikiwa katika kazi yake, yupo mtu ana kiu afanikiwe kupata mke/mume, yupo mtu ana kiu apate mtoto kwenye ndoa yake.

Yupo mtu ana njaa na kiu ya kukua zaidi kiroho, yupo mtu ana njaa na kiu ya kufanikiwa katika usomaji wake wa Neno la Mungu.

Yupo mtu ana njaa na kiu ya kuja kuwa rais siku moja, yupo mtu ana njaa na kiu ya kuwa mbunge wa jimbo fulani, yupo mtu ana njaa na kiu ya kupata kazi fulani, yupo mtu ana njaa na kiu ya kuja kuitwa meneja kwenye kampuni fulani.

Yupo mtu ana njaa na kiu ya kuja kuwa mtangazi bora kabisa wa radio/Tv fulani, yupo mtu ana njaa na kiu ya kuwa mwandishi wa habari.

Njaa na kiu zipo nyingi sana, inategemeana na mtu ana uhitaji gani kwa muda au nafasi au mazingira aliyonayo wakati huo.

Sasa leo nikuulize katika njaa na kiu zako zote hizo, je njaa na kiu ya mambo ya Mungu ikoje kwako, maana Neno la Mungu linasema; wale wenye njaa na kiu ya haki watasibishwa.

Rejea: Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. MT. 5:6 SUV.

Kumbe wenye njaa na kiu ya haki, wakiwa wavumilivu na wakatulia vizuri na Mungu. Lazima watu hawa wapate haja ya mioyo yao.

Mara ngapi tumekuwa na njaa na kiu ya haki, mara ngapi unasikia msukumo wa kwenda ibadani, mara ngapi unasikia msukumo wa kusoma Neno la Mungu, na mara ngapi unasikia njaa na kiu ya maombi.

Kama huna njaa ya hivyo vitu, Mungu hawezi kukushibisha kitu usichokihitaji kiwe kwako. Mungu anawashibisha wale wahitaji, yaani wale wenye njaa na kiu ya haki.

Usishangae unazidi kumwona mtu fulani unayemfahamu, Mtu huyo anazidi kuwa viwango vya juu zaidi kiroho/kihuduma.

Kuwa na viwango vya juu zaidi sio kana kwamba imetokea ghafla, ipo gharama kubwa mno mtu anakuwa ameitoa hadi kufikia malengo hayo makubwa.

Nimalize kwa kusema kwamba, kile una njaa na kiu nacho ndicho utakachokipokea ilimradi kiwe katika kusudi la Mungu na kisiwe kinamkosea Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com