Kuepuka maadui katika maisha yetu ya kila siku, katika huduma, katika masomo, katika biashara, katika kazi, katika familia, na katika ndoa. Inaweza isiwe rahisi sana kukwepa haya yote katika maisha yetu.

Tunaweza kukazana kumpendeza Mungu wetu, kumbe tunavyozidi kukazana kumpendeza Mungu wetu ndivyo tunavyozidi kuongeza maadui zaidi.

Tunavyozidi kusimama katika kweli ya Mungu, badala ya kuwapendeza watu wapo ambao wanakuwa hawapendezwi na vile tunasimamia kweli ya Mungu.

Tunaweza kukazana kufanya vizuri katika maeneo yetu ya kazi, badala ya wengine kupendezwa waje wajifunze mambo mazuri kutoka kwetu. Tunainua maadui wenye chuki dhidi yetu, sababu haswa ya msingi unakuta hakuna ni wivu tu.

Unaweza kusimama vizuri katika huduma yako aliyokupa Mungu wako ndani yako, utafanya kwa bidii zako tena ukigusa maisha ya watu wengi. Kadri unavyozidi kugusa maisha ya jamii kupitia kile Mungu ameweka ndani yako. Hapo ndipo unazidi kuzalisha maadui zako wengi.

Hakuna mahali utasimama na Mungu wako vizuri pasiwepo na maadui zako, tena maadui wanaokuwazia mabaya juu yako. Maadui ambao wapo tayari kuutoa uhai wako ili mioyo yao ifurahie.

Usifikiri unavyofurahia maisha yako na mume/mke wako, watu wanafurahia sana, kadri unavyozidi kupendana na mwenzi wako. Ndivyo unavyozidi kutengeneza maadui zako wengi tu, na usiposimama vizuri na Mungu wako utajikuta amani yenu imevurugwa.

Hatuwezi kujificha kuepuka maadui zetu, tupo duniani tutakutana na mambo kama haya. Popote ulipo ukisimama vizuri tayari umetengeneza maadui kwenye eneo hilo.

Rejea: Walio adui zangu bila sababu Wameniwinda sana kama ndege; Wameukatilia mbali uhai wangu gerezani, Na kutupa jiwe juu yangu. Maji mengi yalipita juu ya kichwa changu, Nikasema, Nimekatiliwa mbali. Naliliitia jina lako, BWANA, kutoka lile shimo Liendalo chini kabisa. Ukaisikia sauti yangu; usifiche sikio lako Ili usisikie pumzi yangu, kwa kilio changu. Ulinikaribia siku ile nilipokulilia; Ukasema, Usiogope. OMB. 3:52‭-‬57 SUV.

Jambo la kuzingatia ili kubaki kuwa salama, hakikisha uhusiano wako na Mungu upo vizuri. Maisha yako yote yawe maisha ya kumtegemea Mungu wako, maisha yako yote yawe maisha ya maombi.

Unapokutana na mambo magumu, unapofika mahali unaona vita vimeinuka juu yako…hakikisha unaanza kupambana navyo katika ulimwengu wa kiroho na si kwa damu na nyama.

Hakikisha hupungukiwi na chakula chako cha kiroho, ambacho ni Neno la Mungu, hii ni silaha muhimu sana kukusaidia kupambana na maadui zako.

Ukiwa msomaji mzuri wa Neno la Mungu na ukawa mwombaji mzuri, hata kama maadui zako watapanga nini juu ya maisha yako. Hawataweza kukuondoa uhai wako, Mungu asiporuhusu hilo.

Njia salama na ya uhakika ya kupambana na maadui zako, ndio hii niliyokueleza, hakikisha uhusiano wako na Mungu upo vizuri. Huhitaji kutafuta waganga wa kienyeji, unamhitaji Yesu Kristo pekee.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.