Je unaona picha ya nini katika maisha yako, wewe ni kijana je unaiona picha ya ndoa yako itakavyokuwa baada ya kuoa/kuolewa na huyo mtu.
Unapomuomba Mungu kwa jambo fulani, kumbuka kwamba utapewa picha ya jinsi itakavyokuwa, kabla Mungu hajakupa maelekezo ya jinsi gani utafanya ili ile picha ionekane kwa uhalisia katika maisha yako.
Vijana wengi huwa wanasema wameonyeshwa wenza wao wa maisha, lakini swali la kujiuliza je! Ulishawahi kuonyeshwa picha ya maisha yako baada ya kuwa umeshaingia kwenye ndoa, hata kabla hujampata huyo mtarajiwa wako?
Nina ujasiri wa kulizungumza hili maana ni ushuhuda wangu wa maisha, mara nyingi Mungu alikuwa akiniletea picha ya maisha yangu ya ndoa, hata kabla sijachumbiwa na sijajua ni nani atakuja kuwa mume wangu.
Hivyo nilizidi sana kumwomba Mungu kwa habari ya maisha yangu, na ninamshukuru Mungu, kile ambacho nilikiona miaka 9 iliyopita ndicho ninachokiona sasa kwenye maisha yangu.
Ni mengi ambayo naweza kuyashuhudia hapa, lakini ni jambo muhimu sana kukaa na kutulia mbele za Mungu, Yeye husema na watu wake kwa njia tofauti tofauti hivyo ni wewe tu na usikivu wako mbele zake.
Ishi maisha matakatifu, ishi maisha ya ibada, epuka makundi yanayokuvuta nyuma, unakosa hata muda wa kutulia wewe na Mungu, huu ndio wakati wako wa kumtafuta Mungu kwa bidii kijana/binti ambaye haujaingia kwenye ndoa bado.
Hata Musa alionyeshwa picha ya jinsi gani hema itakuwa, na inawezekana haikuwa wakati mfupi baada ya kuona ile picha na mpaka kuja kupewa maelekezo namna ya kuitengeneza ile hema na iwe vile vile kama alivyoiona.
Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake ulioonyeshwa mlimani. KUT. 26:30 SUV.
Musa alipewa maelekezo ya namna ya kutengeneza hema, lakini si kwamba ilimradi tu iwe hema, bali iwe sawasawa na mfano wa ile aliyoonyeshwa kule mlimani.
Kumbuka pia hata katika ule UFUNUO WA YOHANA, Yohana alipewa kuona hayo ili kuliandaa kanisa, na kulijulisha kwa habari ya mambo yatakayotokea baadae, hiyo ilikuwa picha ambayo katika baadhi ya mambo yanaanza kutimia.
Na usifikiri kwamba ukishaona tu ile picha ukafikiri kwamba mambo yatajiseti menyewe, hapana wewe mwenyewe unapaswa kusimama na Mungu ili akupe maelekezo na jinsi gani hiyo picha itakuja kuwa halisi kwenye maisha yako, omba Mungu mpaka ndoto yako itimie.
Mungu pamoja na kuonyeshwa ni jinsi gani ilivyo, lakini tunaona akipewa maelekezo, vitu gani atumie, aina ya vitambaa, aina ya miti, aina za rangi na kila kilicho hitajika kwa aina yake.
Hivyo kuna prosses ndefu ili kuweza kukamilisha na kuwa kitu halisi chenye kuonekana kwa macho, hapo njiani utakutana na vikwazo vya kila namna, lakini Mungu atakutetea mpaka utafikia hatima yako, usichoke wala kukata tamaa.
Mungu akubariki sana.
Rebecca Ernest.