Tunaweza kuona bora kufika kwenye vyombo vya sheria, tukaona huko ni salama zaidi na waliotushitaki hawataweza kutufanya kitu chochote. Tunawaacha watufikishe kwenye mikono ya sheria ila kama kweli walitushitaki kwa kosa tulilolitenda kweli, kuingia kwenye mikono ya sheria ni rahisi ila kutoka ndio ngumu.

Ni afadhali sana kupatana na mshitaki wako mapema kabla hajakufikisha kwenye vyombo vya sheria, ukishamwacha akakufikisha huko. Uwe na uhakika kama alikuwa anakudai shilingi 10,000. Utailipa yote na gharama zote za usumbufu.

Kupatana na mshitaki wako kabla ya kufika kwenye mahakama ni bora zaidi, kama haina ulazima wa kufikishwa kwa hakimu. Ni bora mkamalizana njiani na mshitaki wako, kuliko kujifanya mbabe, ukamwacha akufikishe mahakamani kwa Hakimu.

Rejea: Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani. Nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho. LK. 12:58‭-‬59 SUV.

Unaposubiri mshitaki wako akufikishe mahakamani, uwe na uhakika utatupwa ndani, tena ukutane na mshitaki wako anataka kukulipiza yale uliyomtendea. Na ukakutana na hakimu anayeamua kwa haki, nakwambia kama ulikuwa unadaiwa utalilipa hilo deni hadi senti ya mwisho.

Ndivyo ilivyo kwenye ufalme wa Mungu, sasa hivi ukiwa hai unayo nafasi ya kutengeneza maisha yako, ukisubiri siku ya hukumu, hutakuwa na hiyo nafasi tena ya kujitetea. Kitakachofuata ni kutupwa kwenye ziwa la moto.

Patana na mshitaki wako mapema, acha dhambi na uokoke, usisubiri siku umekufa, hutokuwa na uwezo wa kutubu tena, kitakachofuata ni hukumu ya milele.

Patana na mshitaki wako kabla ya siku ya mwisho, ukiisubiri hiyo siku ya mwisho ifike hutokuwa na nafasi tena ya kuokoka. Milango itakuwa imeshafungwa ila kwa sasa ipo wazi, ni wewe kuamua kuchukua hatua ya kupatana na Yesu mapema.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255759808081