Zoezi hili linaweza kuwa gumu kwako, hasa ukizingatia labda umewahi kumwonya mtu kuhusu matendo yake maovu. Alafu mtu yule aligeuka adui yako mkubwa kwa kukuona unamfuatilia maisha yake.

Kuambiwa umekosa kazi ya kufanya baada ya kumwonya mtu, tena ulimwonya kwa nia njema ila ulichoambulia ni tofauti kabisa na matarajio yako. Inaweza kukuvunja sana moyo na kuona bora kukaa kimya hata unapoona ubaya ukitendeka.

Kukaa kimya huku ukiona uovu ukitendeka na wewe umeokoka, uwe na uhakika wakifa katika uovu wao, hizo damu za hao watu utadaiwa mikononi mwako. Usifikiri upo salama kujiepusha mbali na hao ndugu wanaotenda uovu na wewe unajua hilo ni chukizo mbele za Mungu. Uwe na uhakika damu zao utadaiwa mikononi mwako.

Mungu anakataza watu wasiabudu miungu mingine kama vile ndama/ng’ombe, alafu unaona watu wanaabudu hivyo vitu. Usiogope kusema ukweli, usiogope kukemea hiyo tabia, wasikie ama wasisikie, wewe huna hatia kuhusu hilo.

Unajua Mungu anakataza kabisa watu kuabudu sanamu za aina zozote zile, alafu leo unamwona ndugu yako au watu wengine wanafanya hivyo. Usisite kuwaeleza ukweli, wasikie ama wasikie, wewe utakuwa umenawa mikono.

Mungu anasema ili uingie mbinguni ni lazima uwe umazaliwa mara ya pili, kwa maji na kwa Roho. Alafu ukaona watu hawafuati kama Mungu alivyoelekeza, usisite kuwaambia ukweli.

Haijalishi watakubaliana na wewe ama hawatakubaliana na wewe, usisite kuisema kweli ya Mungu wako aliyekutuma. Ukiona tabu kusema, kumbuka damu zao utadaiwa mikononi mwako.

Rejea: Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako. Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake, na kutenda uovu, nami nikiweka kikwazo mbele yake, atakufa; kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu wake, wala matendo yake ya haki aliyoyatenda hayatakumbukwa; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Bali ukimwonya mwenye haki, kwamba yule mwenye haki asitende dhambi, tena ikiwa yeye hatendi dhambi, hakika ataishi, kwa sababu alikubali kuonywa; nawe umejiokoa roho yako. EZE. 3:18‭-‬21 SUV.

Kuanzia sasa jifunze kunawa mikono yako kwa jambo lolote lile unaloliona linatendeka kinyume na mapenzi ya Mungu. Usikubali kuja kudaiwa damu ya mtu yeyote mikononi mwako, hata kama ni ndugu yako, usisite kumwambia kweli.

Ipo gharama ya kueleza ukweli ila usisite kupaza sauti yako, kazi yako ni kuisema kweli ya Mungu. Kazi inabaki kwao, wafuate ulichowaelekeza ama wapuuze kile umewaelekeza. Wewe Unakuwa umenawa mikono yako.

Kunyamaza kimya kwa kisingizio chochote kile, kumbuka hili; damu yake nitaitaka mkononi mwako. Huyu ni Mungu mwenyewe anasema haya, sijui kama utaona haya tena kuisema kweli ya Mungu wako.

Tumekubaliana wote hapa, haijalishi wataupokeaje huo ukweli unaoueleza kwao, hakikisha unausema bila kupindisha maneno. Ataamua mtu mwenyewe kukubali au kukataa kile umemwelekeza.

Paza sauti yako usinyamazie kimya uovu wao, kunyamaza kimya utasababisha udaiwe damu zao mikononi mwako.

Mungu atusaidie sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081