Wengi wetu tumekuwa tukiona kutabiriwa ni jambo moja la mhimu sana katika maisha yetu, na tumeona anayetutabiria huyo ndio nabii wa Mungu wa kweli.

Hili jambo limeteka kanisa kwa kasi kubwa sana, na kuwafanya watu wengi waingie kwenye mtego wa upotovu na kuiacha njia ya Mungu.

Imani nyingi potovu zimeibuka na huu mchezo wa kutabiri, ndio fursa aliyoiona shetani kuliteka na kulisambaratisha kanisa.

Mpango huu umefanikiwa kiasi chake, japo wachache wao Mungu anawafunulia na kuwaondoa kwenye madhabahu za kipepo.

Labda ulikuwa hujui kuwa kuna pepo la utambuzi, hili linaweza kujua mambo yako yote…iwe ofisini/biashara yako linajua. Iwe kwenye eneo lako lolote la maisha yako ilimradi unauhitaji huo litakutambua na kukupa taarifa zote.

Nia yangu sio kukupa injili za mapepo ila nataka kufungua ufahamu wako juu ya maisha yako. Ujue uchukue hatua gani hapo ulipo.

Inaumiza unamwona ndugu/rafiki yako anaingia kwenye mtego huu wa kukimbilia manabii wanaotabiri kutumia nguvu za giza, sisemi hakuna manabii wa Mungu wanaotoa unabii wa kweli. Wapo tena Mungu anawatumia vizuri tu.

Sasa utawezaje kumjua nabii wa kweli na wa uongo, lazima umjue Mungu sana, lazima usome neno la Mungu kwa bidii na kuliweka moyoni mwako.

Unaweza kusema labda huyu naye anaongea nini wakati jana tu nimetoka kutabiriwa maisha yangu…sawa ulikuwa na shida sasa imetatuliwa kupitia huyo mtumishi, swali langu kwako je umetabiriwa na Roho wa Mungu au na pepo la utambuzi.

Naona hunielewi, nasema hivi Sauli baada ya Mungu kumwacha na kukaa kimya alianza kumtafuta mtu wa kumtabiria. Akampata mwanamke mwenye pepo la utambuzi.

Soma; 1 Samweli 28:7-9.
[7]Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori.
[8]Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye na watu wawili pamoja naye, wakamfikilia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukanipandishie yeye nitakayemtaja kwako.
[9]Yule mwanamke akamwambia, Angalia, unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili kuniua?

Kama ni msomaji mzuri wa biblia utakuwa unamjua vizuri Sauli, alikuwa anatumiwa sana na MUNGU kwenye nafasi yake ya ufalme kabla hajamkosea. Lakini baada ya kumkosea Mungu, Mungu alimtupia roho mbaya na Daudi akaenda kupakwa mafuta na Nabii Samweli kuja kukalia kiti cha Sauli.

Hapo mwanzo ilionekana Sauli aliwapinga vikali watambuzi lakini baada ya Mungu kujitenga naye aliamua kuwatumia tena.

Najua umekutana na haya kwa namna moja ama nyingine, ni mambo ambayo yapo maana biblia imeweka wazi kabisa.

Neno linasema; Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Mathayo 24 : 24.

Huenda ulikuwa husikii wala huambiliki kuhusu haya mambo, kuanzia leo ufahamu wako utiwe nuru kwa maneno haya.

Ukiwa una nia ya kuishi maisha mengine ya umilele baada ya haya, hakikisha sehemu unayoabudia ni salama. Hakikisha jina la Yesu linatukuzwa na si mtu anatukuzwa.

Hakuna sehemu kwenye biblia inayoonyesha atatokea Yesu mwingine, zaidi ya hao makristo wa uongo.

Safari yako inamhitaji Mungu sana kuliko unavyochukulia, ombi langu kwa Mungu, uimalize safari salama.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com
+255759808081.