Moja ya matukio ambayo yanasisimua, na yaliyoonyesha ujasiri mkubwa, ni hili tukio la mwanamke kipofu, ni tukio ambalo linagusa maisha ya wengi pale mtu anaposikia mafundisho/mahubiri yake.

Sifa kuu ya huyu mwanamke kipofu, alijulikana kipofu, na sifa ya pili alijulikana kama omba omba, kwahiyo unaweza kuunganisha sentensi hapo na kumwita yule kipofu ombaomba. Ambapo sifa hii haikuwa njema kwake, na bila shaka alishasikia habari za Yesu Kristo ila hakuwahi kuonana naye, siku anapita mahali pale alipokuwa, kwanza aliuza hizo kelele ni za nini? Jibu, ni Yesu anapita.

Alivyosikia Yesu Kristo anapita, hatua nyingine aliyopiga huyu mwanamke kipofu ni kupiga kelele, sijui kama unaelewa vizuri maana ya kupiga kelele, bila shaka utakuwa unaelewa unaposikia kelele. Kelele ina tofauti na mtu anayeita kawaida, mpaka iitwe kelele ilikuwa kubwa kweli.

Huyu mwanamke hakuona aibu, maana tayari alikuwa nayo tayari hiyo aibu, huyu mwanamke hukuangalia watu wangapi wanakerwa na sauti yake ya juu(makelele). Yeye alichojua huyu mwanamke ni kupiga kelele za kumhitaji Yesu Kristo.

Nikakumbuka leo nikiwa mahali kwenye kusanyiko fulani, mtu mmoja nilikuwa karibu naye, wakati kiongozi anahutubia huko mbele. Yeye alikazana kunyoosha mkono katikati ya mazungumzo ya huyu kiongozi, niliona sio vyema kukaa kimya, nilimwambia huyu ndugu asubiri amalize kuongea na aruhusu maswali, ndipo atanyoosha mkono.

Huyu ndugu hakunielewa, yeye aliendelea kunyoosha mkono wake katikati ya kundi kubwa, hakuchukua muda yule kiongozi alimruhusu aongee. Maana tayari alishauona mkono wake muda mrefu, baada ya kuruhusiwa kuongea, na maneno aliyokuwa anamwambia kiongozi yule. Nilijua sababu ya yeye kufanya hivyo, japo hakuwa na subira.

Wakati naendelea kutafakari hilo, andiko hili takatifu ninaloenda kukushirikisha hapo chini, lilinijia kichwani, na kuona kuna wakati kumbe mtu anaweza kuzuiwa kupaza sauti mahali ambapo alikuwa anaona anaweza kupata majibu ya shida yake.

Rejea: Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu. LK. 18:35‭-‬43 SUV.

Hebu tafakari mara ngapi umeshindwa kupaza sauti yako juu ya Bwana, mahali pale ulipofika ukaona kuna upinzani mkubwa, mara ngapi umeona aibu kupeleka hitaji lako mbele za Mungu?

Utaona ni mara nyingi sana umeona aibu/haya kupiga kelele wakati Yesu Kristo yupo kwenye uponyaji, wakati mwingine umeona aibu kwenda kuombewa na watumishi wa Mungu kwa kuwatazama wengine watakuonaje.

Inawezekana kabisa kutokana na umaarufu wako, umeshindwa kujitosa kwa Yesu Kristo mbele za watu kutokana na umaarufu wako, bila kujua umaarufu wako hauwezi kukuponya, wala huwezi kukuondolea shida yako.

Inawezekana kabisa yupo mtu ameshindwa kumfuata Yesu Kristo, kwa kuacha mambo ya Dunia, kwa kufikiri watu watamwonaje akiokoka wakati yeye ni mtu mkubwa mbele ya jamii. Kinachosikitisha ni kwamba, cheo chake kimeshindwa kumwondoa kwenye utumwa wa dhambi, na utumwa wa magonjwa.

Laiti huyu mwanamke angeona aibu kupiga kelele, na angesikiliza mazuio ya watu, Yesu Kristo asingeweza kumwona kutokana na msongamano wa watu. Ile imani yake ya kutaka kupokea uponyaji kutoka kwa Yesu Kristo, hakuishia pale, aliamua kuchukua hatua ya pili ya kupiga kelele.

Ambapo na wewe unaweza kuchukua hiyo hatua ya kumwita Yesu Kristo aje akusaidie kukuondolea shida yako, aje akuponye na ugonjwa wako, aje akuponye na majeraha ya moyo wako. Inawezekana kabisa ukichukua hatua ya kupiga kelele baada ya kusikia hapa, Yesu Kristo anapita.

Mwite Yesu Kristo asikupite saa hii mama, kaka, dada, baba, muujiza wako Yesu Kristo ameubeba, ni wewe kuamini na kuchukua hatua ya pili kumwita na kumweleza unataka akufanyie nini.

Sio upige kelele za kumwita Yesu Kristo, alafu akishakuja na kukuuliza unahitaji akutendee nini, wewe unabaki kupiga kelele bila kumwambia unahitaji nini. Yesu anataka umwambie unataka akufanyie nini, akuponye, akupe amani kwenye ndoa yako, akupe mke/mume, nini unataka kwake, eleza haja ya moyo wako naye atakutendea sawasawa na mapenzi yake.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com