Sio ajabu siku za leo kukutana na kijana wa umri mkubwa akieleza kwa uwazi kabisa bila hofu kuwa hayupo tayari kuingia kwenye ndoa, na ukimweleza habari za kuoa/kuolewa anakwambia hayupo tayari kuingia kwenye ndoa, unaweza ukafikiri anatania ila wengi huwa hawatanii, huwa wanamaanisha wanachosema. Kutokutaka kuingia kwenye mahusiano ya ndoa kunasababishwa na mambo mengi ila leo tunaenda kuangalia baadhi ya sababu zinazoweza kumfanya kijana asitake kuoa/kuolewa.
Zifuatazo ni sababu 5 kwanini baadhi ya vijana hawataki kuoa/kuolewa;
- Kuumizwa Na Mahusiano Yaliyopita
Wapo vijana wamekutana na changamoto hii ya kujeruhiwa na watu waliowaamini sana watakuwa wenzi wao wa maisha badala yake ikawa kinyume chake, wakabaki na maumivu ambayo yamesababishwa na kutosamehe yale waliyofanyiwa.
Wengine wamepitia changamoto ya kuachwa mfululizo, pale alipoamini amekutana na mtu sahihi baada ya siku kadhaa inatokea shida ileile ya kuwatenganisha wawili hao. Inafika kipindi anaona haina haja ya kuendelea kuumizwa na mahusiano.
Dawa ya hili ni kuchukulia kuachwa kwa hali ya kujifunza, muhanga wa hili anapaswa kukaa chini na kujiuliza kwanini mahusiano yake ya uchumba yanaharika mara kwa mara, je chanzo ni yeye? Kama sio yeye nini huwa inasababisha kuachana, inawezakana sio mpango wa Mungu ila huwa anajiingiza kwenye mahusiano kienyeji bila kuwa na uhakika na anayetaka kuishi naye.
2. Kuwa Na Mahusiano Ya Mapenzi
Hili ni janga kwa baadhi ya vijana, wapo vijana wanaonyesha hawana uhitaji wowote wa kuoa/kuolewa kwa sababu wanafanya uasherati/uzinzi. Wanaona haina haja ya kuingia kwenye ndoa wakati huo.
Huyu kijana unaweza kumkuta ni mshirika ila matendo yake ni machafu, anatembea hovyo na wanaume/wanawake, huwa wanafanya kwa siri sana wasijulikane na watu wengine. Wanaoweza kujua hili ni watu wake wa karibu mno au majirani wanaomwona.
Hii inatokana na mtu kukosa hofu ya Mungu, na kutokuwa siriazi kwenye maisha ya wokovu, mtu akishakosa hofu ya Mungu ndani yake ni rahisi sana kufanya uasherati, sasa mtu anayefanya uasherati anaweza asione umhimu wowote wa kuoa/kuolewa.
Neno la Mungu linatuweka wazi kuwa; Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa. 1 Kor 7:9 SUV
Kama mtu hajaoa/hajaolewa na ameshindwa kujizuia akaona ni vyema kuwa na mahusiano yanayomkosea Mungu, mtu huyo anatenda dhambi, bora kuoa/kuolewa kuliko kufanya uasherati/uzinzi.
3. Kuwa Na Mtazamo Mbaya Juu Ya Mahusiano
Mitazamo mibaya juu ya mahusiano ya ndoa wakati mwingine inaletwa na watu walioshindwa kwenye ndoa zao, kama mtu atamsikiliza aliyeshindwa kwenye ndoa yake na anayemsikiliza hana neno la Mungu la kutosha uwe na uhakika mtu huyo atachukia kuoa/kuolewa.
Kama mtu atachukia kuoa/kuolewa na hana uwezo wa kujizuia, utarajie mtu huyo kuwa na tabia mbaya isiyompendeza Mungu, atakwambia hataki habari ya kuoa/kuolewa ila utamkuta ana mahusiano ya kimapenzi na wanaume/wanawake.
Kila mmoja anapaswa kujua kuoa/kuolewa ni mpango wa Mungu, pia ndoa ni taasisi ya Kimungu kabisa ambayo kila mmoja kabla ya kufanya maamuzi hayo anapaswa kumwomba Mungu amsaidie. Tukielewa kuwa ndoa ni taasisi ya Mungu ile mitazamo mibaya tuliyokuwa nayo itatuondoka na tutaona umhimu wa kuoa na kuolewa.
4. Uchumi mbaya
Hili linaweza kuwa tatizo la baadhi ya vijana kuona hapaswi kujiingiza kwenye ndoa kutokana na hali yake ya uchumi, au kuwakataa wanaume wanaomjia alafu uchumi wao upo chini. Pia wapo vijana wa kiume wanakutana na changamoto ya kukataliwa na mabinti kutokana na hali zao duni za uchumi.
Wengine wanashindwa kuoa kutokana na kukosa mahari, anaona ngoja apambane hadi apate mahari ndipo aoe, hii inawaingiza wengi kwenye shida. Maana anaweza kujiingiza kwenye mahusiano na kuanza kuishi na mwanaume/mwanamke, hii ni baadhi na wengine huendelea kukaa bila kuoa.
Suluhisho la hili ni kijana mwenyewe kutokuwa na hofu ikiwa ana shughuli anafanya na inamuingizia kipato kidogo, kupitia hiyo shughuli anayoifanya aendelee kuifanya kwa bidii Zaidi na Mungu atambariki na kumpa hatua nyingine kubwa.
Kijana awe wazi na asitake kujiingiza kwenye mahusiano na mtu ambaye anaona maisha yake ni ya juu sana, msikilize Roho Mtakatifu anavyokuelekeza nani wa kuishi na wewe. Usiongozwe na hisia zako na akili zako, ruhusu mapenzi ya Mungu kwako.
5. Kuchagua Sana
Hili linaweza lisionekana kama ni tatizo kwa wengi ila ni chanzo kimojawapo cha kuwafanya vijana kuchelewa kuoa/kuolewa, kuna watu wanachambua sana wale wanaofikiri wanaweza kuishi nao. Bahati mbaya wanafanya uchaguzi kimwili kabisa hawaangalii mpango wa Mungu juu ya huyo anayetaka kuishi naye, wanajikuta kila anayekuja kwao ana kosoro nyingi.
Unafika umri Fulani wanaanza kulalamika kuwa wanaume hawataki kuwaoa wanataka kuwachezea tu, wamesahau kuwa hawakumsikiliza Mungu wakati amewaletea watu sahihi kwao. Hili linawezekana kuepukwa kwa vijana, kama kila mmoja ataelewa hakuna aliyekamilika ila tunapokuwa pamoja tunakamilishana kwenye yale mapungufu yetu.
Ukipata mtu sahihi kwako haijalishi ana mapungufu mengi atakufaa na wewe unamfaa, na ndoa yenu itakuwa ya furaha na Amani kwa sababu Mungu alikukutanisha na mtu wako sahihi. Sio hilo tu utaweza kulitumikia kusudi la Mungu alilokupa maishani mwako, maana kuna watu wameua makusudi ya Mungu maishani mwao kwa kukosea kuoa/kuolewa na mtu asiye sahihi kwao. Wamejikuta kile Mungu aliweka ndani yao kimezimwa na kupotezwa kabisa.
Mwisho, hizi ni baadhi tu za sababu zinazowafanya vijana wasitake kuoa/kuolewa, ninaamini umejifunza mengi mazuri na mengine Roho Mtakatifu amekuongezea sababu Zaidi ya hizi. Kusudi la kujifunza hizi sababu ni ili uweze kuchukua hatua kwa kuacha fikra potofu juu ya ndoa.
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081