Ndugu msomaji wangu, sio ajabu umekutana na mkasa huu wa kuachana na mchumba wako au rafiki yako siku ya sherehe au sikukuu fulani au tukio fulani maalumu. Kama sio wewe ulikutwa na hichi kisa basi utakuwa umeshuhudia matukio kama haya kwa vijana wenzako au kwa marafiki zako.

Huenda hujawahi kukaa chini ukafikiri huwa inatokana na nini, mfano tu jana kulikuwa na sikukuu ya wapendanao, japo wapo watu wanaopinga nayo na wapo wanaoikubali na kuianzimisha. Ukifuatilia utakuta wachumba kadhaa wameachana jana au kuna jambo lilitokea jana na limewapelekea hawasemeshani hadi sasa, au kuna ugomvi unaendelea kati yao.

Ugomvi ambao utawapelekea hadi kuachana kabisa, nimetoa mfano wa sikukuu ya wapendanao, sikukuu ni nyingi, kama vile Pasaka, Krismasi, mwaka mpya nk. Ipo sikukuu nyingine muhimu ya kuanzimisha siku ya kuzaliwa, hii nayo ina matukio yake, tutaizungumza zaidi hapa chini.

Tuende tukaangalie sababu hizi tano, kupitia hizi sababu zitakupa nafasi ya kufahamu mengi zaidi;

1. Kutomtakia heri ya siku ya kuzaliwa mwenzake.
Moja ya jambo linazuua taharuki kwa vijana walio kwenye mahusiano ni pamoja na hili, ukute mmoja wapo ni siku yake ya kuzaliwa na mwenzake akawa hajamtafuta kumtakia heri. Ama akawa hajaonyesha kumjali na kumpa zawadi, au akawa hajamposti kwenye status, au facebook, au instagram, hiyo kesi itakuwa ngumu sana kwa wawili hawa.

Niliopata nafasi ya kuongea nao, hutafasiri kitendo hicho kuwa hajajaliwa au mwenzake anamwona hana thamani kwake, ndio maana hakumbuki tukio lake la muhimu la kumbukumbu ya kuzaliwa kwake. Na kama anakumbuka anaonyesha kuwa hamthamini mwenzake, hizo ni moja ya hoja zinazoweza kuibuka ndani ya mtu.

Hili linaweza lisifanye kazi kwa mwingine au lisionekane ni jambo linaloweza kuleta shida kwenye mahusiano ila kwa wengine ni jambo kubwa na linachukuliwa kwa uzito mkubwa sana. Na kweli ukiingia ndani zaidi utajua kuna shida, inaweza ikawa mmoja amemchoka mwenzake, haoni tena umhimu wa kufanya yale mwenzake atafurahi.

2. Kuona wenzake wakifanyiwa mambo mazuri.
Katika sikukuu hizi huwa kuna mambo mengi sana walio kwenye mahusiano hufanya kwa ajili ya wenzao, wengine huwanunulia wenzao zawadi nzuri za kuvutia, na wanapofanyiwa hivyo huwa hawakai kimya. Hasa wadada, lazima atamwonyesha rafiki yake kile amenunuliwa na mchumba wake, sasa ukute yeye anayeonyeshwa hajafanyiwa kitu chochote, ujue hiyo ni kesi tayari.

Mmoja akishindwa kuchukulia kama jambo la kawaida na kumchukulia mwenzake, hiyo inaweza kuwa ni njiti ya kuwasha moto wa kuteketeza mahusiano hayo. Ukiipima sababu unaweza usiipate na kuielewa sana ila huo ndio ukweli uliofanya mahusiano hayo kuvunjika, au kunyamaziana kabisa na kila mmoja kuendelea na shughuli zake.

3. Kulazimisha kufanya uasherati.
Baadhi ya wachumba hutembeleana nyumbani, kijana wa kiume anaweza kumtembelea binti nyumbani kwake, au binti anaweza kumtembelea kijana wa kiume nyumbani kwake. Hasa wale waliopanga au waliojenga nyumba zao hutembeleana na kutumia muda mwingi kukaa pamoja.

Unajua shetani yupo kazini masaa 24, inapotokea mmoja wapo kuwaka tamaa, huanza kulazimishana kufanya uasherati, anapoona ni ngumu wengine hulazimisha kwa nguvu na kujikuta amefanya jambo ambalo hakulitegemea.

Akiwa mmojawapo hakutaka iwe hivyo kabla ya ndoa, hayo mahusiano yataingia kwenye shida kuanzia siku hiyo na kupelekea kuachana, na kama walijipanga kufanya hivyo wanapomaliza mmoja anaweza kumdharau mwenzake na kumwona hafai kuwa mke/mume wake.

Wengine hupeana ahadi ya kukutana kwenye sikukuu na kufanya uasherati, inapotokea mmoja hajaonekana au ameenda kinyume na makubaliano yao. Ugomvi huanzia hapo hadi kupelekea kutokuelewana na kuvunjika kwa uchumba huo.

Usiyejua sababu ya kuachana kwao na ukajaribu kuuliza, uwe mchungaji au uwe mzazi au uwe mlezi au uwe ndugu, unaweza usiambiwe kile kilichowafanya waachane, ukitafuta muda wa kuongea nao mmoja mmoja utakachoambulia kuambiwa hata yeye haoni sababu ya kuachana kwao.

4. Mawasiliano kuwa hafifu.
Ikiwa wachumba hawa hawatakuwa waaminifu katika kutunza maisha yao na kuheshimiana, wakawa wanafanya uasherati, kuna wakati utafika watazoeana. Wanapozeana sana yale mawasiliano mazuri yenye kuleta afya kwenye mahusiano yao hupungua au kuisha kabisa.

Mawasiliano yanapopungua kinachofuata ni kulaumiana, kila mmoja hujiona ana haki sana, atasema mbona hunitafuti, na mwingine atasema hadi mimi nikutafute ndio tuongee, mwingine atatoa malalamiko ya kutojibiwa sms zake.

Kama watakuwa wasapu mmoja anaweza kutuma sms, itakaa hata masaa matatu au sita bila kujibiwa na anamwona mwenzake yupo online, na akipigiwa simu anaweza asipokee. Ukiona mahusiano yamefika hivyo ujue hawapo pamoja tena, na itakuwa imeishia hapo, iwe kwa kupenda au kwa kutopenda.

Wengine huwa hawamkosei Mungu kwa kufanya uasherati ila hutokea kuchokana na kumwona mwenzake sio mtu sahihi kwake kama alivyokuwa anaona mwanzo, anachofanya ni kukata mawasiliano. Na moja ya nguzo muhimu kwenye mahusiano ni mawasiliano, hata kama mnapendana sana mkiacha kuwasiliana mara kwa mara kutokana na mlivyojiwekea utaratibu wenu, uwe na uhakika hayo mahusiano yatakufa.

5. Kuvunja ahadi waliyopeana.
Zipo ahadi ambazo wachumba hupeana, na ipo mipaka ambayo wachumba huwekeana kwenye safari yao. Wapo huambiana kuhusu suala la kuagana wanapotaka kwenda mahali fulani, wapo huwekeana muda wa kurudi nyumbani usiku.

Wapo hukuwekeana ahadi za kuoana kila siku au kila jumamosi au kila jumapili, ahadi hizi zinapovunjwa mara kwa mara pasipo sababu za msingi, au pasipo kueleweka kwa mmoja wapo. Ama inapojulikana kuna uongo ndani yake katika kujitetea kwake mara kwa mara, na kuomba misamaha ya mara kwa mara kwa kurudia kosa lile lile kila siku;

Mahusiano hayo huvunjika kwa sababu ya kuvunja ahadi walizowekeana, inawezekana ahadi ya kutokuwa na mahusiano mengine, au inawezekana kutofanya uasherati hadi waoane na mengine mengi.

Inapotokea mmoja wapo amevunja hizo ahadi walizojiwekea, huanza ugomvi unaopelekea kuachana kabisa, hata kama yalikuwa mahusiano sahihi na mtu sahihi. Utashangaa ule upendo uliokuwepo kwa watu hawa wawili umeyeyuka na kumwona mwenzake hafai kabisa.

Hizo ni baadhi ya sababu zinazoweza kuharibu mahusiano ya wawili, ndio maana ni muhimu sana kuendelea kuweka bidii ya kuombea mahusiano yako. Sio hilo tu, muhimu kuendelea kuwekeana mipaka ya kutomkosea Mungu, huo utakuwa ulinzi wenu katika uchumba.

Mwisho, unapaswa kuelewa kuvunjika kwa mahusiano yenu inaweza kuwa ni Shetani amekuharibia na kukutenganisha na mtu wako sahihi, na inawezekana Mungu amewatenganisha baada ya kuona tamaa zako zilikuongoza hakuwa mtu sahihi wa kuishi na wewe.

Usiogope, mwamini Yesu siku zote za ujana wako utafika salama kwenye hatima yako ya uchumba wako, utaitwa mke/mume wa fulani na utakuwa na ndoa nzuri ukimsikiliza Mungu na ukiwa mvumilivu.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
+255759808081