Kutembeleana baina ya wachumba sio vibaya, ikiwa nia yao ni moja na haina tamaa ya ngono ndani yake.

Hakuna ubaya wowote mchumba kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine kwa ajili ya kumtembelea mwenzake.

Inakuwaje mkaka unatembelewa na mchumba wako mnalala naye chumbani kwako kwa ujasiri mkubwa kabisa, huku kanisani wanakujua umeokoka, ni mtoa huduma mzuri.

Inakuwaje mdada unasafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa/wilaya nyingine unaenda kulala na kaka ambaye hata kwenu hajapeleka mahari.

Zipo nyakati tunajidanganya na kujiharibia ujana wetu wenyewe, dada anadanganya WAZAZI wake anaenda kwa ndugu yake, kumbe anaenda kwa mwanaume.

Wazazi wanafika kipindi wanaulizia binti yao yupo wapi, na wanapata hofu na kuanza kutaka kufika kituo police kwa ajili ya kutoa taarifa za upotefu wa mtoto wao. Kumbe dada huyu ameshafanywa mke na mpuuzi mmoja asiyejielewa.

Funga safari ya kwenda kwa mpenzi/mchumba wako, akiwa tayari amekuandalia sehemu ya kulala. Baada ya mazungumzo yenu, baada ya kula na kufurahi pamoja. Kila mmoja aelekee sehemu yake ya kulala.

Huo ndio ukristo, huo ndio utakatifu, huo ndio ustaratibu kwa mtu anayemjua Kristo na hataki kuangukia dhambini na dada/kaka ambaye bado hajafunga naye ndoa.

Mwingine atasema sijalala naye, hiyo michezo ya kimapenzi mmeitoa wapi, hiyo michezo ya kuchezea sehem za siri mpaka mnamalizana haja za miili yenu mnaitoa wapi.

Ujinga huu usipokemewa, tutakuwa na ndoa feki nyingi sana, wengi tunaharibu misingi wenyewe alafu yakishatufika shingoni tunaanza kusema Mungu ametuacha.

Mdada unajiachia kwenye chumba/nyumba ya mwanaume kama upo kwako, mwanaume mwenyewe mwaka wa pili sasa hajawahi hata kusema akajitambulishe kwa wazazi/ndugu zako.

Mkaka unacheza na kufanya uasherati na wadada kwenye kitanda chako kama wake zako, alafu unabaki kusema sijaona wa kuoa.

Utamwonaje mke wako wa kuoa, wakati moyo wako umechafuliwa na ngono. Utawezaje kumjua aliye mwaminifu kwako dada, ikiwa wewe mwenyewe unajiachia ovyo kwa wanaume.

Naamini unafanya haya ukiwa na akili timamu kabisa, utoto unaoufanya sasa yapo matunda yake, wakati huo utakuwa umeanza kukomaa kifikra na utakuwa huna tena uwezo wa kurudi nyuma.

Wanaume acheni kuwaita wachumba zenu makwenu, alafu mnakuja kulala nao kama wake zenu.

Wadada acheni kusafiri safari ya mbali kuwapelekea wanaume hawa uchi wenu, mtakuja kulia siku mmetoa mimba mpaka na kizazi chake.

Ujinga mnaofanya leo una mwisho wake, kabla hujafika mwisho huo bora kuacha uchafu wako sasa, na kutubu. Kabla neema ya Mungu haijaondoka kwako, ni vyema kuchukua maamzi sasa.

Mnawapelekeaga wanaume ninyi wenyewe alafu mnaanza kuja kuongea kauli za ovyo sana, eti hakuna mwanaume mwaminifu! kwani nani wa kulaumiwa kati yako na yeye, wote ni wapuuzi…maana ungekaa kwenu au kwako yasingekukuta hayo.

Mnawaitaga wadada wenyewe kuja kufanya upuuzi wenu, akishakubadilikia, unaanza kusambaza sumu mbaya. Eti wanawake wote mama yao ni mmoja, acha ujinga. Kuna wanaume wanaishi na wake zao mpaka unatamani kabisa wafungue shule ya ndoa kusaidia wengine.

Ujanja ni kuokoka kweli, ujinga ni kudanganya watu umeokoka alafu mfuko/mkoba wako umejaa vidonge vya majira na kondomu za kike. Utafikiri una mume kumbe unazitumia ili usipate mimba.

Ujinga ni kujaza begi/sanduku lako kondomu, ili kujiepusha na magonjwa/mimba isije ikampata mdada wa watu.

Usipoacha uasherati kijana lazima uje utumikie matunda ya uchafu wako, vinginevyo uje utoe gharama ya toba ya kweli kwa Mungu. Lakini kama utakuwa na wokovu wa vuguvugu, haijalishi utakuwa na pesa nyingi kiasi gani, utalizwa tu.

Umenisikia na kunielewa, tubu upesi na kuacha kabisa tabia hiyo kabla hazijaja nyakati mbaya kwako.

Ulitenda kosa na sasa umevuna kile ulichopanda, huna haja ya kumlaumu mtu, tubu na uanze upya na Bwana, utakuwa shuhuda mwema hekaluni mwa Bwana.

Samson Ernest.
+255759808081.