Kumekuwa na changamoto kwa vijana wengi wanapofika wakati wa kufanya maamuzi ya kuoa na kuolewa, imekuwa changamoto ya kuweza kumtambua mwenzi sahihi wa kuweza kuishi naye ni yupi, anakuwa mwombaji mzuri na ametunza maisha yake ya ujana ila anakuwa hana maarifa ya kutosha ya kuweza kumbaini mume/mke wake sahihi ya kuishi naye.

Sio ajabu kumkuta kijana aliyeokoka ana mahusiano na mtu asiye sahihi kwake, ndio asiye sahihi kwake, yeye anaweza asijue aliyenaye siye sahihi ila watu wengine waliokomaa kiroho wakajua hilo kutokana na vile wanavyomjua Mungu kupitia neno lake.

Wakati mwingine akiambiwa mtu uliyenaye sio sahihi kwako, anakuwa mgumu kuelewa na kuwaona wanaomwambia hivyo hawampendi na wanamwonea wivu, hii inatokana na ndugu huyu kutokuwa na mafundisho sahihi ya kuweza kung’amua hili jambo nyeti la maisha yake.

Wapo wanaume/wanawake wazuri sana kimwonekano na kimatendo ila sio wote wanaweza kufaa kuwa mke/mume wako, hata kama macho yako yanakufanya uvutiwe naye, ukitulia na ukamsikiliza Mungu utaona sio mtu wa kuweza kuishi na wewe. Atakuwa anamfaa mwingine ila sio wewe.

Leo tunaenda kujifunza mambo machache muhimu ya kukusaidia kufanya uamuzi sahihi unapotaka kuoa/kuolewa, baada ya kujifunza sifa hizi sita utaweza kufanya maamuzi yasiyo na majuto kwenye maisha yako.

Zifuatazo ni sifa sita(6) muhimu za kuweza kumtambua mke/mume wako sahihi wa ndoa;

  1. Awe Ameokoka

Hili sio la kuchukulia kawaida na kulipuuza na kuona unaelewa sana na utaweza kufanya chochote pindi mtakapokuwa ndani ya ndoa, ili kutambua uliyekutana naye au uliyemwona na macho yako anaweza akawa mume/mke wako anapaswa awe na sifa hii.

Kuokoka ni sifa muhimu sana, hii inaweza kukupa mwanzo mzuri wa kuangalia sifa zingine ili kujiridhisha kabla hamjaanza kuchukua hatua za kikanisa, na kwenda kwa wazazi wenu kujitambulisha.

Bila shaka haitakuwa ngumu kwako kumbaini aliyeokoka, kama inakupa ugumu unapaswa kujenga mahusiano Zaidi na MUNGU, tafuta kumjua Mungu Zaidi kupitia neno lake na mafundisho mbalimbali ya watumishi wa Mungu.

2. Amani Ya Moyo Wako

Hii ni silaha muhimu sana ya kuweza kumtambua aliyekuja kwako au unayemwendea ni mtu sahihi wa kuishi naye kwenye maisha ya ndoa au la, Amani hii ni ya Kristo ndani yako, unaweza kupata Amani nyingine nje ya Kristo ikakuingiza kwenye matatizo. Kwa kawaida Amani iliyo nje na Kristo huwa ya muda mfupi sana kwa hiyo ni rahisi kuitambua kupitia Roho Mtakatifu aliye ndani yako.

Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Kol 3:15 SUV

Utajua tu ndani ya moyo wako unakuwa na utulivu, kila ukijaribu kuingiza sababu ya kumkataa unajikuta unasikia shwari ndani ya moyo wako pasipo kushawishiwa sana na marafiki zake/zako au ndugu wengine waliye karibu nawe.

Ukiona ndani yako unakosa Amani usifanye haraka nenda mbele za Mungu, omba Mungu, yeye ni mwaminifu sana utaelewa tu kwanini ulikuwa unakosa Amani, hiyo itakusaidia kumtambua ni mtu sahihi ama sio sahihi.

3. Utayari Wa Kuishi Pamoja

Sio kila mtu anayekuja kwako utakuwa na utayari wa kuishi naye, na sio kila unayemwona ni mzuri utakuwa na utayari wa kuishi naye, unaweza ukawa unapata uzito ndani ya moyo wako. Kila ukijitahidi kujilazimisha unaona huna utayari ndani yako, hii ni alamu mhimu sana kwako.

Unapaswa kutulia na kujua kwanini unakosa utayari ndani yako, wakati mwingine sababu zinaweza zisionekane kwa macho ila kunakuwa na jambo la kiroho ambalo limejificha kwa macho ya nyama, unapaswa kumsikiliza Mungu anachokuelekeza kupitia Roho Mtakatifu.

Utajiuliza sasa nitajuaje kama Roho Mtakatifu amezungumza nami, usipate shida kama hujajua sana kumwelewa Roho Mtakatifu, ukiona baada ya maombi ya kina bado unasikia uzito ndani yako na huoni utayari ujue huyo sio mtu sahihi kwako. Roho Mtakatifu hutumia hii kama njia ya kukusaidia kufanya maamuzi sahihi, ukikosa utayari using’ang’ane, na ukipata utayari usiwe na wasiwasi.

4. Sifa Ulizojiwekea Zinaendana

Huwa tumejiwekea sifa za mtu tunayetaka kuishi naye, sifa hizi huwa za kwetu na zingine huwa za Kimungu kutokana na mtu anavyomjua Mungu. Unapokutana na msichana au mvulana unapaswa kurudi kwenye zile sifa zako, ukiona kuna baadhi ya sifa hana na asilimia Fulani kubwa anazo hapo unapaswa kurudi kwenye ile sifa ya kwanza, ya pili na ya tatu, utakuwa umeelewa sifa zingine zilikuwa za kwako hata usipozifuata hazina madhara kwenye ndoa yako.

Ukiona katika zile sifa zako  za nje ni nyingi kuliko zile za kiroho au hakuna hata moja ujue huyo sio mtu sahihi kwako, ngoja nikupe mfano huu utanielewa vizuri Zaidi; ulitaka mke mwenye sura zuri, umbo unalolitaka, urefu unaoutaka, ama ulitaka mwanaume mwenye kazi nzuri au pesa za kutosha, mwenye elimu nzuri, mzuri kimwonekano. Alafu katika hizo sifa akawa na zote ila akawa hajaokoka, kwanza utaona mtandao wako ndani ya moyo wako havikamatani, ujue hiyo sio sehemu sahihi kwako.

5. Hana Mahusiano Mengine Ya Kimapenzi

Mwanaume/mwanamke ambaye anakuambia anakupenda na yupo tayari kuishi na wewe alafu ana mahusiano mengine nje tena ya kimapenzi, unapaswa kutulia na umwombe Mungu kwanza. Inawezekana Mungu amekupa huyo, kama amekupa utaona ametulia na kuachana na uasherati, na hutamsikia akikusumbua ufanye naye uasherati, ujue huyo ni wako.

Ukiona habadiliki na anakuambia anakupenda anataka muishi naye kama mume na mke, usidanganyike kuwa atabadilika mkiwa kwenye ndoa, tena wakati mwingine Mungu anakukutanisha naye akiwa na mwanaume/mwanamke mwingine. Ama watu wanakujia na kukueleza kwa uwazi kuwa ana mahusiano na Fulani, na ukifuatilia unakuta ni kweli ana mahusiano ya kimapenzi, huyo achana naye.

Mtu sahihi kwako hawezi kuwa na michanganyo ya mahusiano, hii unaweza usielewe sana ila ukipuuza itakugharimu kwenye ndoa yako, sasa kabla hujaanza kuteseka na kumwomba Mungu ainusuru ndoa yako, unayo nafasi ya kufanya maamuzi mapema kabla ya ndoa.

6. Unaweza Kuvumilia Madhaifu Yake

Kila mtu ana madhaifu yake, hata mimi nina madhaifu yangu, hata kama nimeokoka yapo madhaifu, sisemi udhaifu wa kutembea na wanawake hovyo, hiyo ni dhambi iliyo ndani ya mtu na akiingia miguu yote kwa Yesu anaweza kuishinda. Nadhani unanielewa sasa, sasa unapokutana na mwenzako akawa anakerwa na vitu Fulani kwako au wewe ukawa unakerwa na tabia Fulani kwake usijalimishe kuwa naye.

Mfano labda wewe ni mwanaume na unapenda sana chakula kitamu kilichoandaliwa vizuri na mke wako, na binti uliyekutana naye anajua kuoga vizuri na kujiremba vizuri ila kwa ulivyofuatilia umejua hajui kupika. Umetumia namna ya kumwonyesha umhimu kujua kupika ila umefeli na unamwona hayupo tayari kujifunza, nikuambie utakuwa na ugomvi na mke wako kila siku kama hutaweza kuchukuliana naye.

Utafika wakati utaacha kula nyumbani, hapo utaongeza tatizo lingine ndani ya nyumba yako, kwanini uingize matatizo haya yote wakati unao uwezo wa kufanya maamuzi mapema kabla ya kuingia kwenye ndoa. Ni mambo madogo ila kwa wengine ni mambo muhimu sana na hawawezi kuyavumilia, wapo watu wamesahau ladha ya chakula cha wake zao kwa sababu hii. Na hakuna kitu kibaya kama mwanamke kuona mume wake hali chakula nyumbani, hiyo kesi inaweza isitatuliwe na mchungaji wake.

Huo ni mfano, unaweza kuona mifano mingine zaidi kwa yale usiyopenda kwa mke/mume wako na huwezi kuyavumilia kwake maana wewe unajifahamu vizuri kuliko watu wengine. Chukua mwanamke ambaye unaona moyoni mwako una utayari wa kuishi naye bila kujalisha madhaifu uliyoyaona kwake, na kubali mwanaume ambaye umeyajua baadhi ya madhaifu yake na huoni mzigo mzito wa kuishi naye.

Mwisho, hizi ni baadhi ya sifa zinazoweza kukusaidia kumtambua mume/mke wako sahihi wa kuishi naye, zingine Roho Mtakatifu atakufundisha Zaidi unavyoendelea kujifunza neno la Mungu kupitia kusoma na kusikiliza mafundisho ya watumishi wa Mungu.

Mungu akubariki sana

Samson Ernest

+255759808081