
Uongo upo, wapo wanautumia uongo kujiokoa kwenye hatari, wapo wanatumia uongo wapate msaada, wapo wanatumia uongo kutapeli watu, wapo wanatumia uongo kama sehemu yao ya maisha.
Uongo unatumiwa na watu wengi sana, wapo wanatumia uongo kwa makusudi kabisa wakijua wanachofanya sio sawa.
Kupitia uongo, wapo watu wameingizwa kwenye shida kubwa na waliowadanganya hadi leo wanajuta.
Wapo wameingia kwenye ndoa wasizozitarajia kwa kudanganywa. Na leo wanatamani siku zirudi nyuma wafanye maamzi upya.
Wapo wameingia kwenye hatia mbaya kwa kudanganywa na watu waliowaamini. Na leo wanaona dunia yote haina watu waaminifu.
Wapo wameingia kwenye biashara ambazo hawakuzitarajia kwa kudanganywa kuwa zinalipa sana. Na mitaji yao imepotea yote.
Wapo wamejiingiza kwenye tabia mbaya wasizozitarajia kwa kudanganywa na watu wao wa karibu. Na leo wanapambana kujitoa kwa akili zao imeshindikana.
Unaweza kuona vile uongo umetumika maeneo mengi katika maisha yetu na kutuletea shida.
Lakini leo tunaona vile uongo ulitumika kwa watu hawa kujiponya na kifo. Ambao ni Wagibeoni.
Rejea: Nao wakamwendea Yoshua hata maragoni huko Gilgali, nao wakamwambia yeye na watu wa Israeli, Sisi tumetoka nchi ya mbali sana; basi kwa hiyo fanyeni agano pamoja nasi. Basi watu wa Israeli wakawaambia hao Wahivi, Labda mwakaa kati yetu; nasi tutawezaje kufanya agano nanyi? Nao wakamwambia Yoshua, Sisi tu watumishi wako. Yoshua akawauliza, Ninyi ni nani? Nanyi mwatoka wapi? Nao wakamwambia, Sisi watumishi wako twatoka nchi iliyo mbali sana, kwa sababu ya jina la BWANA, Mungu wako; kwa kuwa sisi tumesikia sifa zake, na habari ya hayo yote aliyofanya huko Misri, YOS. 9:6-9 SUV.
Hawa Wagibeoni walishasikia habari za taifa teule la Mungu Israeli, na walisikia habari za Mungu aliyewaahidia nchi waliyokuwa wanaikalia wao.
Sasa wakakaa na kuona watumie mbinu ya kuvaa hovyo na kutembea na mkate ulioharibika ili waonekane wametoka mbali kweli.
Wakiwa na uhakika kufanya hivyo itakuwa salama yao ya kutokuawa. Na kweli ikawa hivyo ila baadaye wakaja kugundulika.
Rejea: Kisha ikawa, mwisho wa siku ya tatu baada ya kufanya hilo agano nao, walisikia habari ya kuwa watu hao ni jirani zao, na ya kwamba waliketi kati yao. YOS. 9:16 SUV.
Kosa lililofanyika tayari walishaapiwa kwa Mungu wa Israeli, kwahiyo haikuwezekana tena kuwaua hata kama waliwabaini ni watu waliopaswa kuuawa.
Majibu yao yalikuwa hivi baada ya kugundulika walichokifanya, yaani baada uongo wao kujulikana kwa uwazi.
Rejea: Nao wakamjibu Yoshua, na kusema, Ni kwa sababu ya sisi watumishi wako kuambiwa hakika, jinsi huyo BWANA, Mungu wako alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote, na kuwaangamiza wenyeji wote wa nchi hii watoke mbele zenu; kwa sababu hii tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, nasi tumefanya neno hili. YOS. 9:24 SUV.
Unaona hayo maelezo ya watu hao, hili linapaswa kuwa somo kwako/kwetu. Hasa wewe ambaye umeokoka na unamtumikia Mungu.
Adui yako anaweza akajua nguvu uliyonayo, akatumia kila namna ya kujifanya mtu mwema. Alafu baadaye unakuja kugundua hakuwa mtu mwema kwako.
Watu wanaweza wakajua habari za Mungu wako anavyokutumia kwenye huduma yako. Wakatumia namna ndogo tu ya kuwafanya uwaonee huruma, ukija kushtuka sio watu sahihi tayari utakuwa umechelewa.
Ndio maana ni muhimu sana kumsikiliza Roho Mtakatifu, yapo maelekezo Roho Mtakatifu anaweza kukupa. Ukaona labda yalikuwa mawazo yako tu, baadaye ukaingia kwenye hatia mbaya sana.
Uwe mwangalifu sana kwenye nyakati ambazo Mungu anakutumia sana kwenye maisha yako ya huduma.
Kwa lugha nyingine naweza kukuambia hivi “usijisahau” wakati unafikiri hali ni shwari ndio wakati ambao adui anapata mlango wa kuingia.
Mungu akubariki sana.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana,
Samson Ernest.
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255 759 80 80 81