
Kuna nyakati kanisa linaweza kupitia katika kipindi kigumu sana, kipindi ambacho wapo wanaoshindwa kuendelea mbele na kujikuta wamekimbilia sehemu zingine zenye utilivu mzuri. Na wengine huacha kabisa wokovu kwa sababu ya misukosuko mingi ya kanisa.
Kipindi kama hicho huwa kuna hali nzito sana, watu hujaa huzuni nyingi wanavyoona jinsi mambo yanavyozidi kwenda mbele. Hali hiyo huzidi kuathiri hata wale waliookoka siku za karibuni, wanaona kuwa ukristo mbona uko hivi?
Kumbe ni wakati ambao kanisa linakuwa kwenye mpito fulani mgumu sana, wakati ambao hata mkiomba mnaona maombi yenu hayajibiwa. Huzuni inakuwa imetanda ndani ya kanisa, siku za kukusanyika pamoja unaona palivyo pazito.
Hali hiyo inaweza kukufanya ukaanza kufikiri labda mahali ulipo sio mahali sahihi, ukiwa mtu unayesoma neno la Mungu. Hili jambo halitakuwa geni kwako, wala hautakuwa mtu wa kushangaa sana.
Tangu zamani kanisa lilipita kwenye hichi kipindi kigumu, kipindi ambacho halikuwa na raha kabisa, kipindi ambacho walikuwa wanaona ndugu zao wakiteseka kwa ajili ya jina la Yesu Kristo, kipindi ambacho walikuwa wakiona watu wakiuawa kwa jina la Yesu Kristo.
Hakuna mshirika aliyekuwa na raha kwenye hicho kipindi, kila mmoja aliangalia usalama wake zaidi na familia yake, hofu ya kuawawa ilikuwa imetanda kwa kanisa.
Hilo ni kanisa la mwanzo, ila hata sasa tunaona mambo kama haya yakitokea kwenye kanisa la leo, utakuta washirika hawamtaki mchungaji wao kutokana na sababu wanazotoa wao, utakuta wachungaji kwa wachungaji hawaelewani kutokana na sababu wanazotoa.
Mambo kama haya yanapokuwa yametokea, hata ile idadi ya watu hupungua, licha ya kwamba kuna baadhi ya watu wanaweza kusambaratika. Bado na ile idadi ya watu wapya kuongezeka kanisani inakuwa ngumu kutokana na vurugu zinazoendelea ndani ya kanisa.
Pamoja na misukosuko hiyo mingi, upo wakati Yesu Kristo hurejesha raha ya kanisa, raha ambayo ni ya kweli kabisa. Baada ya kanisa kupita kwenye mpito fulani mgumu, Yesu hurejesha ile raha iliyopotoa kwa muda mrefu.
Hili tunajifunza kupitia Neno la Mungu, baada ya Sauli kukutana na Yesu Kristo, akambadilisha maisha yake, yaani kutoka kuua watu hadi kuwa mhubiri wa injili. Kitendo hicho kilifanya kanisa liwe na utulivu mkubwa sana.
Baada ya raha ya kanisa kurejea tena kwa upya, kanisa lilijengwa tena na likazidi kuongezeka, na faraja ya Roho Mtakatifu ikaendelea kuwa pamoja nao.
Rejea: Basi kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu. MDO 9:31 SUV.
Ndugu, unaweza kukosa raha kwa muda mrefu sana kwa sababu ya mapito magumu unayopitia katika maisha yako, Neno la Mungu linatuambia siku ya leo. Kanisa lilifika mahali likapata raha, ile furaha iliyoondoka kwa watu, ikafika mahali ikarejeshwa na Yesu mwenyewe.
Yesu hatakuacha kamwe kwenye huzuni yako, mateso yako anayajua, kulia kwako anakuona, endelea kumtazama yeye. Ipo siku mateso yako yataondolewa na furaha yako itarejea kwa kiwango kingine kabisa.
Kupita kwenye wakati mgumu, isiwe sababu ya kumwasi Mungu, kupita kwenye wakati mgumu sio kana kwamba umemkosea Mungu. Wakati mwingine shetani huleta huzuni kwetu ili tumkosee Mungu wetu, ili yeye apate mfuasi wake.
Ukiwa kama kanisa, simama imara, bila kujalisha mazingira magumu unayopitia, bila kujalisha mazingira magumu unayokutana nayo. Yesu hatakuacha kamwe kwenye magumu yako, ipo siku yale yote yaliyokuwa yanakufanya ukose raha yataondolewa kwako.
Ni muhimu sana kukua kiroho, hakikisha unasoma Neno la Mungu kila siku, na hili liwe jambo la lazima kwako, sio hiari tena, kama umejaribu kusoma kwa hiari imeshindikana. Badilisha utaratibu wako, soma kwa kujilazimisha, baada muda utaona matunda yake.
Unaweza kuungana na wenzako wanaosoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya wasap group, kama unahitaji kujijengea nidhamu ya kusoma Biblia yako. Kundi hili la wasap litakufaa, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com