Kibali mbele za watu ni neema ya Mungu inayokuwa juu ya mtu, anaweza akawa mhubiri wa injili, anaweza akawa mwimbaji za nyimbo za injili, inategemeana na huduma aliyonayo.

Mara nyingi si watu wote utawakuta wana neema hii ya kukubalika sana mbele za watu wengi, unaweza kushangaa kuna mtu anafanya huduma ile ile na yule anayekubalika na watu.

Ukashangaa anaonekana mtu wa kawaida kabisa, na watu wakawa hawana muda naye kabisa isipokuwa watu wachache ndio wakawa wanamkubali.

Ndio maana wale ambao bado hawajapata neema ya kumjua Yesu Kristo, huwa wanaenda kutafuta kibali kwa miungu mingine. Ila sisi tuliokoka huwa hatuendi huko, ukishaokoka hichi kibali kwa watu hupewa mtu kama zawadi na Mungu.

Ninaposema zawadi namaanisha kwamba sio kitu ambacho kila mtu anaweza kupewa hii zawadi, kuna wachache wanapata neema hii, na kuna wapo bado hawajaipata, na kuna wapo waliondolewa hii neema.

Watu wengi wanashindwa kujua hili, wanapopata kibali mbele za watu, yaani Mungu anapowapo kibali chake kwa watu. Watu wale huanza kuona bila wao watu hawawezi kufanya kitu au bila wao mambo hayawezi kuwa vizuri.

Wengine huanza kugoma kufanya huduma, hawana sababu ya msingi sana ya kuwafanya washindwe kutoa huduma kwa watu, ila hujiona wamekuwa watu maalum sana.

Ule unyenyekevu wao wa mwanzo kabla hawajajulikana sana na watu kwa kitu Mungu amewapa ndani yao, walikuwa watu wazuri kabisa, walikuwa wana ukarimu mzuri, na walikuwa wana heshimu wengine wenye huduma. Lakini pale wanapoinuliwa na Mungu, wapo kiburi huanza kuota ndani yao.

Ndipo unapoanza kumwona yule mpiga kinanda kanisani anaanza kusumbua, ndipo unapoanza kumwona yule mpiga kitaa anaanza kuleta shida kanisani. Anataka kubembelezwa kila kitu kisa yupo pekee yake pale kanisani, kisa watu wanamkubali sana anapokuwa anapiga kinanda au kitaa.

Ndipo unapoanza kuona yule mwimbaji mwenye sauti nzuri sana aliyekuwa anaimbisha nyimbo za kuabudu na kumsifu Mungu hadi watu wanaponywa magonjwa yao, unamwona anaanza kiburi. Kwa akili yake na kwa jinsi ya kawaida kabisa, anaona bila yeye hawataweza kufanya vizuri.

Pasipo kujua wengi, hapa ndipo anguko lao kubwa kwenye huduma zao limewakuta wengi. Utashangaa mtu alikuwa vizuri, kila mtu anatamani aimbe, kila mtu anatamani ahubiri/afundishe, lakini baada ya kuingiwa na kiburi ile neema ya kukubalika iliondoka kwake.

Hujawahi kuona hata ofisini kama umajiriwa au umeajiri, mfanyakazi fulani alikuwa vizuri sana, utendaji wake wa kazi ulikuwa unasifiwa na kila mtu. Baada ya kukubalika sana na waajiri wao, na kila mfanyakazi alimwinulia mikono kwa ufanyaji wake wa kazi, ghafla alianza kiburi.

Ule unyenyekevu wake uliondoka, akaanza kujiona bila yeye ofisi ile haiwezi kupata mafanikio kama yalivyo sasa, inafika wakati waajiri wale wanaanza kumsihi asiwe na tabia hiyo. Unamkuta haielewi kitu, wafanyakazi wenzake nao wanamlalamikia yeye tu, na wafanyakazi wengine wanakuwa na ujasiri wa kumweleza ukweli ila anakuwa haelewi.

Baada ya muda utashangaa ile sifa na kukubalika sana kwa boss na wafanyakazi wenzake, kunaisha kabisa, kama alikuwa na cheo fulani anashushwa kabisa chini anakuwa mfanyakazi wa kawaida.

Mahali popote kiburi hakiwajawi kumwacha mtu salama, kiburi kinampoteza kabisa kwenye njia sahihi aliyokuwa anatembelea mtu. Ndio maana unapaswa kufahamu madhara ya kiburi kibiblia, ili siku ukikuruhusu uwe unajua kinachoenda kutokea.

Rejea: Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa. Mithali 29:23.

Unaona hilo andiko ndugu, Neno la Mungu limeweka wazi kabisa hili ninalokueleza hapa. Ndio maana ni muhimu sana usikaukiwe na Neno la Mungu, kila siku unapaswa kutenga muda wako wa kusoma Neno la Mungu, kufanya hivyo utaepukana na shida/matatizo mengi sana.

Dawa ya kukushusha haraka na kukuondolea kibali chako mbele za watu ni kiburi, kiburi ni hatari sana kwa mtu. Hupaswi kabisa kukiruhusu kibali kiinuke kwako, kubali kuendelea kunyenyekea chini ya mkono wa Bwana.

Huna haja kuwa na kiburi, kumbuka hii ni neema ambayo Mungu huachilia kwa mtu. Ukiichezea hiyo neema itaondoka kwako na kubaki mtupu, sasa kuja kuirejesha tena kwako hiyo gharama yake ni kubwa sana.

Tena angalia Neno la Mungu linavyoendelea kusema kwenye huu mstari chini ninaoenda kukushirikisha hapa, uone ni jinsi gani kiburi kilivyo hatari sana kwa maisha ya mwanadamu, hasa mwenye huduma fulani au cheo fulani.

Rejea: Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa Bwana; Hakika, hatakosa adhabu. Mithali 16:5.

Umeona huo mstari, pale mwishoni unasema hivi, “hatakosa adhabu” kwahiyo bila kukupa maneno ya kukufariji, mwenye kiburi yeyote lazima apewe adhabu. Maana ni chukizo kwa Bwana, sio kwa boss wako, sio kwa mume wako, sio kwa mke wako, ni chukizo kwa Bwana.

Tena neno la Mungu likagongelea misuri kabisa kwenye mstari huu ninaoenda kukushirikisha hapa chini, nimekupitisha kwenye mistari mingi kidogo uone uzito wa hili jambo.

Rejea: Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu. Mithali 11:2.

Nataka utazame yale maneno yanayosema hivi; Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu… Mithali 11:2a. Unaona kinapokuja kiburi kinachofuata ni aibu! Je! Unakubali aibu iwe kwako? Kama ni hapana usikubali hichi kitu kikuingie kabisa.

Linda sana moyo wako kiburi kisiingie ndani mwako, madhara yake ni rahisi kusoma kama hivi ila siku likikufika hili utaelewa vizuri ninachokueleza hapa. Kwa sababu umeshajua hichi ninachokueleza hapa, hakikisha huruhusu kiburi kwa namna yeyote ile.

Je, unapenda kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu kila siku? Karibu sana kwenye kundi letu la wasap, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com