
Miongoni mwa watu ambao wanageukwa na kuanza kupewa majina mabaya, kama vile amerukwa na akili, ana wazimu, na majina mengi ya kuonyesha mtu yule anayesema kweli hayupo sawa.
Watu hao ni wale wanaosimamia kuisema kweli au wale wanaokaa kwenye upande wa kweli, watu wale lazima watafika mahali wataonekana hawapo sawa kiakili.
Kama huwajui vizuri, unaweza kuungana nao wanaosema hivyo kwa kusema fulani amerukwa na akili siku hizi, au fulani siku hizi ana wazimu, au fulani siku hizi akili yake haipo sawa.
Sio kana kwamba mtu huyo au watu hao wanakuwa wamerukwa na akili, au wana wazimu, au akili zao hazipo vizuri, wanakuwa wapo vizuri kabisa isipokuwa wanakuwa kinyume na baadhi ya watu wenye mamlaka.
Wanaweza wasiwe watu wenye mamlaka, wakawa watu tu wakawaida wenye dini zao ila wanakuwa hawapo tayari kukubaliana na mtu yule anayesema kweli. Au anakuwa mtu huyo anayesema ukweli, anakuwa sio mtu aliye upande wao, bali anakuwa mtu aliye kinyume chao.
Kwa kuwa watu wengi hatuna muda wa kutafuta kuujua ukweli, au kwa kuwa watu wengi tunapenda kusikia zile habari tunazozipenda tu. Ziwe za uongo ama ziwe za ukweli, sisi huwa tunataka kusikia zile habari ambazo tupo tayari kuzisikia tu.
Tunapoambiwa fulani siku hizi amerukwa na akili, tunaweza kuamini haraka kwa sababu huyo mtu anakuwa sio mtu mzuri sana kwetu. Huenda amekuwa ni mtu anayeharibu mipango yetu mingi ovu, tunajikuta tunakuwa na hasira naye ndani ya mioyo yetu.
Mtu mmoja mwenye nafasi fulani kubwa kwenye jamii au mwenye uwezo mkubwa kifedha, anaposimama kusema mtu fulani siku hizi akili yake haipo sawa, au siku hizi fulani ana wazimu. Mtu huyo anaweza kuaminika na kundi kubwa la watu, kutokana na watu wengi huwa hatuna muda wa kuchimba ukweli wa jambo.
Hili la kuonekana una wazimu, au umerukwa akili, au haupo sawa kiakili, tunajifunza kupitia maandiko matakatifu. Tunaona mtume Paulo akionekana ana wazimu kutokana na imani yake ya kumwamini Yesu Kristo, na kumtumikia Mungu kwa kuwatangazia watu habari za Yesu Kristo.
Rejea: Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili. Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili. MDO 26:24-25 SUV.
Kama mtume Paulo alivyonekana ana wazimu kwa kueleza ukweli wake uliompelekea kuwa hivyo alivyo, hata leo wapo watu wengi sana ambao wapo upande wa kuisema kweli au kusimamia kweli. Watu hao wanaonekana wana wazimu, ndani ya ufahamu wao wanaonekana hawapo sawa.
Bahati mbaya itokee mahusiano yako na mume/mke wako hayapo sawa, hapo ndipo watapatia pa kukupigia vizuri. Watazusha maneno ya uongo na utaonekana kwa watu kuwa akili yako haipo sawa kweli, kumbe upo vizuri kabisa na uliyotamka yanatoka moyoni.
Tuwe makini katika hili, hasa sisi wakristo, nasema hivi kwa sababu tunaweza kujiingiza kwenye makundi ya ushabiki wa uongo, ukawa unajiona upo sawa kumbe unamkosea Mungu wako.
Uwe makini pia wewe ambaye unapenda kusikia habari fulani nzuri tu, zipo habari ni za kweli kabisa ila zinaweza zikawa kinyume na vile unavyoamini. Unapoguswa kwenye ukweli unaweza kupinga sana na kumwona aliyesema hivyo ni muongo.
Unafikiri kama mtume Paulo alifika mahali akaonekane ana wazimu, unafikiri wewe utaacha kuonekana hivyo kwa watu walio kinyume na Neno la Mungu? Lazima ukutane na kashfa kama hizo, kama usipokuwa na Neno la Mungu la kutosha, unaweza kuingiwa na uoga na kuanza kuona usiwe unasema ukweli au uache kusimama upande wa ukweli.
Usiogope, simama kama mtume Paulo aliyesimama kwenye kile alichoamini, yale maono yake hakuyakana kabisa mbele za watu. Hata kama walionekana hawamwelewi vizuri, bado alisimamia msimamo wake na kuendelea kuwaeleza iliyo kweli.
Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nakusihi uchukue hatua ya kujiunga na kundi hili. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa baada ya kupewa kanuni za kundi.
Mungu atusaidie sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081.