Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za muda huu ndugu yangu katika Kristo, pole na shughuli za kutwa nzima. Na hongera kwa kuimaliza siku ya leo, hongera pia kwa kupambana na changamoto za kutwa nzima ya leo. Wewe ni mshindi, haijalishi umejeruhiwa moyo wako kiasi gani, bado wewe ni mshindi.

Matendo yetu mema yanatazamwa na watu wengi sana, jinsi unavyozidi kufanikiwa katika eneo fulani la maisha yako, iwe kimwili au kiroho. Jua kuna watu wanazidi kukufuatilia na kukufahamu zaidi, na kupeleka habari zako mbali zaidi na zaidi.

Huna haja ya kujitangaza sana, kama una kitu cha thamani kwako wengine wanachokipata, lazima watapeleka habari zako mbali zaidi. Wanapozidi kupeleka habari zako, katika hao, wengi hao wapo ambao wanakuwa hawaamini kile wanachoambiwa juu yako.

Huenda zamani walikujua kama mtu wa kawaida kawaida, ila kwa kuwa Mungu anakutumia kwa viwango vya tofauti kuitenda kazi yake. Lazima wapo watu watakuwa na mashaka na habari wanazosikia.

Yawezekana tangu kuumbwa kwa misingi ya dunia hawajawahi kusikia mtu wa namna yako, sasa watu wanaposikia habari zako lazima wafunge safari kuja kukutazama vizuri wewe ni wa namna gani.

Wanaokuja wote kwako, wapo kweli wanakuwa na uhitaji wa huduma unayotoa, na wapo hawahitaji huduma ila wanataka kukuona tu. Na wapo pamoja na kukuona bado watahitaji kuthibitisha kitu ulichonacho ndani yako, ambacho kila mtu anakisema kwako.

Ikiwa wewe ni mkaka na hujaoa, na wadada wamesikia habari zako za msimamo ulionao juu ya kutunza ujana wako. Alafu wakaja wadada kukujaribu kukuwekea kila mtego, lakini wakashindwa kila mbinu walizototumia. Jua kwamba umemwinua YESU Kristo zaidi ya awali, na watasema hakika wewe ni kaka wa YESU Kristo.

Shida inakuja pale waliposikia habari zako za kuwa wewe ni kaka unayejiheshimu na kumpenda Mungu. Wakaja kukujaribu kidogo tu kwa kukuwekea mitego, alafu ukaingia kwenye kumi na nane zao. Nakwambia kuanzia siku hiyo utalisababisha jina la Yesu Kristo kusemwa vibaya kuhusu tabia uliyoionyesha kwa watu kukujaribu.

Hili jambo la kujaribiwa huwezi kuliepuka, kama unatoa huduma ya KIROHO na habari zako zikaenea kote, jua hicho kitendo shetani hawezi kukubaliana nacho na akakifurahia. Lazima atakuja na mtego ambao ukiushindwa kuutegua ujue sifa yako ya kumbeba Kristo itapotea kabisa.

Ndio maana mara nyingi umeona watu wakisema, kama yule dada/kaka ameokoka, na mimi nitakuwa nimeokoka. Maana yake walikuja kuujaribu wokovu wako, wakakutana na hewa iliyojaza pulizo.

Ushindi kwa Yesu Kristo pale watu wanaposikia habari zako njema, wakaja kwako kuthibitisha kama kweli. Wakakuta yanayosemwa ni kweli na mengine hayakusemwa vizuri ila unayo wewe zaidi ya hayo.

Haya tunayathibitisha kwa mfalme Suleiman, sifa zake za hekima aliyokuwa nayo, ziliwavuta watu wa mataifa mbalimbali duniani kote. Yaani inaleta ladha hata ya kusimlia kwa kweli.

Rejea: Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani, alikuja ili amjaribu Sulemani kwa maswali ya fumbo huko Yerusalemu, mwenye wafuasi wengi, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akamwambia mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie. 2 NYA. 9:1‭-‬2 SUV.

Ndugu yangu unanielewa nilichokuwa nakisema? najua umenipata vizuri baada ya kusoma hayo maandiko Matakatifu. Naomba uwaza vizuri, usiogope kuonyesha kitu alichokupa Mungu ndani yako, ninachotaka hapa uone ni jinsi gani mambo yanaweza kuwa katika huduma yako.

Nalazimika tena kukupa maandiko mengine machache huenda ukaelewa zaidi habari hii, ili ujue kwamba wewe ni barua inayosomwa na dunia nzima.

Rejea: Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako. 2 NYA. 9:5‭-‬7 SUV.

Mbaya sana mtu kukuambia nilisikia wewe ni mtumishi wa MUNGU mzuri kumbe una tabia mbaya hivi. Ni heri wakasema nilisikia wakikusema vibaya kumbe haupo vile walikuwa wanakusema, ni heri watu wakasema tulisikia habari zako njema nusu nusu ila sasa tumethibitisha wewe ni zaidi ya tulivyoambiwa.

Ishi maisha ya wokovu ukilitambua hili, itakufanya uwe mwangalifu sana eneo lolote utakalokuwepo, haijalishi utakuwa nchi isiyo yako. Utaishi maisha ya utakatifu maana unajua wewe ni chombo chema kinachotumiwa na Mungu kutangaza habari zake.

Watu wanaanza kuona uzuri wa tumbo la mzazi aliyekuzaa, watu waanze kuona wamependelewa wale unawahudumia, watu wamtukuze Yesu Kristo kupitia matendo yako mema.

Nasikia kuandika zaidi, ila nikuachie hapa, kutokana na kujali muda wako, naamini umenielewa vizuri. Na utaanza kufanyia kazi haya uliyojifunza.

Nashukuru sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.