Siku hizi imekuwa kama fasheni fulani hivi, au tuseme imekuwa kama kichaka cha watu kujifichia maovu yao, mtu anatenda kosa, watu wanamwendea na kumwambia hilo unalofanya halifai. Wengine wanamkemea vikali sana, badala ya kubadilika, anageuza maneno.

Utasikia mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe, yaani ujinga anaofanya ndio anajiona ni mti wenye matunda. Anashindwa kutofautisha kabisa hili, kwa kujua, ama kwa kutojua, hajui wanaopigwa mawe wakati mwingine hawana matunda yeyote.

Miti mingine huwa inapigwa mawe sio kwa sababu ina maembe mazuri, sio kana kwamba ina machungwa mazuri, sio kana kwamba ina maparachichi mazuri, sio kana kwamba ina mapera mazuri sana. Miti mingine inakuwa imebeba nyoka hatari, kwa hiyo watu wanakuwa wanaupiga mti ili kuua nyoka asije akawadhuru.

Sasa mtu asiyejua kitu, anaona yeye anapigwa mawe kwa sababu ni mti wenye matunda, kumbe ni mti wenye nyoka, huna matunda yeyote. Na kama ni mti wa matunda, wakati huo unakuwa hujazaa matunda yeyote isipokuwa kuna nyoka hatari yupo juu ya mti huo.

Mtu akishaiacha njia sahihi, alikuwa ameokoka vizuri akawa amerudi nyuma, watu wakaona matendo yake sio mazuri, wakamwendea kumwonya juu ya tabia yake. Anaweza kuwaona wanafuatilia maisha yake, kwa kuwa hajakubaliana na maonyo yale, ataona yeye ni mti wenye matunda ndio maana watu wanamsakama sana.

Acha kujidanganya rafiki, kama unashumbuliwa kwa maneno, kwa sababu umetoka kwenye njia sahihi, ambayo maneno hayo tunayaita ni mawe, na mti ni wewe mwenyewe. Acha kujifariji kuwa unapigwa mawe kwa sababu ni mti wenye matunda, watu wanakupiga kwa sababu ni mti wenye nyoka mwenye sumu kali.

Unapaswa kujikagua sana, hasa pale unapoona watu wanakushambulia kwa maneno, na wengine wanataka kutoa uhai wako, ukaanza kujivuna wewe ni mti wenye matunda ndio maana unapigwa mawe. Inaweza ikawa kweli zamani ulikuwa mti wenye matunda, ila matunda hayo yalioza na sasa watu wanapambana kuua nyoka kwenye mti.

Watu wanaoweza kusema wanapigwa mawe kwa sababu ni watu wenye matunda, watu hao ni kama Paulo, alipigwa mawe kwa sababu ya kulihubiri jina la Yesu Kristo. Mtu aliyetoa maisha yake kuitangaza kweli ya Mungu, Wayahudi wakakasirika sana.

Rejea: Lakini Wayahudi wakafika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhania ya kuwa amekwisha kufa. Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na siku ya pili yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe. MDO 14:19‭-‬20 SUV.

Watu kama Paulo wanapaswa kujivuna ni mti wenye matunda ndio maana unapigwa sana mawe, nje na hapo usijivune wewe ni mti wenye matunda. Watu wanakusakama kwa sababu ya tabia zako mbaya, sio kwa sababu unafanya mambo mazuri.

Utambea na wake/waume za watu alafu ukiambiwa unasema wewe ni mti wenye matunda? Huo ni ujinga, wewe hujabeba matunda ila umebeba uovu. Watu wanakushambulia waue nyoka wa uovu juu yako, maana ni sumu hatari inayoharibu ndoa za watu.

Kuanzia sasa mtu asikuumize kichwa, hasa wale wanaomtenda Mungu dhambi, wakionywa/wakikemewa wanakimbilia kusema wanafanyiwa hivyo kwa sababu ni mti wenye matunda. Ukikutana na mtu wa namna hiyo mwambie wewe sio mti wenye matunda, bali ni mti wenye nyoka mwenye sumu kali.

Karibu kwenye darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa mtiririko mzuri, tuma ujumbe wako wasap wenye maneno CHAPEO YA WOKOVU kwa wasap namba +255759808081.

Soma Neno Ukue Kiroho.
Mungu akubariki sana,
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com