Tumezoea kuona tukiwa kwenye msiba wa kuondokewa na ndugu zetu au marafiki zetu au majirani zetu. Huwa tunajawa na majonzi mengi sana, ambapo hutufanya tulie pamoja na waombolezaji Wengine.

Imezoeleka pia unapokutana na shida, huwa wanajitokeza watu wa kuja kuungana nawe katika kulia kwako. Wapo watakaokupa faraja kwa kukutia moyo, na wapo watakaoonyesha ukaribu wao kwako.

Kutiana moyo na kupeana faraja, ni jambo la muhimu sana tukiwa kama binadamu. Ila hili suala linaweza kukuletea madhara kwa upande mwingine.

Mtu anaweza kuonyesha kuungana na wewe katika msiba wako, kumbe huyo mtu ana ajenda nyingine ya siri kwako. Pasipo kujua nia yake ni mbaya, ukajisikia vizuri upo na ndugu/rafiki yako wa karibu wa kukutia moyo.

Unapokuja kujua hakuwa mtu mzuri kwako, utakuwa unapambana dakika za mwisho kupigania uhai wako. Uhai ambao umetolewa na mtu aliyeonekana kukukarimu, na mtu aliyeonyesha kulia na wewe katika shida yako.

Sikuelezi haya uanze kuhisi vibaya kila mtu anayelia na wewe katika shida yako, nakueleza haya upate kufahamu. Lazima ufike mahali ukue kiakili, ili Mungu anaposema na wewe kuhusu hatari iliopo mbele yako uweze kuelewa haraka.

Haya ninayokueleza hapa ni habari za kweli zilizowapata watu waliotoka Shekemu, Shilo, na Samaria, watu takribani wasiopungua themanini. Hawa watu walikuwa wamenyoa ndevu zao, na kurarua nguo zao, nao wamejikata-kata, wakichukua sadaka na ubani mikononi mwao, ili wazilete nyumbani kwa BWANA.

Ishmael aliwapokea kwa kilio kuonyesha kuungana nao, kumbe moyoni mwake alikuwa na ajenda nyingine mbaya. Hawa watu waliishia kuuawa na mtu aliyeonyesha kulia na wao.

Rejea: Ikawa siku ya pili baada ya kumwua Gedalia, wala hapakuwa na mtu aliyejua habari hii, wakafika watu kadha wa kadha toka Shekemu, na toka Shilo, na toka Samaria, watu themanini, nao wamenyoa ndevu zao, na kurarua nguo zao, nao wamejikata-kata, wakichukua sadaka na ubani mikononi mwao, ili wazilete nyumbani kwa BWANA. Na Ishmaeli, mwana wa Nethania, akatoka Mizpa kwenda kuwalaki, akilia alipokuwa akiendelea; ikawa alipokutana nao akawaambia, Njoni kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu. Basi ikawa walipokuwa katikati ya mji, Ishmaeli, mwana wa Nethania, akawaua, akawatupa katika shimo, yeye na watu wale waliokuwa pamoja naye. YER. 41:4‭-‬7 SUV.

Hupaswi kuishi kwa mashaka ila unapaswa kuwa na ufahamu ndani yako, elimu ya kiMungu inapaswa kujaa kwa wingi ndani yako. Utaweza kutambua makusudi mabaya ya mtu anayekujia kwako kwa njia yeyote ile.

Laiti hawa watu wangetambua mapema Ishmael sio mtu mzuri kwao, wangetimua mbio kali sana. Badala yake wakaishia kuawa kifo kibaya sana.

Usiishie kufurahia umepata mtu wa kulia na wewe, hebu jaribu kujiuliza maswali kadhaa. Maana wapo watu wanalia na wewe wakiwa na malengo yao mabaya kwako.

Binti unaweza kukutana na mwanaume mwenye kuonyesha kukuhurumia katika shida yako. Ukamwona ni mwanaume wa pekee sana kwako, ukafika mahali ukaona anafaa kuitwa mume wako. Kumbe mwanaume yule alikuwa na mahesabu yake maovu ya kukunasa.

Kwa kutojua kwako, unajikuta umelala naye, na kukuachia zawadi ya mimba na ugonjwa wa Ukimwi. Sio kwamba ameokuoa, hayo yote anakufanyia na kukuacha hapo. Unabaki kulaumu wanaume wabaya sana, kumbe wewe mwenyewe ulijirahisha kwake. Kwa sababu alikuonyesha ni mtu wa kujali sana.

Hata pale mtu anapoonyesha kukusaidia jambo fulani, uwe makini sana na msaada huo. Misaada mingine ukishaipokea inakupelekea umauti moja kwa moja.

Mungu afungue ufahamu wako.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081