Haleluya, nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine bora kabisa Bwana ametupa kibali cha kuifikia na kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana wetu mwenza wa yote, maana ni fursa adimu sana kuipata, wapo walioitamani lakini hawakuweza kuifikia leo.
Tumefika mahali badala ya kusimama kwa miguu yetu wenyewe huku tukiwa na ujasiri wa kuwa na Yesu Kristo moyoni, tumezidi kuwa na mashaka na hofu ndani ya mioyo yetu ya kuwatukuza watu kuliko Yesu Kristo.
Tumezidi kuwa tegemezi kwa wengine siku hadi siku pasipo wenyewe kusimama kwa miguu yetu, sababu inayotufanya tuwe hivi ni wale wanaotuongoza hawataki tumjue Mungu wetu na tukaweza kujisimamia wenyewe na kujiombea wenyewe.
Asiyetaka uwe na uwezo wa kusimama mwenyewe anafikiri ukiweza kusimama kwa miguu yako utamzidi akili za kushindwa kukuendesha anavyotaka yeye. Anachokifanya kwako ni kukupa mafundisho mengi ya kumfanya umwogope yeye kuliko Mungu wako.
Najua unajua wapo wazazi ambao wametengeneza mazingira ya kuogopwa sana na watoto wao, yaani kama ni baba akiingia ndani watoto wote wanajifanya kama wajinga fulani wasioweza kusema chochote.
Mazingira yale yamewafanya watoto hawa hata wakiwa na kitu cha kusema wanashindwa kwa sababu hawajafundishwa kusimama wenyewe kama wenyewe. Inafika wakati wanakutana na changamoto huko nje wanashindwa kukabiliana nayo, na wakifikiri kwenda kwa baba kuomba msaada wanaona kama simba yupo mbele yao.
Wengine wamefundishwa wasifanye jambo bila kuuliza, mfano halisi; nimekutana na wamama wengi sana kwenye maduka wanashindwa kuongea biashara na mtu mpaka mume wake awepo. Yaani huyu mwanamke anakuwa dukani kama urembo tu, maamzi yeyote hata madogo sana ambayo hayahitaji akili kubwa sana hataweza kuchukua hatua yeyote ni mpaka mume wake awepo.
Tunaweza kusema ni sawa wanaume hawa wapo sahihi lakini ni ulemavu mbaya sana, vipo vitu vya msingi vitapotea kwa sababu umelemaza akili/ubongo wa huyu mwanamke aliyeoko dukani. Vizuri kushirikishana vitu kwa pamoja ila sio kumfanya mtu ashindwe kufanya kitu bila wewe kuwepo.
Ikitokea siku haupo hata kama mambo yanaharibika hayataweza kurekebishwa mpaka utoe kauli yako, je kama upo mbali na eneo hilo na kwenye simu hupatikani si ndio itakuwa hasara kwako?
Tunaweza kutengeneza mazingira magumu tukifikiri ni njia sahihi ya kujenga, kumbe tunawafanya wengine washindwe kujitegemea wenyewe hata pale wanapokutana na hatari kwenye maisha yao watashindwa kujiokoa.
Umeokoka una miaka karibia mitano au kumi, lakini huwezi hata kujiombea mpaka ukamwone mchungaji wako akuombee. Huu ni ulemevu mbaya sana wa kiroho alafu ukitoka hapo unasema kanisani kwetu kuna upako mwingi sana kupitia kwa nabii/mtume/mchungaji wetu.
Nia ya Mungu ni uwe na uwezo wa kusimama kwa miguu yako mwenyewe, mchungaji/mtume/nabii/mwalimu yupo kukusaidia wewe kuelewa yale usiyoelewa. Yupo kukuongoza na kukusaidia baadhi ya maeneo ambayo Mungu anamtumia kulifikisha kundi salama msije mkatawanyika njiani.
Sasa kama mchungaji kazi yake ni kuwafanya mmtegemee yeye tu, ni hatari kubwa sana kwenu, kama ni kondoo basi hawachungi majani mpaka wamelishwa mdomoni. Ni nzuri kwa wale wachanga wa kiroho ambao hawajui mbivu na mbichi, ila kadri siku zinavyoenda wanapaswa kuwa na uwezo wa kujisimamia wenyewe.
Siku mchungaji/nabii/mtume/mwalimu/mwinjilisti wenu hayupo karibu na ninyi kama Musa kwa wana Israel mtamwomba Haruni awatengenezee NDAMA mmwabudu kama Mungu wenu. Kumbe hapo mnamwabudu mungu mwingine ambaye atasababisha chukizo baya kwa Mungu wa kweli.
Hebu tuone Mungu anasemaje kuhusu hili;Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe. Naye aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami. EZEKIEL. 2:1-2 SUV.
Mungu anakutaka usimame kwa miguu yako mwenyewe ili aweze kukutumia kwa kile amekuleta hapa dunia, Mungu anataka utayari wako wa kusimama ili aanze kukutumia katika huduma aliyoweka ndani yako.
Kuitika kwako na kusimama mbele za Mungu, inategemea sana ukuaji wako wa kiroho, unapaswa kuwa msomaji wa Neno la Mungu. Ili kadri unavyozidi kumjua Mungu wako uwe na uwezo wa kujitegemea hata kama kiongozi wako wa kiroho akiwa mbali nawe, Mungu aweze kukusaidia wewe kama wewe.
Ukuaji wako wa kiroho hautokufanya umdharau kiongozi wako wa kiroho, huo ni wasiwasi wa kiongozi ambaye hatumikii kusudi la Mungu. Kusudi la Mungu ni ili wewe uwe na uwezo wa kusimama kwa miguu yako mwenyewe, ndio maana amekupa kiongozi wa kukusaidia kukutoa tongotongo kwenye macho.
Bidii yako ya kumjua Mungu kupitia Neno lake, ikufanye uwe na uwezo wa kusimama, huko ndio tunaita kukua kwa mtu kiroho. Sio miaka nenda rudi upo vilevile hata ukisikia bundi analia dirishani unaanza kuhaha na kuanza kutafuta msaada wa wengine. Huo ni utoto wa kiroho uliopitiliza kupita kiasi yaani bundi tu anakutoa jasho na kuanza kutafuta msaada!!
Hakikisha sehemu unayosali inakufanya ukue kiroho na sio uwe tegemezi chini ya mtu fulani, ukiona umedumaa kiroho na huna uwezo wa kusimama kwa miguu yako mwenyewe. Tafuta msaada wa haraka sana, mlilie Mungu wako aweze kukusaidia, biblia unayo mikononi mwako isome kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Neno la Mungu linakupa uwezo wa kusimama kwa miguu yako mwenyewe, nakueleza kitu halisi kabisa. Kusimama kwa miguu yako mwenyewe ni muhimu sana, itakupa kuwaheshimu hata hao wanaokubana uwe tegemezi kwao, itakupa kuwasaidia na wengine ambao bado wapo kwenye vifungo.
Bila shaka kuna kitu umekipata kupitia ujumbe huu, endelea kutafakari haya uliyojifunza ili kuhakikisha yamekaa moyoni mwako ipasavyo. Usikimbilie kujihesabia haki, kama huna uwezo wa kumweleza Mungu shida zako na ukaamini amekusikia, uwe na uhakika bado ni tegemezi.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.