Bwana Yesu asifiwe mwana wa Mungu, siku nyingine tena njema kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona tena, nikutamkie uzima wewe uliyeamka unajisikia kuumwa na nikumbushe kwamba usiache kumzalia Bwana matunda hata kama unakutana na changamoto.

Kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu, Mungu anazidi kukupa neema ya kuyajua maandiko yake Matakatifu. Kujua kwako maandiko Matakatifu ndio inakupa kumjua Mungu wako vizuri, na kadri unavyozidi kujifunza zaidi ndivyo unavyozidi kuelewa mengi zaidi.

Kwa kuwa Roho Mtakatifu yu ndani yako, anakusaidia kukufunulia zaidi Neno la Mungu ukazidi kuelewa vizuri zaidi. Usije ukafikiri unavyozidi kufanikiwa katika eneo hilo utaacha kukutana na changamoto katika maisha yako ya wokovu.

Wapo watu pamoja na kujua kwao Neno la Mungu, watakuona huelewi chochote wao ndio wanaolewa Neno la Mungu. Unaweza kuhangaika usiku na mchana kujaribu kuwaelewesha waelewe kile Mungu anazungumza juu yake. Hawatakaa wakuelewe na usipokuwa vizuri unaweza kuanza kuona wewe ndio labda haupo sawa.

Kuna maeneo watu wamefungwa fahamu zao wasipate kuelewa vizuri Neno la Mungu, utakaa ukipigizana nao kelele. Lakini unaweza ukashindwa kwa sababu jinsi unavyoona wewe, wao hawaoni kabisa na Usifikiri wanajifanyisha la hasha walipo ndio ufahamu wao umeishia hapo.

Hujawahi kuona mtu anaheshimu dini yake kuliko hata Mungu, yaani anaweza kuwa anafanya dhambi bila uoga wowote. Ila ukigumsa kwenye dini anaheshimu sana na anatii sana utafikiri dini ndio yenye mbingu.

Pamoja na wengine hawataweza kukuelewa hata kama upo sahihi kupitia Neno la Mungu, bado wale ambao wamesimama na Mungu katika roho na kweli. Ukisema Neno la Mungu linasema hivi na vile, watakuelewa unachokisema ni kweli, na wataheshimu hilo.

Nakueleza haya ili uelewe, ili ukikutana na changamoto kama hii usiweze kushangaa sana. Wapo watu wamefungwa ufahamu/akili zao wasiwe Kumwelewa Mungu kupitia Neno lake, usifikiri wanaobisha hivyo hawasomi Neno la Mungu. Wanasoma vizuri sana na tena wamekariri na baadhi ya mistari, ila wanavyoelewa wao sivyo Mungu anataka.

Roho Mtakatifu ni wa muhimu sana sana kuwa naye, narudia tena Roho Mtakatifu kuwa ndani yako ni wa umhimu sana. Unaweza kujifariji kwa namna yeyote ile, ila umhimu wa Roho Mtakatifu kuwa ndani yako ni mkubwa mno. Na huyu Roho Mtakatifu hakai mahali pa chafu, kama unatenda maovu uwe na uhakika hachangamani na hayo.

Kitu kingine omba sana Mungu afungue ufahamu wako, moyo wako ukifunguka utaona mabadiliko makubwa sana ndani yako. Kazi ya kufungua moyo wa mtu ni ya Mungu pekee, wengine wamefunguliwa baada ya kujua Neno la Mungu na wengine wamefunguliwa baada ya kumdai Mungu haki zao kwenye maombi kupitia Neno la Mungu.

SOMA: Madhara Ya Mtu Kufungwa Ufahamu/Akili Zake Ndani Ya Moyo Wake.

Nilieleza kwa upana sana kwenye somo la Madhara Ya Mtu Kufungwa Ufahamu/Akili Zake Ndani Ya Moyo Wake. Kama hukulisoma hilo somo ukifungua hayamaandishi ya kijani utasoma zaidi. Ninachotaka ni uelewe kwamba kuna maeneo magumu utakutana nayo ambayo utahitaji neema ya Mungu kumweleza mtu akuelewe, itahitajika neema ya Mungu watu kujua jambo unalopitia ni Mungu amehusika mwenyewe uwe hivyo.

Neno la Mungu linahitaji ulitilie maanani, na uliamini, usipoyaamini maandiko Matakatifu utaendelea kushikilia misimamo yako potofu. Hakuna utakivuna kwenye Neno la Mungu, ndio matokeo ya wengi wanasoma biblia lakini bado wanaendelea kusimamia hata yale ambayo Mungu anayakataza.

Ukielewa wewe Neno la Mungu hata kama upo katikati yao na wanajua ni mwenzao, watakuona umepotoka, upaswa kurejeshwa upya ndani ya kundi. Pamoja na hayo isikuvunje moyo kama unajua upo ndani ya kweli ya Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.