Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Kumekuwa na wimbi kubwa sana la watu kufikiri Mungu anaweza kuwa mbabe na mkatili sana, kufikiri kwao huko kunahusiana na kutomjua Mungu vizuri. Wangemjua vizuri wanayemtumikia wasingekuwa na wasiwasi mkubwa kiasi kile, sawa na baba/mama yako hupaswi kumwona ni mtu fulani wa kutisha sana.

Mungu sio mkatili kiasi kwamba anaweza kukupa jambo la kufanyia kazi wewe alafu akakuacha njia panda bila kukupa maelekezo ya namna ya kufanya hilo jambo. Wala Mungu hawezi kukupa jambo la kuchukua hatua za haraka au hatua za siku zijazo, baada ya hapo ikatokea akakuacha kwenye utata huo wa kushindwa cha kufanya.

Naona hujanielewa vizuri, nasema hivi; Mungu kuruhusu Mariam apate mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, malaika aliyeleta ujumbe wa mariam kushika ujazito kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Hakumwacha Mariam kwenye utata, badala yake Mariam alipoona hilo jambo lina utata kwake alimhoji na akamjibu vizuri, kwa kumpa maelekezo ambayo Mariam hakuwa na mashaka tena.

Mungu kuruhusu Mariam apate mimba, hakuruhusu Yusuf abaki kwenye utata wa kumwona mke wake mtarajiwa ana ujauzito ambao yeye hakuhusika nao. Pale Yusuf alipodhamiria kumwacha Mariam kwa siri, Malaika alisema naye kwa njia ya ndoto kuwa asimwache Mariam, kwa sababu ujazito alionao umetokana na uweza wa Roho Mtakatifu.

Rejea;Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe; asimjue kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU. MATHAYO 1:18‭-‬25 SUV.

Haikutokea tena Yusuf aanze kujiuliza inawezekana vipi Mariam apate mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu?!, haikutokea aanze kujiuliza huyo Roho Mtakatifu ndio yukoje?. Kama ilivyo leo wengi wanasema ingekuwa mimi nisingekubali, Mungu anajua nia zetu, hawezi kukupa maelekezo na jambo lenye utata Kwako bila kukusaidia uelewe.

Mungu hawezi kukuletea huduma alafu akakuacha kwenye utata wa kushindwa cha kufanya, Mungu atakupa maelekezo yasiyo na ukakasi juu yako. Haijalishi hilo jambo unaliona ni kubwa sana kwako, uwe na uhakika Mungu akikupa ujue akakuamini.

Tunamwona mtu mwingine Yona, aliyepewa kazi na Mungu. Lakini Yona akataka kukimbia asiende mahali alipoambiwa aende kuhubiri habari njema. Hakujua Mungu akishasema amesema, Mungu alihakikisha anafika mahali ambapo alimtaka aende.

Rejea;Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu. Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA. Lakini BWANA alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika. Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani? Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu. Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata. Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka. BWANA akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku. YONA. 1:1‭-‬4‭, ‬8‭-‬9‭, ‬11‭-‬12‭, ‬15‭, ‬17 SUV.

Unaweza kusoma sura nzima ukapata hiyo habari vizuri, mimi nimekupa mistari michache kukuonyesha kile nakueleza hapa. Pamoja na Yona kuona kwenda nchi hiyo itakuwa ngumu kwake, kukimbia kwake hakukubadilisha uamzi wa Mungu. Mungu kumthibitishia kuwa yeye ndiye, umeona tafrani iliyotokea ndani ya meli mpaka ilitaka kusababisha ajali mbaya, kwa sababu ya mtu mmoja aliyepewa wajibu akataka kukimbia.

Unaona ni jinsi gani Mungu akikupa jambo kupitia Neno lake, anajua namna ya kwenda kulifanya yeye. Hata kama mazingira uliopo na unayoenda ni magumu kiasi gani, yeye atasimama na wewe mpaka jambo hilo linafanikiwa. Haikuwa na sababu Yona kumezwa na samaki, ni uoga tu wa kibinadamu ulimfanya hivyo, ila mwisho wake alikubali mwenyewe.

Inakuwaje wewe leo Mungu anasema na wewe, badala ya kusikiliza maelekezo kutoka kwake, unaanza kukosa usingizi na kubaki njia panda pasipo kumuuliza Mungu itakuwaje hili. Hivi unafikiri akina Sarah, Elisabeth na mke wake na Manoa, kukaa kwao bila watoto miaka mingi. Siku wanapewa taarifa ya kupata watoto, unafikiri jambo hili liliwafanya wakose amani na kupata mihangaiko mikubwa ndani ya mioyo yao? Lazima kuna namna ambayo Mungu aliiweka ndani yao wasiwe na mashaka yasiyo koma.

Mungu akisema na wewe uwe na uhakika hilo jambo litatimia, haijalishi litachukua muda gani, lazima litimie. Kama unabisha mtazame Yusuf alivyouzwa utumwani kwa ndoto yake aliyompa Mungu, kumbe ndio ilikuwa kwenda kutimia kwa kile Mungu alisema naye.

Unaweza kumwona Daudi, pamoja na Samweli kumpaka mafuta ya kuja kuwa mfalme. Alipita kwenye mateso mengi sana baada ya kumuua Goliati, Sauli alimtafuta sana aweze kumuua, hiyo haikuweza kumkatisha tamaa Daudi. Kuteseka kwake kote alikuwa kwenye maandalizi ya kuikabidhiwa nchi kubwa.

Usiwe na wasiwasi Mungu anaposema na wewe kuhusu Jambo lolote lile kupitia Neno lake, kama hujamwelewa vizuri muulize kama alivyofanya Mariam kumhoji malaika aliyemletea ujumbe wa yeye kushika mimba. Malaika naye hakusita kumweleza jinsi itakavyokuwa, unaweza kuona jinsi gani mambo ya Mungu yalivyo hayana ugiza mnene wa kushindwa kukupa maelekezo juu ya lile linalokuhusu.

Mungu akiona bado humwelewi atazidi kurudia kukuita tena na tena kama alivyofanya kwa Samweli, pamoja na kutoelewa sauti ya Mungu. Alipata mtu wa kumwelekeza namna ya kuitika, Mtu huyo si mwingine bali ni Eli.

Rejea;basi, wakati huo BWANA akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa. Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena. BWANA akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. Basi Samweli alikuwa hamjui BWANA bado, na neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. BWANA akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa BWANA ndiye aliyemwita yule mtoto. Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake. 1 SAM. 3:4‭-‬9 SUV.

Napenda uelewe hili, Mungu akisema na wewe kuna maelekezo atakupa, hawezi kukuacha hewani ukabaki huelewi chochote. Atatumia namna nzuri ya kuelewa kile amekuambia, Mungu hawezi kuwa mkatili kwako.

Bila shaka kuna kitu umekipata kupitia ujumbe huu, hii ni faida ya kusoma Neno la Mungu. Pasipo Neno la Mungu hatuwezi kuondoka kwenye uchanga wa kiroho, ili kuzidi kumjua Baba yetu aliye mbinguni, lazima tuwe na bidii ya kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.