Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona tena leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Safari hii ya wokovu inaweza ikafika wakati ukaona njia uliyoifuata huenda ulikosea, mawazo haya yanakuja pale unapokuwa katika safari hii ukakutana na watu wanaokuona ulipo sio sahihi. Ila wao walipo ndio sahihi, na wanakutaka ufuatane nao katika kile wanaamini wao.

Usipokuwa na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako na usipokuwa na misingi mizuri ya imani ya Kristo, utafika wakati utaona wanayosema ni kweli kabisa. Badala ya kukazana kuwaambia maneno ya Mungu yanayoweza kuwavuta waje upande ulio sahihi, wataanza wao kukuvuta wewe. Maana tayari watakuwa wamekuzidi uwezo wa hoja, na ukaachia hoja zao zikaushika moyo wako.

Unaweza kuwaambia Neno la Mungu linasema hivi, watakujia na andiko lingine humo humo kwenye biblia, wakikikuonyesha haupo sawa. Kumbe wao ndio hawapo sawa maana walivyoelewa ni tofauti na Neno la Mungu linavyosema, maana ufahamu wao umefungwa wasipate kumjua Mungu wa kweli.

Rejea; Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. EFE. 4:17_18 SUV.

Ndugu yangu unapaswa kuelewa vizuri haya mambo ili unapokutana na changamoto kama hii usione imani yako haipo sawa, maana wana maneno mengi kiasi kwamba unaweza kujihisi wewe ndio umepotoka. Nakuhakikishia kama mchanga kiroho wanaweza kukuchota ufahamu wako, maana watakupitisha humohumo kwenye biblia yako.

Unachopaswa kuelewa ni hichi;Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Mathayo 13:15 SUV.

Mioyo yao kuwa mizito;maana yake hawawezi kuelewa Neno la Mungu, wanachoamini wao ndio watabaki nacho kuamini wapo sahihi na wengine wamepotoka. Ukitaka kuwaleta kwenye mstari sahihi wanakuwa wabishi na kuona unapowapeleka sio mahali sahihi kwao.

Masikio yao kutosikia;sio kana kwamba hawasikii kabisa, kusikia wanasikia ila wanachokisikia hawakielewi. Na ukijaribu kuwaelewesha vizuri wanaibua hoja za kuikataa kweli ya Mungu, unaweza kufikiri labda wanafanya makusudi la hasha ndivyo wanavyoamini wao. Ndio maana mtu wa namna hii akishaponywa masikio yake ya ndani akaupokea wokovu halisi, utamwona anavyoshuhudia alivyokuwa mbishi.

Macho yao kutokuona;usifikiri kwamba ni vipofu wa mwili, kimwili wanaona kabisa, ila macho yao ya ndani yamepofushwa hata wanapotazama hawaoni kile kilicho sahihi. Bali wanakuwa wanaona kile kisicho sahihi kwao, wao wanaona kipo sahihi. Utapigizanao nao kelele sana wakuelewe ila hawatakuelewa mpaka pale Mungu atakapoingilia kati.

Unapaswa kuomba Mungu akupe stamina za kuwaelimisha kuhusu Neno la Mungu watu wa namna hii, vinginevyo utaanza kutukanana nao matusi mabaya na kumkosea Mungu wako. Maana wanauzi kuliko unavyoweza kumwelezea mtu akakuelewa jinsi unavyojisikia moyoni mwako.

Ashukuriwe Mungu atupaye kufahamu wa kutusaidia katika haya yote, katika hili Mungu ametupa Neno lake kutusaidia wana wake namna ya kupambana na watu wa aina hii. Ndio maana unapaswa kusoma Maandiko Matakatifu yaweze kukupa uwezo wa kukabiliana na kila mazingira unayoweza kukutana nayo katika kumtangaza Yesu Kristo.

Rejea; Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi. Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli; wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake. 2 TIM. 2:23‭-‬26 SUV.

Hupaswi kuwa mgomvi ndugu yangu, mtumishi mwenzangu, mwamini mwenzangu, na mtenda kazi katika shamba la Bwana. Bali unapaswa kuwa mvumilivu, na kuendelea kuwaonya na kuwafundisha kweli ya Mungu iliyofunuliwa kwako ukaelewa. Hata wewe ulikuwa upo gizani kama wao, ila Mungu amekufungua wewe ili upate kuwa chombo chema cha kuwasaidia wengine.

Kadri unavyozidi kuwapa elimu ya Mungu, na kadri unavyozidi kumwomba Mungu juu yao, wataweza kutoka kwenye mtego wa shetani. Unaweza kuona ngumu na taabu, ikiwa Mungu ameweka mzigo ndani yako, uwe na uhakika atakuwa nawe siku zote. Hata pale unapojisikia kuchoka yeye atakupa tena nguvu za kusonga mbele, Roho Mtakatifu yupo kuhakikisha unalitimiza kusudi lile aliloliweka Mungu ndani yako.

Kuwatukana sana matusi watu wa namna hii, haiwezi kuwavuta waje kwa Yesu Kristo, haiwezi kuwaondoa kwenye miungu ya mabaali, haiwezi kuwaondoa kwenye vitu vinavyomchukiza Kristo. Badala ya kuona wanapoenda sio sahihi, wataona mbona unafanana na wao maana na wao huwa wanatukana matusi.

Kemea kwa kiasi, kwa nia ya kuwarejesha kundini. Usikemee kwa nia ya kuwaondoa kabisa wasimjue Mungu wa kweli, kile kile kiasi chao cha kumfahamu Mungu. Unaweza kukitumia kuwaondoa kwenye giza, kwa ufahamu wao wanaweza kuwa wanajiona wapo sahihi kumbe sivyo.

Yesu Kristo alileta Neema ya wokovu ili kila mtu aipate, haijaja ili kanisa/dini/dhehebu fulani iwe nayo tu. Haijaja ili kabila fulani iwe nayo hiyo neema, ni haki ya kila mwanadamu atakayekubali kuwa Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yake.

Shida nyingine imekuja shetani anawatumia watumishi wake, kuwapotosha watu wa Mungu kupitia jina la Yesu Kristo. Wanalitaja jina la Yesu kumbe sio huyu aliyetufia msalabani, wanakuwa na yesu wao mwingine.

Hebu unganisha neema ya Kristo uliyoipata kwako, kusoma Neno la Mungu kwa bidii zote. Hakikisha unasoma Neno la Mungu ili kuendelea kujifunza mengi kuhusu imani yako, hii itakusaidia maeneo mengi katika wokovu wako, Neno litakusaidia mengi katika huduma yako.

Mpaka hapo utakuwa umepata kitu cha kukusaidia katika safari yako ya kuendelea kumzalia Mungu matunda yaliyo mema, kile umekipata kitumie vyema ili uweze kuona mabadiliko katika maisha yako ya wokovu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Samson Ernest.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.