Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona tena leo. Ni kumshukuru Mungu kukupa nafasi hii iliyotamaniwa na wengi ila haikuwezekana kuifikia.

Tunajitengenezea sababu nyingi sana kiasi kwamba zingine sio tena sababu za kutuzuia tusifanye vitu vya msingi, bali zimekuwa ni sababu ambazo ni uzembe wetu wenyewe kushindwa kuheshimu muda wetu na kushindwa kupangilia vizuri baadhi ya shughuli zetu.

Mara nyingi nimewaambia watu, kama huwezi kuingia kwenye mitandao ya kijamii siku nzima kwa sababu umebanwa na majukum, kama huwezi kupokea simu yako kwa kubanwa sana, kama huwezi kujibu sms yeyote kwenye simu yako wanazokutumia marafiki na ndugu zako. Hapo tunaweza kusema kweli huyu mtu kazi anayofanya haiwezi kumpa muda wa kusoma Neno la Mungu.

Lakini cha kushangaza ni hichi, huyu mtu anayekuambia hawezi kusoma Neno la Mungu na hana muda kabisa wa kufanya hivyo kwa sababu ya kubanwa na majukum. Huyu mtu ndiye unamkuta kwenye mitandao ya kijamii, anaingia na kutoka, yaani haipiti masaa mawili hajachungulia simu yake.

Huyu huyu anayekuambia hana muda wa kusoma Neno la Mungu amebanwa na majukumu mengi, unamkuta kwenye mazungumzo na marafiki zake. Ambayo hayo mazungumzo anaweza kuwaambia nina kazi natakiwa kufanya, badala yake siku inaisha kwa kupiga soga za hapa na pale.

Mwingine anakuambia nipo chuo/shule siwezi kuwa na muda wa kusoma Neno la Mungu, hivi kusoma Neno la Mungu ni jambo kubwa sana linaloweza kuvuruga masomo ya mtu? Kusoma Neno la Mungu kwa sura moja/mbili huwezi maliza dakika 30. Lakini mtu anakwambia maneno mengi ambayo mengine unaona nafasi aliyompa Mungu moyoni mwake ni ndogo sana.

Mwingine anakwambia nakaa barabarani kwenye foleni muda mrefu sana siwezi soma Neno la Mungu, hapo ana smartphone yake ambayo anaingia kwenye magroup ya wasap na kujibu sms mbalimbali ila Neno la Mungu hawezi. Hiyo simu yake inaweza kumsikilisha audio ya kitabu anachotaka kukisoma, hilo hilo gari kama ni la kwake anaweza kuchomeka simu yake akasikiliza audio ya biblia akaweza kujenga umakini wa kulitafakari Neno la Mungu wakati anaendelea na safari.

Unaweza kuona hakuna mahali kuna ugumu wa kukuzuia kusoma Neno la Mungu, ni vile unaona kusoma Neno la Mungu ni mzigo kuliko kusoma hadithi mbalimbali kwenye mitandao. Mwingine humkosi online wasap, facebook na instagram ila kusoma Neno la Mungu anakuwa hana muda kabisa.

Atakwambia huko si naingia na kutoka, kwani kuingia ukafungua biblia yako uliyonayo kwenye smartphone yako kunakuwa na uzito gani. Zamani tulikuwa tunasema huwezi kutembea na biblia sehemu zote, ni sawa kabisa ila mbona leo biblia yako unaweza kutembea nayo mkononi mwako na kuifungua mara nyingi uwezavyo.

Badilika kutoka ndani ya moyo wako, hutoona tena mzigo wa kusoma Neno la Mungu badala yake utaona ni kama chakula chako cha tumbo cha kila siku. Usipokipata siku hiyo unahakikisha kesho hulali njaa, maana kulala njaa siku nyingi itakupelekea kupoteza uhai wako, na hakuna anayekubali kufa kirahisi hivyo.

Muda unao wa kutosha ndio maana unapata nafasi ya kwenda kula chakula cha tumbo, chakula cha kiroho kwanini ukikosee muda? Lazima ushtuke hiyo hali sio nzuri, mwongozo wa maisha yako kiroho upo ndani ya maandiko Matakatifu. Hakikisha popote ulipo unasikia kelele za kusoma Neno la Mungu pale unapoona siku inataka kukatika bila kusoma biblia yako.

Hili zoezi nimeliweka kipaumbele tangu mwaka 2015, sijawahi kujipa sababu ya kukosa kusoma Neno la Mungu isipokuwa siku za jumapili nimezipa kutembelea ndugu na kutafakari yale niliyojifunza kwenye ibada ya pamoja. Ila siku zingine zote huwa nikikosa kusoma biblia ni uzembe wangu mwenyewe, na kwa mwaka siwezi kuruka sura hata moja kwa kitabu nilichopanga kukisoma na kukimaliza.

Hata kwako inawezekana ukatenga muda na kujiwekea mkakati wa kutokosa kusoma Neno la Mungu kwa siku, hata kama ujikute upo mahabusu/magerezani omba biblia usome. Maana zipo biblia za kutosha, piga kelele uletewe biblia usome, ona kama unapoteza kitu kilichobeba uhai wako usipokipewa kwa haraka.

Ukishajua umhimu wa Neno la Mungu utaanza kujipa ratiba zako bila kuzuiliwa na changamoto yeyote, na ushindi wako ndipo utaanzia hapo.

Bila shaka kuna kitu umekipata kupitia ujumbe huu, chukua hatua za kujiweka vizuri katika hili eneo la kusoma Neno la Mungu kila siku. Hakikisha unakuwa umekolea haswa katika eneo hili la kusoma Maandiko Matakatifu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia usikwame njiani katika kusoma kwako Neno la Mungu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.