Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa na njema machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali cha kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.
Ukiwa na kiu ya kumaanisha kutoka ndani ya moyo wako unaweza kupokea chochote kile unachokitamani mbele za Mungu. Na kitu unachokitamani hakitakuwa nje na kile unachokisoma ndani ya biblia au hakiwezi kuwa nje na kile unachokiona kwa watumishi wengine wa Mungu.
Utatamani kitu cha kiMungu ulichowahi kukifundishwa, utatamani kitu cha kiMungu ulichowahi kukisikia/kukisimliwa, utatamani kitu cha kiMungu ulichowahi kukisoma mwenyewe ndani ya biblia. Kitu kile unavyozidi kukitamani ndivyo na bidii yako ya kumtafuta Mungu inazidi kuongezeka ndani yako.
Ukishaanza kutamani jambo/kitu chochote Mungu akufanyie au akutendee kama vile unavyotamani moyoni mwako, uwe tayari kufuata Neno la Mungu linavyokuelekeza na usije ukajizuia kwa mapokeo fulani ya dini yako yaliyo kinyume na maandiko matakatifu.
Unaweza kutamani kwa namna yeyote ile na usikipate hicho kitu kwa wakati ule unaotaka wewe, maana Mungu anajua kile kitu unastahili kwa wakati huo au wakati ujao. Vilevile Mungu anajua namna ya kukuandaa ukipokee kile kitu kwa namna ambayo hakitasumbua ndani yako.
Kadri unavyozidi kuweka bidii ya kumtafuta Mungu kwa kusoma Neno lake na kwa maombi, ndivyo unavyozidi kujiwekea mazingira mazuri ya kukaribia kile ulichokitamani siku nyingi kutoka kwa Mungu.
Kuna jambo limenitokea maishani mwangu hivi karibuni ambalo ninaweza kusema ni zawadi kubwa sana kwangu. Nimekuwa nasoma biblia kwa mfululizo tangu mwaka 2015 hadi 2017, mara chache sana imetokea sijasoma Neno la Mungu kwa siku husika. Kwa mwezi inaweza kutokea mara moja au mbili, lakini siku inayofuata nitahakikisha naunganisha kusoma sura niliyopanga niisome jana yake.
Utaratibu huu wa kusoma Neno la Mungu umenifanya niondoe taka taka nyingi sana nilizokuwa nazo kabla sijaanza kusoma Neno la Mungu. Nimejikuta nazidi kusikia kiu zaidi ya kusoma Neno la Mungu kadri siku zinavyozidi kwenda mbele. Nikimwona mtu hajisikii kusoma Neno na wala hana uzito wowote wa kuwa na ratiba ya kusoma Neno la Mungu, natamani mtu yule nimwambukize ile hali na kiu iliyo ndani yangu.
Kutamani kumwambukiza kila mtu kiu iliyo ndani yangu, nimekuletea kurasa za SOMA NENO UKUE KIROHO. Ambapo leo tupo ukurasa wa 203, ndio maana kila siku nimekuwa na mzigo wa kukusisitiza kila siku usome Neno la Mungu. Ndio maana tumekuwa na utaratibu wa kusoma Neno la Mungu kila siku isipokuwa jumapili kupitia group la wasap la Chapeo Ya Wokovu. Hii yote ni kukufanya uone umhimu wa kuwa na Neno la Mungu moyoni mwako.
Namshukuru Mungu pamoja na kuwa na changamoto mbalimbali katika maisha yangu ya kila siku, sijawahi kutamani kuacha kusoma neno la Mungu. Sijawahi kuacha kuwasisitiza watu waliokoka na wenye safari ya kwenda mbinguni kuacha kusoma Neno la Mungu. Namshukuru Mungu kuweka uzito wa hili jambo ndani ya moyo wangu, maana haikuwa rahisi kabisa. Huko nyuma nimejaribu kufanya hili zoezi ilishindikana kabisa, ila ilivyofika 2015 Mungu alifufua kile kilichofukiwa.
Nia ya kukushuhudia hayo nilitaka uone jinsi gani Mungu anaweza kukutengeneza vizuri kama utaamua mwenyewe kwa kusema sasa namfuata Yesu Kristo katika roho na kweli. Pamoja na hayo yote kuna kitu nataka kukuambia hapa, ambacho unaweza kujifunza na ukakifanyia kazi katika usomaji wako wa Neno la Mungu.
IKO HIVI; nilivyoanza kusoma Neno la Mungu agano jipya mpaka kumaliza kitabu chote, sikuwa na uelewa sana na niliona kama adhabu kusoma Neno la Mungu. Japo moyoni nilikuwa napenda sana, hata ile kuniambia nitoe upana wa mawazo kwa kile nilichojifunza haikuwa rahisi sana. Nilivyofika agano la kale, hapo ndio niliona mapichapicha kwa baadhi ya sehemu nyingi yaani niliona agano la kale ni gumu sana kuliko agano jipya.
Wale ambao tupo pamoja wasap group, wanakumbuka nimewahi kuwaambia hivi, mtu akifanikiwa kusoma agano la kale lote. Na akamwomba Roho Mtakatifu amsaidie kuelewa kile alichosoma, atatoka akiwa ameiva kisawasawa. Na agano jipya halitamshinda na ufahamu wake utaongozeka mara dufu katika usomaji wake wa Neno la Mungu.
Kuanzia kitabu cha mwanzo mpaka nafika kitabu cha Ayubu, sikuwahi kumwelewa Mungu kwa kiwango nilichokutana nacho kitabu cha Ayubu. Kitabu cha Ayubu kimefungua ufahamu wangu kwa kiasi kikubwa sana ambacho huenda nisiweze kukueleza vizuri hapa kama ninavyojisikia moyoni mwangu.
Nasikia furaha kuu sana ambayo sikuwahi kujua Mungu alivyo kwa wamtumainio. Kupitia kitabu hichi nasikia kuondolewa tongotongo nyingi sana. Hali hii ya kuondolewa tongo tongo ndio imenifanya nimwone Mungu kwa namna ambayo hakuna mtu yeyote ataweza kunibadilisha kwa namna yeyote ile.
Nakushuhudia kitu ambacho nimejionea mwenyewe, haijalishi watu watasema nini juu ya maisha yangu ya wokovu, haijalishi nitapatwa na nini katika maisha yangu ya wokovu. Bado nitajua Mungu ni yeye yule jana, leo na hata milele.
Unaweza kuona ni kwa kiasi gani Neno la Mungu linaweza kukubadilisha misimamo yako ya kutangatanga, na kubaki na msimamo uliosimama kisawasawa. Kitu ambacho unaweza usiwe nacho tangu kuokoka kwako, ila kupitia Maandiko Matakatifu unaweza kujiona wa tofauti sana.
Huenda mtu aliyeniona huko nyuma alitamani kuwa kama mimi na huenda aliniona nimefika. Ukweli hakujua, kumbe kuna eneo nakesha usiku na mchana nataka kufika, na hapa ni mwanzo tu. Natamani kuwa zaidi ya nilivyoshuhudia hapo juu, naamini Mungu ni mwaminifu kwangu kama Neno lake linavyonifundisha.
Kwanini ukubaliane na hali inayokuzuia kutosoma Neno la Mungu, linaloweza kukubadilisha ukawa kwenye mstari ulio sahihi na usioyumbishwa na kitu chochote kile. Amua leo kusoma Neno la Mungu, hujui utafunguka kwenye kitabu gani na kwa siku gani, songa mbele kwa bidii.
Bila shaka lipo jambo jema umeweza kujifunza kupitia ujumbe huu, fanyia kazi yale yameugusa moyo wako na yamenasa ndani yako. Utaona mabadiliko kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu CHAPEO YA WOKOVU, kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.