Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya na njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona. Sio kwa uwezo wa walinzi tuliowaweka magetini, wala sio kwa uweza wa makomeo/magufuli/vitasa tulivyoweka milangoni. Bali kwa uweza wake Mungu ametulinda na kutuamsha salama, sifa na utukufu tumrudishie yeye.

Kuna siku tunaamka hatujisikii kabisa kufanya yale tuliyozoea kuyafanya kila siku, unaweza kupanga ratiba zako za siku husika. Ila ukaamka mwili hutaki kabisa kufanya, kila ukijaribu kujisukuma unaona mwili unakataa.

Hali kama hizi zinamkuta karibia kila mtu ambaye ana mwili wa nyama, wakati mwingine unaweza kujitahidi kufanya jambo ambalo ulitaka kulifanya siku hiyo. Mwili wako ukawa unakugomea kabisa, na ukirajibu kuulazimisha unaona hata utendaji wako wa hilo jambo haupo vizuri kabisa.

Hali hii inaweza kukuta ukiwa hata kazini, ukaamka huna msukumo kabisa wa kufanya kazi zako, zaidi unaweza kuwa unajisikia kukaa tu. Na kukaa kwenyewe unaweza kuwa unatangatanga kimawazo bila utulivu wowote.

Hali kama hizi humjia mtu aliyeumizwa na jambo fulani katika maisha yake, inaweza kuwa ofisini kwake ameumizwa, inaweza kuwa biashara yake imepata shida, inaweza kuwa uhusiano wake wa uchumba umeleta shida, inaweza kuwa mahusiano yake ya ndoa hayapo vizuri, inaweza kuwa amezunguka sana na bahasha akitafuta kazi ya kufanya amekosa, inaweza kuwa hali yake kiuchumi/kifedha haipo vizuri na uhakika wa kula na kulipa kodi ya nyumba haupo.

Wengi tunapokuwa kwenye vipindi vya hali kama hizi, huwa tunaruhusu hali hizi ziondoe hamu ya kusoma Neno la Mungu, kuomba Mungu na kufanya kazi zingine za mikono.

Mwingine alivyoumizwa katika mahusiano ya uchumba kwa kuachwa na mwenzake, uhusiano wake na Mungu ulikatika hapo hapo. Mwingine mchumba wake asipokuwepo mahali alipotakiwa wawepo wote, na yeye hawezi kwenda sehemu hiyo. Hata kama inamsaidia yeye kiroho.

Hatuwezi kukataa wala hatuwezi kupinga haya yote, hakuna mwenye moyo wa ziada wa kuweza kuyahimili haya. Lakini wapo watu pamoja na changamoto mbalimbali za maisha, bado wanaweka bidii ya kumtafuta Mungu kwa nguvu zao zote. Lakini wengine wakishaguswa na hali moja wapo nilizokutajia hapo juu, ndio hawezi tena kufanya jambo lingine mpaka miezi au mwaka unaisha.

Ninalo jambo la kukuambia ikiwezekana tumia ushauri huu nitakaokumbia hapa, ili uweze kusimama katika eneo la kusoma Neno la Mungu bila kuachia njiani. Huenda hapo ulipo unasikia kelele za kuacha kusoma Neno la Mungu, na ukitaka kusoma unaona uvivu mkubwa sana. Wakati mwingine umesingizia ulikuwa upo bize sana, kumbe hukuwa na ubize wowote, ila ule utayari ndani yako haupo.

Ili uwe na uwezo wa kusoma Neno la Mungu kila siku bila kurukaruka pasipo sababu yeyote, uwe unajisikia ovyo/vibaya sana hakikisha unailazimisha akili yako itulie sehemu moja ili uweze kusoma Neno la Mungu. Hata kama unasoma huelewi unachokisoma, soma mpaka mwisho kama ulivyojipangia ratiba yako ya kila siku kisha rudia tena kusoma. Ukiona bado huelewi usikate tamaa wala usihamishe akili yako kufanya jambo lingine, tulia hapo hapo na narudia tena kusoma.

Kadri unavyozidi kufanya hilo zoezi la kurudia rudia kusoma, utaona taratibu ile hali inakuachia. Hata kama sio kwa kiwango kikubwa sana, kwanza utajisikia vizuri na kuona umetimiza ratiba yako ya siku. Usiangalie matokeo makubwa sana wakati huo wala usijilinganishe na siku zingine ukiwa vizuri.

Nakwambia hata kama upo hospital kama hujazidiwa sana, utashika biblia yako kuisoma, watu wanaweza kukushangaa kwanini upo kwenye hali fulani ya maumivu ila bado una moyo wa kufanya vitu vya kiMungu.

Kuna Jambo hili la msingi sana ambalo ukiwa nalo ndani yako litakusaidia sana, hakikisha unalipenda na kuliewa hili zoezi la kusoma Neno la Mungu.Usipopenda na kuelewa kwanini usome Neno la Mungu, hata kama utapigiwa kelele za namna gani, utaona unasumbuliwa na kukerwa.

Ukishaelewa na kulipenda hili suala la kusoma Neno la Mungu, wewe mwenyewe ukifika muda uliojipangia kusoma Neno la Mungu utaona kelele ndani yako. Na kuzituliza hizo kelele ni mpaka utakapo chukua hatua za kusoma Neno la Mungu, na ukishafanya hivyo utaona ghafla hizo kelele zitakuondoka na kubaki na furaha.

Penda kujisikuma na kujilazimisha kusoma Neno la Mungu hata kama hujisikii kufanya hivyo, nakwambia kila siku utakuwa unasonga mbele. Maana ukisoma sura moja leo, kesho hutorudia hapo, kama ulianza kusoma kitabu chenye sura 21 au 28. Mpaka kumaliza mwezi utakuwa umemaliza kusoma kitabu kizima.

Usidharau hatua zako, hata kama kuna siku inakukuta haupo vizuri sana, wewe jisukume kwa nguvu kufanya hata kidogo. Kesho hutorudia pale pale, utaenda hatua nyingine zaidi. Ila ukisubiri uwe sawa, kila siku utakuwa unasema hivyo bila kufanya chochote.

Bila shaka umepata kitu cha kukutia moyo na kukusaidia katika usomaji wako wa Neno la Mungu, usikubali kubaki na hali ya udhaifu kila siku. Kiri ushindi ndani yako, jiulize wengine wanawezaje kusoma Neno la Mungu kila siku alafu wewe ushindwe. Ina maana wanaosoma Neno la Mungu kila siku wao hawana Changamoto zozote za maisha la hasha ni kitu kisichowezekana.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovukwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kukujenga katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.