Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa kwetu aliyotuzawadia Mungu wetu. Tunayo kila sababu ya kumshukuru kwa nafasi nyingine ya kutengeneza pale tulipokosea kwa kutubu, vile vile tunayo nafasi ya kwenda kufanya vizuri zaidi ya jana.
Ukitaka kumua nyoka, mpige kichwa na hakikisha hakina uwezo wa kufanya chochote. Hata kama hutogusa mwili wake, we piga kichwa. Ukiona kulenga kichwa moja kwa moja itakupa shida, mdhoofishe kwa kumpiga mwili wake kisha malizia na kichwa.
Ukitaka kuondoa tabia ya uvivu, itafutia sababu moja yenye nguvu. Alafu itumie sababu uliyoipats kuilenge tabia ile inayokufanya uwe mvivu. Usihangaike na mambo mengi itakupa uvivu mwingine wa kuona kazi kubwa ya kufanya ili ufanikiwe zoezi lako, tafuta sababu moja tu.
Unaweza kusema kinachonifanya niwe mvivu wa kusoma Neno la Mungu, ni kushinda muda mwingi na marafiki wasiopenda kusoma Neno la Mungu. Ukitaka kusoma Neno la Mungu wanakupa maneno ya kukukatisha tamaa, ukitaka kupata utulivu wa kusoma Neno la Mungu unakuta wamekuzoga kiasi kwamba unaona shida.
Ukishajua tatizo lako lipo wapi, ni hatua moja kubwa sana ya kuelekea kulimaliza hilo tatizo. Utakachokifanya ni kuanza kuwakwepa hao marafiki zako, ukiona siku za nyuma ulikuwa unawashirikisha unaenda kufanya nini alafu wanakupa maneno ya kukuvunja moyo na wewe unaacha. Sasa anza utaratibu mpya wa kutowaambia kabisa unachoenda kufanya. Ondoka kimya kimya kama huwa ukitaka kuondoka unaaga, na ukiaga tu wanaanza kukuletea story za kuendelea kubaki au wanaambatana na wewe kuondoka wote.
Ukishaondokana na hilo tatizo la marafiki wasiopenda kusoma Neno la Mungu, anza kujishughulikia mwenyewe, angalia ni mstari gani wa biblia unaupenda sana na umeushika kichwani. Nataka usitazame mistari mingine, ni mmoja tu.
Bila shaka umeupata huo mstari na kama hujashika mstari wowote basi usiogope, fuatana nami utajua kitu cha kufanya. Huo mstari unaoupenda uwe sababu kuu ya wewe kuanza kusoma Neno la Mungu kila siku. Amini ipo mistari mingine zaidi inayoweza kukusaidia katika maisha yako zaidi ya huo, amini ipo mistari mingine zaidi ya kukujenga kiroho na kimwili zaidi ya huo unaoupenda.
Sasa huyu rafiki yako ambaye ni mstari mmoja, mtumie kumwambia Mungu kama mstari moja wa andiko takatifu unaupenda kiasi kile na umekuwa msaada kwako. Kwanini asikuwezeshe uwe na uwezo wa kuchota mistari mingine ya kukujenga kiroho na kimwili, bila shaka ni suala ambalo lipo ndani ya uwezo wako, ni wewe kuamua sasa.
Ikiwa unaamini mstari mmoja au tunaweza sema andiko moja, utashindwaje kuamini yapo maandiko Matakatifu mengi zaidi ambayo hujawahi kuyajua ila ni msaada mkubwa sana kwako, na yangeweza kukufungua ufahamu wako na kukupa mwanga wa kuweza kusimama na Mungu wako vizuri pasipo kuyumbishwa na yeyote.
Tupo na mstari mmojawa biblia kwa wewe mwenye huo mstari, na wewe ambaye huna huo mstari wa biblia. Unaweza kushika hili, kumwamini Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako, ikiwa unaamini kuhusu Yesu Kristo. Shida inakuja wapi usilione Neno lake ni la muhimu zaidi ili umjue vizuri unayemwamini?
Ondoka na hiyo sababu, maana usipomjua vizuri unayemwamini, ipo siku utadanganywa na shetani na utashangaa unaondoa imani kwa Mungu wa kweli. Na kupeleka imani yako kwa miungu mingine ya mababu na mabibi zako.
Utaanza lini sasa hili zoezi la kusoma Neno la Mungu baada ya kujua cha kufanya? Au umeanza kuwaza kesho au mwezi ujao ndio utaanza kusoma Maandiko Matakatifu. Hiyo ni roho nyingine inakushawishi ukubali kuanza kesho au mwezi ujao, ili ukikubali tu ujue hautakaa usome biblia. Utakuwa unaimba kesho kesho kesho mpaka mwaka unaisha hujafanya chochote.
Ukimua na ukasema kuanzia sasa naanza kutenga muda wa kusoma Neno la Mungu, na ukajiwekea mikakati ambayo inakuwa kama sehemu yako ya maisha. Nakwambia utafika mbali sana, hutojuta maamzi uliyochukua leo.
Teketeza uvivu wote kwa kutazama jambo moja tu ambalo ni mstari mmoja wa biblia kwa wewe ambaye unaujua. Na wewe ambaye hujui huo mstari unaweza kuondoka na kumwamini Yesu Kristo. Kama hayo yote huna, basi unahitaji Kumpokea Yesu Kristo aliye hai kama Bwana na Mwokozi wako.
Bila shaka kuna kitu umekipata kupitia ujumbe huu, cha kukusaidia kuanza kusoma Neno la Mungu. Na kuweka juhudi zaidi kwa wewe uliyekuwa unasoma kwa mazoea na kwa kawaida.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.