Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Leo nikuulize na ujijibu mwenyewe na kujipa alama ya mkasi au vema, ujipe maksi mwisho wa makala hii. Maana unajijua mwenyewe tangu uanze kusoma Neno la Mungu mpaka hapa ulipo leo. Kuna kitu gani umekipata ndani ya maandiko Matakatifu, au unasoma tu ili uonekane umemaliza kusoma kitabu fulani.

Inawezekana umesoma vitabu vingi sana vya biblia, je hivyo vitabu ulivyosoma vimebadilisha mitazamo yako hasi juu ya Mungu, je hivyo vitabu ulivyosoma vimebadili mapokeo yako ya dini na sasa unaweza kufikiri kama mtu asiyesimamia aliyomezeshwa. Bali ana uwezo wa kusimamia kile Neno la Mungu linasema nini juu ya maisha yake?

Kipi umekivuna ndani ya biblia tangu uanze kusoma, mabadiliko yapi unayaona kabisa hapo awali ulikuwa haunayo, ila sasa unajiona wa tofauti kabisa. Kipi unachojivunia katika usomaji wa maandiko Matakatifu, kipi ukikaa unajiona kweli Mungu amekubadilisha kwa asilimia fulani.

Tabia ipi utajivunia leo uliyoichota kwenye Neno la Mungu, kipi ambacho wale marafiki zako wanakiona kwako, kipi cha tofauti wazazi wako wakiona kwako, kipi cha tofauti mke/mume wako anakiona kwako. Au tangu uanze kusoma Neno la Mungu upo vile wala hakuna mabadiliko yeyote ndani yako.

Ukijiona hauna mabadiliko yeyote ujue unasindikiza watu, ili na wewe uonekane unasoma biblia kumbe una agenda zako tofauti. Lakini mtu aliye na kiu na nia ya kujua kilicho ndani ya biblia, lazima atakuwa ameanza kuona utofauti fulani ndani yake.

Utofauti wa mtu unaonekana kwa matendo yake, hata ule usikivu wake unaanza kuonekana tofauti na mwanzo alivyokuwa hasomi Neno la Mungu. Hata ile tabia yake ambayo ilionekana kushindikana kwake, kupitia Neno la Mungu inaondolewa kwake kwa kuchukua hatua na kubaki kama Mungu anavyotaka awe.

Moyoni mwako unasikia ujasiri kabisa mahali ulipo na kiwango ulichonacho tangu uanze kusoma Neno la Mungu? Kinaweza kumshawishi mwingine akatamani na yeye kuanza kusoma Neno la Mungu? Bila shaka unaweza kuwa na jibu, ila mbaya sana kama unasoma biblia yako kila siku, inakukataza kufanya jambo fulani baya. Lakini pamoja na Neno la Mungu kukutaza bado unafanya.

Itakuwa ajabu Neno la Mungu linakataza kufanya jambo fulani lililo kinyume na Mungu, unashindwa kuliacha kwa sababu dini yako inalifanya na kukubaliana nacho. Hapo unaweza kujipima na kujichunguza, inakuwaje unapingana na Maandiko Matakatifu na kuona dini yako ni bora zaidi ya Neno la Mungu.

Neno la Mungu halileti jeuri kama wengi wanavyofikiria, maana mtu akishaanza kuonekana amekua kiroho. Wale aliokuwa nao pamoja wanaanza kumwona anawasaliti na amekuwa jeuri, hataki tena kuwasikiliza na kufuata kile wao wanaamini.

Ukishachunguza maeneo yako, ukajiona tangu uanze kusoma Neno la Mungu huna mabadiliko yeyote na wakati mwingine umetumia nguvu nyingi kupingana na maandiko yanavyosema. Jua ipo shida ndani yako, shida ambayo inakutaka uchukue hatua za haraka kuiondoa.

Hakikisha Neno la Mungu linakutoa hatua moja kukupeleka hatua nyingine, iwe kiroho au kimwili, hakikisha kuna mabadiliko unayaona katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Neno la Mungu halipaswi kukufuata wewe unavyotaka bali wewe ndio unapaswa kulifuata lenyewe kama linavyokuelekeza.

Mwongozo na dira ya maisha yako ya wokovu, upo ndani ya Neno la Mungu, ukiona unayoamini ni bora zaidi kuliko Neno la Mungu basi utakuwa huna haja kutumia nguvu nyingi kupinga maandiko matakatifu. Usije ukawa unajifariji na kujivunia upo njia sahihi, kumbe njia uliyofuata inakupeleka jehanamu.

Neno la Mungu litusaidie na tuone mabadiliko tunavyozidi kulisoma, hakikisha unaliweka hili moyoni mwako. Usije ukawa msindikizaji tu wa wengine, unapaswa kusikia ndani yako umefunguka. Bila shaka ninaposema kufunguka moyoni mwako utakuwa unanielewa, ukishafunguka hekima na ufahamu juu ya maisha yako kiroho na kimwili unakuwepo, ukishafunguka kusamehe waliokukosea inakuwa sio tabu kwako.

Chochote kilicho ndani yako na kitanzi kwako, Neno la Mungu likiachiliwa kwako na ukalipokea pasipo vipangamizi vyovyote. Uwe na uhakika vichomi vya tumbo vilivyoletwa na kushindwa kusamehe, vitapona haraka sana.

Bila shaka kuna kitu umekipata na umetamani kiwe kwako, hakikisha kinakuwa kwako kweli, furaha yangu kukuona wewe una uwezo wa kusimama kwa miguu yako mwenyewe. Kama mkristo aliyemwamini Yesu Kristo aliye hai kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake, pasipo kuyumbishwa na imani yeyote potovu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovukwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.