Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali cha kuiona siku ya leo. Kibinadamu linaweza kuonekana ni jambo la mazoea kuamka kila siku kuelekea kwenye shughuli zetu, ila kwa mtu anayefikiri kwa kina hawezi kuona kupata fursa ya kuwepo leo ni kawaida.
Changamoto za maisha hazitakaa ziishe tukiwa kama wanadamu, kila mmoja anakutana na vikwazo mbalimbali kutokana na eneo alipo au kutokana na nafasi aliyonayo katika familia, nchi, au jamii. Kama ni mwanafunzi anakutana na changamoto kwenye masomo yake, kama ni ajira mtu anakutana na changamoto za kwenye ajira yake, kama ni biashara mtu anakutana na changamoto kwenye biashara zake, na kama ni kutafuta kazi napo mtu anakutana na changamoto za ajira.
Hakuna mtu aliye na nafuu sana ya maisha kuliko mwingine, wengine huwa wanafikiri kuwa Mtumishi/Mchungaji/Askofu/Padrii. Unakuwa umeipukana na changamoto za maisha, yaani mtu anaona kuwa mchungaji wa kanisa unakuwa hukutani na changamoto ngumu za kiuchumi.
Siku moja tukawa katika mazungumzo na rafiki yangu mmoja aliyekuwa anaokana kazi anayoifanya ameichoka. Wazo alilokuwa nalo ni bora awe mchungaji wa kanisa atakuwa anapata pesa kirahisi kuliko anavyoteseka sasa. Nilimsikitikia kwa sababu kwanza alifikiri kutumika madhabahuni ni kupata fedha, na pili aliongea kwa kujiamini na kunitolea mifano ya watu wanaowajua yeye ni watumishi wa Mungu na wana maisha mazuri.
Huyu ndugu ameutamani uchungaji kwa ajili ya kupata pesa za kujikimu, hebu vuta picha akaingia na fikra hizo. Huku washirika mkijua wana mchungaji mwenye wito wa kulitumikia kusudi la Mungu. Kumbe mwenzenu ana agenda tofauti, hebu fikiri sadaka zitakapokatika atakuwa bado ana moyo wa kuchunga kondoo wake au atakimbia.
Kila eneo unaloliona wewe ni zuri, fahamu kuna mtu/watu wamehusika sana kutumikia kusudi lao na kulifanya hilo jambo liwe zuri. Humohumo kwenye uzuri kuna changamoto nyingi sana, hakuna eneo lenye urahisi sana kama unavyofikiri wewe.
Ulipo unaweza kukutana na changamoto ngumu ambayo hata watu wanaosema wameokoka watashindwa kung’mua na kubaki kukuona utakuwa umemkosea Mungu wako. Maana wakijaribu kukuangalia ulivyo na jinsi mazingira ya jambo lenyewe lilivyokaa, wanaona kabisa huyu ndugu atakuwa amemtenda Mungu dhambi.
Hebu fikiri watu wanakufahamu kama mwana wa Mungu kwa jinsi matendo yako yalivyo safi mbele za Mungu. Ikitokea shida ya kiroho wanajua wewe unaweza kuitatua kwa kukabiliana nayo, na wewe moyoni mwako unashuhudia kabisa Mungu anakutumia katika maeneo fulani kumwakilisha yeye kusaidia watu wake. Alafu ikatokea ukapata jambo baya ambalo haliwezi kutatuliwa na mtu yeyote, na hilo jambo lililokupata wewe mwenyewe Mungu hajasema na wewe kama ilivyozoeleka siku zote.
Moyoni mwako utakuwa unajisikia hujamtenda Mungu dhambi, ila utakuwa na maswali kwanini hayo ya kupate. Unaweza kujipa majibu kutokana na Neno la maarifa lililo ndani yako, ila jamii inayokuzunguka haitaweza kukuelewa kirahisi kihivyo.
Lazima watu wajiulize inawezekana vipi mtu anayeombea watu wanapona yeye ameshindwa kujiombea apone, inawezekana vipi mtu anaombea wengine wanapona ila kuna ndugu yake ameshindwa kumwombea apone. Kuna vitu lazima wafike kipindi watu washindwe kung’amua kutokana na uhalisia wa jambo lenyewe.
Unaweza kuwa kazini kwako ukapewa kesi isiyo yako ukaonekana wewe unasema umeokoka kumbe mwizi, unaweza kuwa kwenye biashara zako ikatokea kitu ambacho watu wakasema wewe hujakoka. Lakini hayo yanaweza kukutokea kwa kusudi maalum kutoka kwa Mungu, ili kupitia wewe watu wajue kweli wewe ni mtu wa Mungu na Mungu anajivunia mtoto wake mwaminifu mbele zake.
Jiulize wakati watu wengine wanashindwa kung’amua kuhusu baya lililokupata, wewe utakuwa bado unamwamini Mungu na kutofikiri kutoka nje ya mstari wa Mungu? Maana yapo mambo yanakujia pasipo Mungu kusema na wewe chochote. Je kiwango chako cha Kumwelewa Mungu wako kitakuwa kinatosheleza kumwona Mungu ni yeye yule jana, leo hata milele? Au utatazama uzito wa tatizo lako na kumwona Mungu sio kitu tena na kutamani kugeukia miungu mingine!
Ustahimilivu wa haya yote ni lazima uwe umeshiba Neno la Mungu, Neno la Mungu litakujenga kwa kila eneo la maisha yako kuweza kumwelewa Mungu vizuri pasipo kuchanganywa na kelele za watu walioshindwa kung’amua kilichokupata.
Elekeza nguvu zako nyingi katika kulijua Neno la Mungu, kulijua kwako Neno la Mungu ni kwa kulisoma na kulitafakari kila wakati. Haya maisha yanaweza kukuambia una marafiki wengi na wazuri, ila likikutokea la kukutokea, watakukimbia wote na kukutaa kuwa wewe siye yule waliyekujua. Kadri unavyozidi kuongeza uaminifu mbele za Mungu, ndivyo unavyozidi kufanikiwa kiroho na kimwili. Ila mafanikio hayo hayatakaa yampendeze shetani, kupitia mafanikio yako utashitakiwa nayo.
Umejipanga vipi ndugu yangu katika Kristo, umejiwekea ratiba ya kusoma Neno la Mungu ili uendelee kukuza uhusiano wako na Mungu au baada ya kuokoka ndio umeona imetosha. Lazima ujue ulivyokoka kuna matunda unapaswa kumzalia Mungu, utamzaliaje matunda kama hutomjua unayemzalia?
Neno la Mungu ni uhai wako wa maisha ya wokovu, ukilipuuza kuna siku utaacha wokovu kizembe mpaka watu watakushangaa na utakuwa umesababisha jina la Yesu Kristo kutukanwa kwa ajili yako. Maana ndani yako hukuwa na stamina yeyote ya kuweza kuhimili mikimiki ya changamoto mbalimbali za maisha.
Bila shaka umeelewa umhimu wa kuwa na Neno la Mungu moyoni mwako ili uwe na uwezo wa kung’amua mambo ambayo kibinadamu yanaokane ni magumu. Lakini kwako utakuwa unaendelea kumtumainia Mungu wako, hata kama watu watakuwa wanakuona hustahili kulitaja jina la Yesu Kristo kwenye shida yako.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.