Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena bora kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, ni nafasi adimu sana kwetu, vyema tukaitumia vizuri kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.
Watu wengi wamekuwa na mawazo hasi kuhusu Neno la Mungu, anafikiri anaweza kusoma Neno la Mungu kwa siku chache akatosheka moja kwa moja. Bila kuhitaji kusoma tena Maandiko Matakatifu, ni kosa kubwa sana kufikiri hivyo, na ndio wengi tunalifanya.
Haitokei tu siku moja ukawa imara katika Neno la Mungu, unahitaji kujenga tabia ya kila siku kusoma Neno la Mungu. Tabia hii ndio itakusaidia kumairisha moyo wako, Neno la Mungu litazidi kuleta mabadiliko ndani ya moyo wako kadri siku zinavyozidi kwenda mbele.
Unaweza kusoma Neno la Mungu ukapata yale yanayokufaa kwa wakati huo, na unaweza kusoma Maandiko Matakatifu usione uzito wa baadhi ya mistari ya biblia. Lakini kadri unavyozidi kujifunza ndivyo unavyozidi kufunguka zaidi ndani ya moyo wako kwenye maeneo mbalimbali katika maisha yako.
Unaposikia Neno la Mungu ni jipya kila siku usije ukafikiri huwa linabadilika baadhi ya maneno, halibadiliki maneno wala maana. Ila Neno la Mungu linaonekana jipya kutokana na mazingira husika siku hiyo, si huwa unasikia watu wakisema sijawahi kufikiri Neno la Mungu linaweza kutolewa maana kama hii. Hapo uelewe hilo Neno limemwingia huyo Mtu kutokana na Mungu kumpitisha eneo halisi kupitia Neno lake.
Acha kujidanganya utaanza kusoma Neno la Mungu leo, alafu baada ya kusoma siku kadhaa hutokuwa na haja tena ya kusoma Neno la Mungu. Huko utakuwa unajidanganya, huwezi kupata kitu cha kukusaidia katika eneo fulani basi ikawa imetosha. Yapo maeneo mengi katika maisha yako yanahitaji kujengwa na kuimarishwa kila iitwapo leo.
Uzuri wake unavyozidi kujifunza Neno la Mungu kuna maeneo mengi uliyokuwa mchanga, utazidi kuondolewa uchanga huo hatua kwa hatua. Usifikiri uchanga wa kiroho unaondoka ndani mwa mtu kama ajali ya siku moja, huko ni kujidanganya ndugu yangu. Uchanga wa mtu kiroho unaondolewa hatua kwa hatua kutokana na bidii ya mtu binafsi.
Unaweza kubaki mkristo mchanga wa kiroho miaka yako yote, na uchanga wa kiroho unatofautiana kama ifuatavyo;
1. Kuna uchanga wa kiroho kwa yule aliyempokea Yesu Kristo siku sio nyingi.
Hawa wanajulikana na huwa wapo wazi kabisa kukueleza ukweli, na huwa wapo tayari kujifunza pale wanapopewa maelekezo sahihi ya kuchukua hatua. Wanavyozidi kujifunza huwa wanajisikia hamu zaidi ya kuendelea kujua mengi zaidi, na uzuri wake huwa hawana kiburi cha kuokoka muda mrefu.
Mara nyingi sana huwa wanawapita wengine uelewa na ujasiri juu ya imani juu ya Kristo kuliko aliyejiona ana miaka mingi ndani ya wokovu. Kiu ya kumjua Mungu ndio huwa inawafikisha mahali ambapo hata wale waliokoka siku nyingi hawakuweza kufika hapo. Na huwafikisha kwenye kiwango fulani ambacho wengi wao huwa wanakuwa watumishi wa Mungu wazuri sana.
2. Kuna uchanga wa kiroho kwa yule mkristo baada ya kuokoka aliona imetosha hahitaji kujifunza zaidi.
Huyu ni yule mtu baada ya kuokoka aliona imetosha hahitaji tena kujifunza mambo mengine zaidi, ndio wale unaowaona wazembe kwenye Neno la Mungu, ndio wale unaowaona wavivu kwenye vipindi vya mafundisho ya Neno la Mungu. Ndio wale wale utawakuta kwenye kundi la kupenda miujiza ya Mungu pasipo kujua hiyo miujiza imetokana na Mungu wa kweli au mungu mwingine.
Watu wa kundi hili wengi wao huwa hawana uwezo wa kusamehe waliowakosea, mioyoni mwao huwa wamejaa uchungu wa kutosamehe. Kundi hili ndilo huwa linajivunia miaka ya kuokoka kwao ila ukiwatazama matendo yao hayafanani na umri wanaokutajia wakiwa ndani ya wokovu.
3. Kuna uchanga wa kiroho kwa yule mkristo anayejiona anajua kila kitu hahitaji kujifunza zaidi.
Mtu wa kundi hili hana tofauti sana na kundi namba mbili, ila huyu anakuwa anaona anaelewa kila kitu, hawa mara nyingi ndio wale wanaoshikilia sana dini kuliko kumshikilia Yesu Kristo. Unakuta mtu ameokoka miaka mingi sana ila anajivunia dhehebu/dini yake tu, ukimhoji zaidi mbona dini yako haikusaidii kuacha dhambi anakuwa mkali, ukimwambia mbona dini yako haikusaidii kuweza kujisimamia kiroho kwa miguu yako mwenyewe anakuwa anajikanyaga tu.
Watu wa kundi hili ni wazuri sana kama wakifunguliwa fahamu zao wakatoka kwenye udini na kuamua kumtafuta Mungu wa kweli. Na wanakuwa mabalozi wazuri sana kuwaamsha wenzao waliolala kwenye usingizi wa dini.
Watu hawa hawa ni wagumu sana kubadilisha, kwa sababu wamemeza yale wanayoamini ndio kweli. Wapo tayari kupinga maandiko Matakatifu, ilimradi atetee kile dini yake ilimwambia ndio sahihi. Na hachelewi kukuambia hilo andiko umelitoa wapi wakati unamwonyesha katika limetoka kitabu fulani.
Watu wa namna hii unapaswa kusikiliza sana maelekezo ya Roho Mtakatifu, ndio uweze kuwapa maarifa ya kuwatoa kwenye eneo la udini/udhehebu, na kuwaleta katika njia sahihi ya Yesu Kristo.
Unapaswa kumwomba Mungu usiku na mchana afungue ufahamu wako uzidi kusoma Neno lake na kulielewa. Unavyozidi kujifunza Neno la Mungu ndivyo unavyozidi kujengeka zaidi na zaidi ndani ya moyo wako. Hutokuwa mtu mwenye tabia za kukurupukia utapeli wa mafundisho potofu, hutokuwa mtu wa kuhangaishwa huku na kule kwa elimu zisizofaa.
Pamoja na hayo yote unapaswa kuelewa Neno la Mungu ni kama chakula cha mwili wako, ambacho unaweza kula sasa hivi vizuri sana. Ila baada ya masaa fulani ukasikia njaa tena, ndivyo ilivyo na chakula cha KIROHO. Mwili wako wa ndani usionekana kwa macho ya nyama, unajengwa na Neno la Mungu, na tumbo la huo mwili ni moyo wako.
Bila shaka kuna kitu umekipata kupitia ujumbe huu, usiache kukifanyia kazi kile ulichojifunza siku ya leo. Tamani kumjua Mungu kupitia Neno lake.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma makala hii, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kukua kiroho.
Imeandaliwa na kuletwa kwako na Samson Ernest.
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
Blog; www.chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.