Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa kwetu wanadamu, Mungu ametupa kibali cha kuifikia leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote. Ni fursa kwetu kwenda kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.
Wengi huwa tunatamani kuwa watu wa namna fulani, ila tunapoanza hatua za kuwa jinsi tunavyotaka tuwe, huwa tunakutana na changamoto ngumu zinazotufanya tuone kile tulichokuwa tunakitamani kiwe kwetu kionekane hakiwezekani.
Wengi wanapokutana na changamoto ngumu, huwa hawana ujasiri wa kuendelea kupambana kuhakikisha wamefikia lengo lao. Badala yake wamerudi nyuma huku wanaendelea kutamani kilekile walichokianza na kukiacha. Wanapoona mwingine ameweza ambaye hawakutarajia kama na yeye angekuwa vile wao wanatamani, huwa wanaanza tena kwa upya ile safari waliyoikatisha.
Wanapoanza tena kwa upya huwa wanajikuta wanakutana na changamoto zilezile tena, na wakati mwingine zinazaliwa changamoto zingine mpya kabisa ambazo zinawafanya waone wanachokihitaji kwao hakiwezekani. Wanapoona tu hakiwezekani wanaacha tena kufanya au wanaendelea kufanya wakiwa wamekata tamaa, wanachoangalia wao ni ilimradi siku ziende basi.
Napenda kukusaidia jambo hili; vile unawaona watu walivyo na mafanikio fulani unayotamani wewe uwe nayo, hawakufanikiwa kirahisi kama unavyofikiri wewe kwenye ufahamu wako. Ukijaribu kumuuliza changamoto alizokutana nazo mpaka kufikia hapo, anaweza kukueleza vitu vingi sana. Ambapo vitu vingine vinaweza vikakufanya ukajiona mzembe sana tena wa mwisho wa kukata tamaa haraka.
Wakati mwingine ni muhimu kusikiliza shuhuda mbalimbali kuhusu wale waliofanikiwa kihalali kwa kile unachotamani ukifikie na wewe. Kutamani ninakokuzungumzia ni kule kufikia ndoto/malengo yako, yupo mtu ametambua kile Mungu ameweka ndani yake ila haoni afanye nini kukifikia pale, yupo mtu ana huduma ndani yake ila hajui atafikaje pale anatamani afike.
Yupo mwimbaji anatamani kuwa kama mwimbaji fulani, yupo mwalimu wa Neno la Mungu anatamani kufikia viwango kama vya mwalimu fulani, yupo mwinjilisti, mchungaji, mtume, nabii anatamani kuona akiwa katika viwango fulani alivyonavyo yule aliyefanikiwa zaidi yake. Kufikia sasa hivyo viwango, haiji kama muujiza, ni uaminifu na uvumilivu mbele za Mungu, ipo gharama mpaka mtu kufika hapo alipo.
Pamoja na hayo yote, lipo jambo kubwa lingine linalowasumbua watu wengi vichwa vyao na wamefika wakati wamevunjika mioyo yao. Kundi hili ni wanaopenda kusoma Neno la Mungu, anatamani kuwa kama fulani anavyosoma mistari ya biblia na kuifafanua vizuri kiasi kwamba alikuwepo wakati hayo maandiko Matakatifu yanaandikwa.
Sasa mtu anapojitazama mbona nimeokoka na nimejazwa na Roho Mtakatifu ambaye wengi wanasema ukiwa nayo atakusaidia kuelewa vizuri Neno la Mungu. Lakini unashangaa pamoja kuwa na sifa hizo zote, bado uelewa wako upo chini sana. Inawezekana kabisa ni mtumishi wa Mungu na una hudumu madhabahuni, ambapo kwa lugha nyingine unategemewa na watu uwape Neno la Mungu liweze kuwasaidia. Ila unakuwa chini sana sio vile unapenda uwe.
Wakati mwingine unasoma Neno la Mungu huelewi kama unavyoona wenzako wanaelewa na kuelezea vizuri kiasi kwamba unasikia kuguswa sana moyoni mwako. Unaona kabisa huyu mtu hakika ana Roho wa Mungu ndani yake, na sio kwamba anafafanua maandiko Matakatifu kisanii sanii la hasha, anaeleza mpaka wewe mwenyewe unaona kabisa kipo kitu cha tofauti ndani ya mtu yule.
Unapotazama hayo na ukajilinganisha na wewe inaweza kukuvunja sana moyo, ila ninachoweza kukuambia siku ya leo ni hichi, usivunjike moyo. Endelea kumtegemea Mungu aliyekuumba kwa mfano wake, yeye ndiye aliyekuokoa na kukufanya ulivyo. Elewa kufikia hatua fulani kuna hatua ndogo ndogo unapaswa kupitia ndipo uweze kufikia viwango unavyovitamani wewe.
Unyenyekevu, bidii, uvumilivu na utii wako mbele za Mungu, ndio utakaokufikisha hapo unapopatamani. Usichoke kujifunza Neno la Mungu kwa kisingizio cha huelewi kitu, nakwambia unajirudisha nyuma mwenyewe. Hebu we fikiri ukiacha ndio utaelewa au ukiacha utapata nini? Bila shaka ni hasara zaidi. Maana ungeendelea kusoma ungekuwa unapata vitu vichache vya kukusaidia kuliko unavyokaa husomi kabisa.
Unaowaona wewe wanasoma Neno la Mungu na kuelewa vizuri, hawakuanza hivyo moja kwa moja kwa kuelewa wala hawakuwa hivyo mwanzo. Ila wamepita katika mapito mengi mpaka kufikia hapo, muhimu kwako ni kuendelea kumwomba Mungu afungue moyo wako uelewe zaidi kile unasoma. Moyo wako ukifunguka, akili zako zitafunguka, ufahamu wako utapanuka zaidi na kuwa na uwezo wa kuelewa vitu vingi kwa undani zaidi. Ni suala la muda tu.
Jambo lingine ni hili, muhimu sana kujifunza kwa wengine, kama hutokuwa na tabia ya kujifunza kwa waliofanikiwa na waliokutangulia, itakuwa ngumu sana kwako kufika pale unapopatamani. Yule unaona kwako anafika kipindi anakuvunja moyo kwa jinsi anavyolinyambua Neno la Mungu hatua kwa hatua, huyo huyo awe mwalimu kwako na chachu kwako kufikia pale unapenda.
Mungu ameweka watu wake ili kuwasaidia wengine, ndio maana unasikia kupelea kadri unavyomtazama mwingine. Hiyo ni ishara njema kwako Mungu kukusemesha kupitia mwingine ili uwe na bidii zaidi. Usiwe mtu wa kubaki palepale kila siku, Mungu wetu ni wa viwango.
Unavyozidi kujifunza zaidi Neno la Mungu, hutokuwa kama ulivyokuwa jana, hajalishi unajiona vipi. Ila ukweli ni kwamba umeweka kitu cha tofauti sana ndani yako, tofauti kabisa na yule ambaye hasomi kabisa. Cha kuzingatia kwako ni kutokata tamaa.
Nina uhakika kabisa usipovunjika moyo wako, ukaendelea kuweka bidii yako katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Nina uhakika vipo vitu Mungu anaendelea kuvijenga hatua kwa hatua ndani mwako, ni wewe mwenyewe kuwa na muda wa kujitafakari na kujihoji ulivyokuwa jana ndivyo ulivyo leo? Tangu uanze kusoma Neno la Mungu mwezi uliopita upo vile vile? Bila shaka ni kitu ambacho hakiwezekani kwa mtu aliyeokoka na mwenye kiu ya Neno la Mungu.
Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia kuwa huna haja ya kudharau hatua zako ndogo ulizoanza nazo, umeona ni jinsi gani hupaswi kukata tamaa kutokana na uelewe wako mdogo wa Neno la Mungu ukijilanganisha na wengine. Endelea kumtegemea Mungu wako na kuweka bidii yako ya kujifunza Neno la Mungu kila siku.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu. Kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kukua katika usomaji wako wa Neno la Mungu.
Imeandaliwa na kuletwa kwako na Samson Ernest.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.