Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana, ameona vyema kutupa kibali kingine tena cha kuweza kuifikia leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, sio wote wamelala jana na kuamka leo wakiwa hai. Wapo waliolala moja kwa moja, ila mimi na wewe tumepata nafasi hii. Hebu tuitumie vyema kumzalia Bwana matunda yaliyo mema, hebu tuimie vyema kutengeneza uhusiano wetu na Mungu wetu.

Kuna hatua huwa tunafika tunajiona tumeshajua kila kitu, hatuhitaji tena kujua zaidi. Tunapofika hatua kama hii huwa dharau inatuvaa ndani mwetu na kuanza kupuuza baadhi ya mambo. Hapo ndipo utakuta wengi wanasema siendi kanisani maana yanayofanyika ni yale yale kila siku.

Hali kama hizi huwa zinatukumbuka sana wengi waliopata neema ya kupata maarifa ya Mungu, ni sawa na mtu aliyesoma sana akafika kiwango fulani cha elimu ya darasani. Mara nyingi sana huwa anafika hatua anaona mtu asiye na elimu hawezi kumshauri jambo, huwa anaona mtu asiye na elimu hawezi kufanya mambo makubwa ya kiMungu.

Dhana hii imewapotosha watu wengi sana kufikiri wakishafikia kiwango fulani kumfahamu Mungu, ndio hawahitaji tena kuendelea kujifunza Neno la Mungu. Wamesahau kujifunza kwa Neno la Mungu kunakufanya uendelee kumwona Mungu kwa kiwango kingine zaidi.

Neno la Mungu ni chakula chako cha kiroho, hakuna siku ukafika hatua ukasema huna haja tena kula chakula cha KIROHO. Nakwambia maarifa ya Mungu huwa hayashibishi mtu siku moja, alafu akawa hahitaji tena kujifunza mambo mengine zaidi.

Usifikiri umemjua Mungu hapo ulipo ukajiona imetosha huna haja tena ya kuendelea kujifunza Neno la Mungu, ukijiona huna haja tena ya kuendelea kuhudhuria mafundisho ya Neno la Mungu, ukijiona wewe ni kiwango cha juu sana kuliko wengine. Unapojiona huna haja tena ya kuendelea kujifunza Neno la Mungu kwa kujiona wewe umesoma sana chuo cha biblia, umeshajitengenezea mazingira ya kupotea.

Ndio maana kuna wakati watu walipata shida na akina Petro na Yohana, kwa jinsi walivyokuwa wamejaa ujasiri na uweza wa Mungu. Walifikiri elimu ndio inamfanya mtu awe vile wanafikiri wao.

Rejea; Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. Matendo 4:13 SUV.

Usifikiri umemjua sana Mungu huna haja tena ya kumjua zaidi, huenda hapo unavyojiona umemjua sana. Ndio hatua ya kwanza kabisa ya mtu anayetoka kwenye uchanga wa kiroho, huenda hapo ulivyofikia na kujiona huhitaji tena kujua zaidi ndio ulipaswa kujua zaidi.

Dharau kwa mtu wa Mungu kwa kufikiri anamwelewa sana Mungu, ni kujidanganya mwenyewe. Hali hiyo inaweza kumwondoa kabisa kwenye mstari mzuri wa kiMungu. Maana Mungu anawapenda wale wanyenyekevu wanaolitii Neno lake.

Usijione umefika, elimu yako ya darasani isikudanganye kabisa, kuimba kwako vizuri kusikudanganye kabisa, kuhubiri kwako vizuri kusikudanganye kabisa, kusoma kwako historia za kale kuhusu mitume na manabii mbalimbali kusikudanganye kabisa. Mungu kusema na wewe mara kwa mara kupitia ndoto/maono au sauti yake, kusikufanye ukajaa kiburi na dharau kujiona umefika hatua za juu sana.

Rejea; Wayahudi wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma? Yohana 7:15 SUV.

Ikiwa dharau na kiburi chako kimetokana na elimu/maarifa ya dunia hii, nikuombe utubu haraka sana kama unapenda maisha ya umilele pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo.

Nyenyekea chini ya mkono wa Bwana, jifunze kutoka kwake, penda kujua kilicho ndani ya Neno la Mungu. Tamani kusikia kiu zaidi kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu, hata kama Mungu anakutumia sana kwa viwango vya juu kwenye huduma aliyokupa ndani yako. Usifike hatua ukaanza kuonyesha dharau kwa wengine, hata hao wanahitaji msaada, wanahitaji neema ya Mungu iwe juu yao, hii neema ya wokovu ni yetu sote wanadamu.

Acha dharau, hujafikia kiwango cha kumjua Mungu sana mpaka ukawa na kiburi kiasi hicho, acha kutolea wenzako maneno ya kejeli na dharau. Wasaidie waweze kutoka huko, wasikie, wasikie wewe utakuwa umenawa mikono yako.

Ukiweza kujibu maswali haya endelea na dharau zako za kujiona unamwelewa sana Mungu, ikiwa huwezi kujibu nikuombe utubu mbele za Mungu.

Rejea;Je! Umeziingia chemchemi za bahari, Au umetembea mahali pa siri pa vilindi?

Je! Umefunuliwa malango ya mauti, Au umeyaona malango ya kuzimu?

Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema, ikiwa unayajua hayo yote.

Iko wapi njia ya kuyafikia makao ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi?

AYU. 38:16‭-‬19 SUV.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutafakari kwa kina hayo maandiko Matakatifu. Kuna jambo kubwa utaondoka nalo hapo.

Imeandaliwa na kuletwa kwako na Samson Ernest.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.