Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, kama umepata kibali cha kuiona siku ya leo, mshukuru sana Mungu kwa fursa hii adimu. Jitahidi siku ya leo isipite bila kufanya kitu chenye alama mbele za Mungu, kiwe akiba kwako.

Karibu sana baba, mama, kaka, na dada tujifunze kwanini hatuwezi kupongezwa kwa juhudi zetu za kila siku. Na wakati tunafanya vizuri mambo yanayompendeza Mungu wetu.

Unaweza kuzoea kupongezwa na kupewa sifa nyingi sana kwa kile unachofanya kila siku, na kweli unaweza kuona moyoni mwako unachofanya na unachopongezwa unastahili kabisa kupongezi hizo. Moyoni mwako utaona kabisa unastahili kutiwa moyo kwa kile unachofanya kila siku.

Unaweza kuzoea mazingira haya ya kupongezwa kila siku na kutiwa moyo, na watu wako wa karibu, au na wale wanakufuatilia, au wale wanaokuzunguka mtaani/ofisini kwako, au wale ndugu zako mnaoishi nao kila siku, au mke/mume wako mnayekaa naye, au mchumba wako anayejua huwa unafanya nini.

Usitegemee hizo sifa au pongezi zitaendelea kila siku, unapaswa kuelewa hili usije ukarudi nyuma kwa safari yako uliyoanzisha. Kama kiu yako ya kufanya jambo fulani inatokana na kupongezwa na Makundi niliyokutajia hapo juu. Ujue upo hatiani kuishia njiani kwa kile ulichokianza kukifanya.

Kupongezwa kunatia moyo na kuonyesha kile unachofanya kinawasaidia wengine, inatia moyo wa kuendelea kufanya vizuri zaidi ya mwanzo. Lakini unapofanya jambo/kitu kikaonekana hakuna anayejali wala hakuna anayesaidika na hicho unachofanya, mara nyingi huwa inavunja moyo na inahitaji uwe na wito kutoka ndani kuendelea kufanya hilo/hicho unachoona kina msaada kwako na kwa kizazi kijacho na kile kitakachopita mikononi mwako kujifunza.

Pamoja na kupenda kupongezwa na kutiwa moyo kwa yale unayofanya, kuna wakati utafika wale wale waliokupongeza kuwa unachofanya ni kizuri na kinamletea Mungu utukufu. Ndio haohao kesho wanaweza kukuambia achana na hicho unachofanya, ndio hao hao watakaokuambia umekosa cha kufanya, kila siku unafanya kile kile.

Walewale ndio watakaokuambia huna kazi ya kufanya ndio maana unapata muda wa kufanya hayo ambayo wao hawafanyi. Ukiangalia muda wanaousema unao wewe, unaona wao wanao mwingi zaidi yako wewe.

Yapo maeneo mengi katika maisha yako ambayo unaweza kukutana na changamoto hii, ila leo nizungumze upande wa kusoma Neno la Mungu. Hili jambo kwa wengi bado linaonekana halina ulazima sana, hata unapomwambia mpendwa mwenzako umhimu wa kusoma Neno la Mungu anakuona sijui vipi.

Ni jambo fulani linalomwingia mkristo kwa taratibu sana, ndio maana wengi wameanza kwa hamasa kubwa sana. Baada ya muda fulani waliacha na ukimuuliza vipi ndugu, atakupa sababu ambazo unaona kabisa huyu alikuwa hajadhamiria kutoka ndani ya moyo wake kufanya.

Sasa unapoonekana unaweka nidhamu katika hili, unaweza kuanza kupongezwa sana na wale wanaokuona unafanya hilo jambo lililowashinda wao. Pia unaweza kuanza kwa kuambiwa hutoweza kufika mbali utakuwa umeachana na hilo zoezi la kusoma Neno la Mungu.

Wale wa kwanza waliokupongeza kuwa unachofanya ni kizuri, ndio wale wale wanaweza kutumika kama jeraha kwako kwa kukuambia maneno ya kukuvunja moyo. Kama upo nyumbani kwa wazazi/walezi wako unaweza kuambiwa maneno magumu ambayo yakatufedheishe na kukuondoa kwenye mpango wako wa kusoma Neno la Mungu.

Unaweza kuwa umejiwekea ratiba yako baada ya kumaliza shughuli zako fulani, utakuwa na muda wa kusoma Neno la Mungu. Unafika huo muda ukakutana na kikwazo ambacho unapaswa kuchukua maamzi ya kukiacha kwanza ili ufanye kile ulipanga kufanya.

Kupitia usomaji wako wa Neno la Mungu, hakutakuacha uendelee kubaki vile vile ulivyokuwa mwanzo. Kadri unavyozidi kukua kiroho ndivyo na ishi yako na tabia/mienendo yako inazidi kubadilika, kubadilika kwako kunaweza kutumika kama silaha ya kukupigia kwa kuanza kutupiwa maneno mabaya juu ya usomaji wako wa Neno la Mungu.

Unapojikuta katika hali kama hizi, usivunjike moyo, hata kama mume/ mke wako alikuwa anakupongeza kwa juhudi zako za kusoma Neno la Mungu. Alafu ikatokea akaanza kukuambia maneno magumu ya kukufedhehesha moyo wako, usije ukaacha bidii yako ya kujifunza Neno la Mungu.

Chakula chako cha kiroho ni Neno la Mungu, ukiacha kusoma hali yako ya kiroho itasinyaa kwa kupungukiwa na jambo muhimu moyoni mwako. Acha maneno ya kukuvunja moyo yatokee, wewe jiwekee ukuta ambao hutovunjwa na mtu yeyote isipokuwa Mungu mwenyewe.

Kila njia itakayotumika kukupiga ili utoke nje ya mpango wako wa kusoma Neno la Mungu, usikubali maumivu yale yakuondoe kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu. Usifikiri shetani anafurahia sana unavyozidi kumjua Mungu wako, anaelewa kadri Neno la Mungu linavyozidi kukaa kwa wingi moyoni mwako ndivyo unavyozidi kujitenga na mazingira ya dhambi.

Tazama sana kumpendeza Mungu wako, mwanadamu anabadilika muda wowote, atakapobadilika akuache unaendelea na utaratibu wako. Na atakapojirudi tena akutane na mpango wako ule ule unaendelea nao, tena awamu hiyo akukute umepanda viwango zaidi.

Bila shaka kuna kitu umekipata cha kukusaidia katika usomaji wako wa Neno la Mungu, kitumie hicho ulichokipata kikusaidie kuwa imara katika usomaji wako wa Maandiko Matakatifu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma makala hii. Kupata masomo mengine mazuri zaidi endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu.

Imeandaliwa na Samson Ernest.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.