Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa kwetu sote. Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona siku ya leo, tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu sisi sote tuliopata fursa hii adimu. Maana wengi waliitamani sana leo, lakini hawakuweza kuifikia, tuna kila sababu ya kufanya vitu vinavyomletea Mungu utukufu.

Kabla ya yote, napenda kumshukuru Mungu kuwa pamoja nasi kwa timu nzima ya CHAPEO YA WOKOVU wasap GROUP. Tulikuwa na safari ya kusoma kitabu cha Ayubu chenye sura 42, na leo tunaenda kuhitimisha safari yetu katika sura ya 42. Nikiwa na maana kwamba tulianza sura ya 1 hadi leo tupo sura hii ya 42.

Haikuwa kazi rahisi kama ninavyoweza kukuandikia hapa, ilihitajika nidhamu ya mtu binafsi ya kuweza kutenga muda wake kila siku kupitia sura moja hatua kwa hatua mpaka leo tumefikia sura ya mwisho kabisa katika kitabu cha Ayubu. Kumaliza kitabu cha Ayubu ni maandalizi ya kuanza kitabu kingine, ambacho nacho tutaenda nacho hatua kwa hatua mpaka mwisho.

Niwapongeze wote waliamua kutenga muda wao kwa namna yeyote ile, ili wapate wakati wa kusoma Neno la Mungu na kufakari yale waliyojifunza katika sura husika. Zoezi hili limekuwa baraka kwa wengi sana waliodhamiria kutoka ndani mioyo yao.

Usione ni jambo fulani kubwa sana na gumu sana kwa wewe ambaye bado hujachukua hatua ya kujisomea Neno la Mungu. Ukidhamiria kuanzia sasa utaweza, haijalishi changamoto utakazokutana nazo, ukiwa na nia ya kweli hakuna kitakachokuzuia kufikia malengo yako.

Baada ya kusema hayo, nikurudishe katika kichwa cha somo letu kinachosema;Nipigie Simu Baadaye Kwa Sasa Nasoma Neno La Mungu.

Tumejikuta tunaelewa haraka sana mtu anapokuambia nipigie baadaye nipo kwenye kikao, mtu yule anakuelewa na hawezi kupata shida anajua utatoka na mtawasiliana.

Wakati mwingine hupokei simu yake au unaikata simu na kumwandikia ujumbe mfupi nipo kwenye kikao, nitakutafuta baadaye. Mwingine unampigia simu anakwambia nitafute baadaye kwa sasa nipo kazini, mwingine unampigia hapokei simu na akija kupokea anakwambia nilikuwa na kazi nafanya, mwingine unampigia unaambiwa hapatikani na akija kupatikana anakwambia alikuwa sehemu ambayo asingeweza kuwasha simu yake.

Ikiwa maeneo yote hayo tumefaulu, tunashindwaje kutoa milio yetu ya simu wakati wa kusoma Neno la Mungu, tunashindwaje kupokea simu na kumwambia aliyekupigia niache kwa sasa nina shughuli nafanya, kumbe shughuli yenyewe ni kusoma Neno la Mungu. Tunashindwaje kuzuia kelele zingine au kukaa nazo mbali ili tupate uhuru wa kusikia kile Mungu anasema nasi kupitia Neno lake.

Mambo mengine tumefaulu kwa kiwango fulani, wengine wamefikia kiwango cha juu zaidi, ukitaka kumwingizia ratiba yako anakwambia kwa sasa nina kazi natakiwa kufanya baada ya dakika tano zijazo kwa hiyo nitafute baadaye. Kwa umakini huo huo ambao tumeanza kuufikia na kuthamini muda wetu, tufike hatua tuanze na kuzuia watu wasiingilie muda wetu tuliojipangia kusoma Neno la Mungu.

Utaona baraka kubwa sana kwa hili, usiogope kumweleza aliyekupigia simu kuwa unasoma Neno la Mungu akupigie baadaye. Tena utakuwa umemhubiria bila yeye kujijua yaani kama ni mkristo mwenzako na alikuwa hana ratiba hiyo katika maisha yake, ataanza kujisikia vibaya moyoni. Baada ya muda fulani utaona na yeye anaanza kuwa na tabia hiyo ya kutenga muda wake wa kusoma Neno la Mungu.

Ukiona haina muhimu sana kupokea simu hiyo, vyema ukaikata na kuiondoa mlio kabisa mpaka pale utakapomaliza kusoma na kufakari Neno la Mungu. Ukifikia hatua ya kuanza kuzuia kelele zingine zisiingilie ratiba yako ya kusoma Neno la Mungu, nakwambia utakuwa umejenga msimamo mzuri na wa kuigwa na wengine.

Tabia yeyote njema au mbaya haitokei tu kwa miujiza, kuna hatua mtu anapitia ndipo anaitengeneza tabia aliyonayo sasa. Ukiamua kutengeneza tabia ya kusoma Neno la Mungu itawezekana, bila kusukumwa na mtu yeyote utajikuta unajisukuma mwenyewe. Mwanzoni unaweza kupata shida kwa hili, ila kadri unavyozidi kuweka bidii yako utafika wakati unakuwa vizuri.

Fika hatua watoto wako wajue baba/mama anasoma Neno la Mungu hapaswi kusumbuliwa, fika hatua mume/mke wako ajue huyu Mr/Mrs muda wake umefika wa kusoma Neno la Mungu, fika hatua marafiki zako wajue muda wako umefika wa kujitenga na wao, fika hatua unaoishi nao wajue ikifika muda fulani hupaswi kusumbuliwa. Watakudharau mwanzoni, watakusema vibaya na watakupa kila jina, ila utafika wakati watakuheshimu na kukumbusha kabisa wakati mwingine pale wasipokuona umeshika biblia yako.

Bila shaka lipo jambo umejifunza kupitia ujumbe huu, hilo ulilojifunza vyema ukalifanyia kazi kuanzia hapo ulipo. Utaona matokeo mazuri sana kwa kutoa muda wako kuhakikisha mambo mengine hayauingilii.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, kwa masomo mengine mazuri zaidi usiache kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu.

Imeandaliwa na Samson Ernest.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.