Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, hatuna cha kumlipa kwa hichi anachofanya kwetu ila tunayo nafasi ya kumzalia matunda yaliyo mema.

Wengi tumeshindwa kujitofautisha kipi huwa kinatukwamisha katika usomaji wetu wa Neno la Mungu, badala yake tumejikuta tunachanganya vitu na kushindwa kuijua sababu hasa inayotufanya tubaki vile vile kila siku, ni ipi.

Ukitaka kukomesha tabia inayokusumbua kila siku usifikie lengo lako, unapaswa kuangalia chanzo kikuu kinachokupelekea urudie kosa lile lile kila siku. Utakapojua chanzo cha tatizo lako, ni rahisi kurekebisha ama kung’oa kabisa shina na mizizi yake, ili usiendelee kukwamishwa na hilo.

Unakuta mtu anasingizia huwa anashindwa kusoma Neno la Mungu, kwa sababu hana muda. Wakati huo huo anakwambia hana muda, unamkuta kwenye nyumba za majirani/marafiki zake anapiga stori, mwingine unamkuta kwenye magroup ya wasap anachati na kujibu kila SMS.

Mwingine anakwambia nitakuwa kwenye maombi, sitaweza kusoma Neno la Mungu kwa siku kadhaa. Kwa hiyo maombi huwa yanamkataza mtu kusoma Neno la Mungu au kuwa kwenye maombi imeandikwa usiguse Neno la Mungu? Kuna vitu tunafanya ila hatuelewi tunachofanya kina faida gani na hasara gani.

Mwingine anakwambia nitakuwa kwenye huduma ya kuhubiri sitakuwa na muda wa kusoma Neno la Mungu, kwani hiyo huduma unaenda kutolea nje au ndani ya Neno la Mungu. Kama ni ndani ya Neno la Mungu, hiyo sio kusoma Neno la Mungu au ukishaandaa somo lako huruhusiwi tena kupitia Maandiko Matakatifu.

Mwingine anakwambia kwa sasa nitakuwa chuo/shule sitakuwa na muda wa kusoma Neno la Mungu, wakati huo ana muda kusoma vitabu vyake vingine, wakati huo ana muda wa kuingia facebook, instagram, whatsApp, LinkedIn na YouTube. Ila kwenye Neno la Mungu yupo bize, hana kabisa muda kushika biblia yake.

Sijui Neno la Mungu ndio sumu ya kuharibu masomo yake, sijui Neno la Mungu ndio chanzo cha yeye kufeli masomo yake, sijui neno la Mungu ndio chanzo cha kuharibu huduma/mahubiri/mafundisho yake. Ipo picha mbaya imejengwa kwenye fahamu zetu, hiyo picha inatutafuna chini kwa chini bila wenyewe kujielewa.

Tunateswa na uchanga wa kiroho pasipo wenyewe kujua kabisa kama huo ni uchanga wa kiroho, kuna vitu tunafanya mpaka Mungu anatushangaa. Ukiamua kutoka ndani ya moyo wako, mazingira machache sana yatakuzuia kutokusoma Neno la Mungu, na ukijiweka vizuri yanaweza yasiweze kukubana ushindwe kupata muda na Mungu wako.

Unachopaswa kujiuliza ni hichi;Upi Unaona Ni Usumbufu Kwako, Kusoma Biblia Au Kubeba Biblia? Chukua kalamu na daftari lako;ikiwa ni kusoma biblia unapaswa kuorodhesha sababu zote kwenye karatasi lako. Alafu anza kupitia moja moja kwa kuhoji hivi, je wewe unaweza kunibana nisipate hata nusu saa ya kusoma Neno la Mungu?

Usionee aibu kuandika alafu kuanza kulihoji karatasi na yale uliyoyaandika, hoji hoji kila sababu uliyoandika. Ambayo hiyo sababu huwa inakukwamisha wewe usisome biblia yako, ukishamaliza. Jiulize ukimpa Mungu muda wako huwa unaona unapungukiwa na nini katika siku yako nzima.

Ukishamaliza hapo, njoo kwenye kwenye kubeba biblia, ikiwa changamoto kwako ni kubeba biblia yako. Orodhesha sababu zote ambazo unaona ni kikwazo kwako, fanya kama ulivyofanya kwenye sababu za kusoma Neno. Hizo sababu anza kuandika kwa mbele yake, kwa kujihoji hivi, je wewe ndio unanifanya nimwonee aibu Mungu wangu anayenifanya niishi?

Hili zoezi sio la utani, nataka uondoke na picha kamili ya hayo unayofanya na kuona ni sahihi kwako kutokusoma Neno la Mungu. Pasipo kujitathimini kwa kutafakari zile sababu ambazo huwa tunajipa na kujiona tupo sawa, vizuri tukajenga utaratibu wa kujiweka pamoja sisi wenyewe kujipa semina ambayo inaweza kuchukua lisaa limoja ukatoka umejifunza mengi.

Nimejifunza kwa wanawake wawili ambao wapo Chapeo Ya Wokovu wasap GROUP, wakati wa ujauzito mpaka kujifungua walikuwa wanasoma Neno la Mungu. Nikashindwa kuelewa hawa walipata wapi ujasiri wa kuhimili hili jambo na kutoa muda wao, mwingine akanimbia mtumishi niombee nipone haraka kidonda cha operation. Alafu wakati wa kusoma Neno la Mungu unamwona hewani, hapo ndipo unapojua huyu mtu amejua nini maana ya Neno la Mungu.

Siwezi kukufariji umebanwa sana, siwezi kukufariji mazingira ulipo hayakuruhusu kuwa na biblia wakati smartphone/tablet yako ina App ya Biblia. Ukiamua kutoka ndani ya moyo wako, utaona mwelekeo wa maisha yako ukienda vizuri tu. Kusoma Neno la Mungu hakupunguzi chochote kwenye shughuli zako, zaidi Neno la Mungu linakupa upeo zaidi wa namna ya kukabiliana na dhambi na changamoto mbalimbali.

Bado una sababu inayokuzuia usisome Neno la Mungu? Tuwasiliane kwa email nitakayotoa hapo mwisho au tuwasiliane wasap au nipigie simu kwa namba hizo hapo chini. Au waweza kutoa maoni yako hapo chini baada ya kumaliza kusoma ujumbe huu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu, kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Imeandaliwa na Samson Ernest.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.