Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine tena cha kuweza kuifikia leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Siku zote usipojua matumizi ya kitu unaweza kuanza kutafuta msaada kwa wengine ili wakusaidie, wakati ulikuwa una uwezo wa kujisaidia mwenyewe. Kweli upo wakati utahitaji msaada wa watu, ila sio wakati wote unahitaji watu wakubebe katika jambo fulani.

Yapo mambo huwezi kumsaidia mtoto wako, hata kama ni mchanga sana, huna uwezo wa kumsaidia mpaka yeye afanye. Mfano kunyonya, wewe kazi yako inaweza kuwa kumlazimisha kwa nguvu anyonye, ila kazi ya kumeza itabaki kwake. Maana unaweza kumlazimisha na akatema kile kiasi cha maziwa uliyompa, bado itarudi kuwa baadhi ya vitu unafanya kwa sehemu yako na mengine hutoweza kufanya.

Mtoto huwezi kumsaidia kutoa haja ndogo wala kubwa, ni yeye mwenyewe anafanya hivyo ndipo wewe unaweza kumsafisha. Hata kama unampenda sana, asipoweza kujisaidia utaanza kupata mashaka. Hii ni kwa sababu unajua chakula unachompa lazima kitafanya kazi na baada ya muda utategemea mtoto ajisaidie.

Tunaweza kuwalaumu watumishi wameshindwa kutusaidia shida zetu, tumesahau sisi tulikuwa na uwezo wa kujisaidia. Inahitaji neema mtu kujua ugonjwa unaosumbuliwa nao kama wewe mwenyewe unashindwa kujitambua unaumwa nini, itakuwa kwa asiyeumwa?

Wakati mwingine tumepewa funguo za chumba cha dawa, na maelekezo yake namna ya kuzitumia. Ila umebaki kuzikumbatia na kuanza kutafuta msaada wa nje kwa watu wengine, wakati tulikuwa na uwezo wa kusimama kama wenyewe na Mungu wetu tukavuka eneo ambalo tulikuwa tunapata changamoto.

Tunaweza kuwa waombaji wazuri sana, kama omba yetu haina mizizi ya Neno la Mungu tutafika wakati tutachoka na tunayoomba tutaona mbona hatuyaoni kwa kujibiwa. Badala yake tutatoka nje ya mstari wa Mungu na kwenda kutafuta msaada wa nje wakati huo tumezikumbatia funguo za majibu yetu.

Neno la Mungu limebeba funguo za milango yote ya maisha yako kiroho na kimwili, shida ni kwamba unakosa ujasiri wa kukabiliana na mambo magumu kwa sababu umeziacha funguo mfukoni. Huku umeendelea kutafuta msaada wa nje.

Kweli kabisa kuna milango unaona imefungwa, ila funguo umepewa za kuweza kufungua hiyo milango, imefungwa kwa sababu ina vitu vya thamani ndani yake. Haiwezi kuachwa wazi kienyeji, hata nyumba yako huwezi kutoka ukaacha mlango wazi alafu ukaenda safari ya mbali. Utakuta chumba kitupu.

Funguo ni Neno la Mungu, unafika kipindi unaacha wokovu kwa sababu ulishindwa kutumia funguo ulizopewa. Unapoambiwa kuwa na muda wa kusoma Neno la Mungu, usifikiri ni hadithi tu, ni kweli Neno la Mungu linaweza kukuvusha sehemu ambayo kila mtu aliona ndio mwisho wako kupotea.

Hizi funguo zitakaa ndani ya moyo wako, kadri unavyozidi kulijua Neno la Mungu ndivyo na mageti yenye makufuli makubwa yanazidi kupata funguo zake. Kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu unazidi kuona sio shida tena kuliona geti limefungwa, utajua ukitaka kuingia utaingia kirahisi kwa sababu unazo funguo za kuingilia.

Huwezi kutishwa na geti la nyumba yako mwenyewe kama una funguo zake, isipokuwa utatishwa na geti lako na kuhangaishwa akili ikiwa utakuwa umepoteza funguo zake. Hapo ndipo utaanza kutafuta watu wakusaidie kuvunja, hapo ndipo utaanza kutafuta mafundi wa kuweza kukuvunjia kitasa.

Sikukatazi kuomba wala sikukatazi kuombewa, ila ni muhimu sana ukajua unayo mamlaka itokanayo na Neno la Mungu. Ukiwa na Neno la Mungu moyoni mwako, ni rahisi sana kwenda mbele za Mungu kwa ujasiri, ni rahisi sana kupata maombi ukapokea uponyaji kwa kujua hili Mungu ameniahidi kupitia Neno lake.

Wengi imani zetu zimekuwa hafifu kutokana na kukosa ufunguo umhimu ambao ni Neno la Mungu, uwe na uhakika ukiwa na Neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako. Ni rahisi sana kukabiliana na mambo magumu ambayo kwa akili za kibinadamu yanaonekana hayawezekani.

Kupata funguo hii muhimu kwako ni kusoma Neno la Mungu kwa nguvu zako zote, hakikisha unakuwa na muda wa kulisha moyo wako Neno la Mungu. Utaona matokeo makubwa na mazuri sana katika maisha yako ya wokovu, utamwona Mungu sio mkatili kama unavyofikiri sasa.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu. Kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kujifunza Neno la Mungu na kuweka bidii zaidi.

Imeandaliwa na Samson Ernest.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.