Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, kama ni muujiza basi hata kuifikia siku ya leo ni muujiza. Huu ni muujiza wa pekee sana Mungu kutoa kibali kwako uendelee kuwa hai, huhitaji kuhangaika kutafuta Mungu amekutendea nini. Kuamshwa ukiwa mzima ni jambo la kumshukuru Mungu, hata kama unajisikia vibaya na kuumwa, amini kwamba umepata nafasi adimu miongoni mwa watu waliochaguliwa kuifikia leo.

Mungu hajawahi kumwacha mtoto wake anayemtumikia kwenye eneo lolote lile chini ya jua, unaweza kufikiri hakuna anayejua mchango wako. Na unaweza kufikiri unachofanya unakifanya tu kwa sababu unasikia msukumo ndani yako kufanya, na unaweza kufikiri unachofanya unafanya tu kwa kusukumwa ufanye.

Unaweza kufanya kwa bidii sana, siku za mwanzo ukapata hongera nyingi na ukajisikia hamasa zaidi ya kufanya. Ila ikafika hatua ukaanza kukutana na changamoto ngumu zinazokufanya urudi nyuma kwa kile ulichokianza kukifanya. Vile vile unaweza kuanza kwa shida na kila anayekutazama anakuvunja moyo, ila ikafikia hatua hata wale waliokuambia haiwezekani wakaja kukuomba ushauri umewezaje kufikia hapo.

Mungu anakuona unachofanya ndio maana anazidi kuweka mzigo ndani yako ili usijikie kukata tamaa na kuacha kabisa. Ndio maana utakutana na mtu anakwambia, kuna kipindi nilifika hatua nikavunjike moyo ila nikajisikia kusonga mbele, au kuna siku nilifika hatua nikaona kila kitu kimefika mwisho ila nikakutana na mafundisho ya Neno la Mungu nikajisikia kuinuka tena.

Mungu hawezi kukuacha peke yako, kuna nyakati unaweza kufikiri unachofanya hakioni na unaweza kufikiri unapambana tu peke yako pasipo msaada wowote kutoka kwake. Maana unaweza kumwomba akuondolee maadui wanaokusonga, badala ya kuondoka ndio kwanza unaona wanaongeza makwazo zaidi juu yako.

Kwa akili za kibinadamu unapotazama matokeo ya nje unaona Mungu hukusikii maombi yako, unaona Mungu hakujibu mahitaji yako. Na unaweza kufika hatua ukaanza kufikiri labda kuna dhambi umeitenda, tena kwa kukazia hilo la kumkosea yeye anakuja mtu anakwambia kwa jinsi ulivyo utakuwa umemtenda Mungu dhambi ndio maana hakujibu mahitaji yako.

Usipokuwa imara mbele za Mungu, utajikuta unaanza kuhangaika kuitafuta dhambi hiyo. Tena shetani alivyomjanja atakuletea mazingira fulani hivi ujione kweli utakuwa labda umekosea sehemu, ukijaribu kutubu na kutubu unaona mambo bado yale yale. Tena wakati mwingine unaweza kuona badala ya changamoto kupungua zinazidi kuongezeka.

Tunapofika hali kama hizo, wengi wetu huwa tunaona bora tuachane na kile tulichokuwa tunafanya kumletea Mungu utukufu. Tukifikiri tutakuwa huru na kuepuka lawama za watu na kuonekana sisi ni wabaya, badala yake wale wale uliofikiri utawadhirisha wanaanza kusema tulisema hutofika mbali. Badala ya kujisikia furaha na amani kwa kuacha ulichokuwa unafanya, unaanza kujisikia huzuni kwanini uliacha.

Leo ninao ujumbe mwema kwako, usifikiri unavyosoma Neno la Mungu unapoteza muda wako na usifikiri hakuna unachokipata kupitia usomaji wako wa Neno la Mungu. Zipo hatua kubwa sana za kiroho unasogea pasipo wewe kuona matokeo yake haraka, umefichwa usione hayo kwa makusudi maalum kabisa ambayo Mungu anajua juu yako.

Neno la Mungu linamkuza mtu kiroho na kumwondoa sehemu moja na kumpeleka sehemu nyingine siku hadi siku, hata kama mtu mwenyewe haoni hilo. Uzuri Mungu anatujua kuliko sisi wenyewe, anajua namna ya kukuza hatua kwa hatua, ila kama huwa una tabia ya kujitathimini maisha yako. Lazima utaona mabadiliko fulani kwenye maisha yako, ukijitazama ulivyokuwa mwanzo na ulivyo hapo ulipofikia utaona baadhi ya vitu vilivyoongezeka kwako na vingine visivyofaa kuondoka kabisa.

Pamoja na kujitathimini na kujiona umevuka baadhi ya maeneo bado kibinadamu unaweza usiridhike na unaweza kuletewa picha fulani mbele yako. Ambayo hiyo picha itakuwa inakufanya uone unachofanya hakina matokeo makubwa sana, unapoona hivyo unafika hatua unaona bora uache kusoma Neno la Mungu.

Ukiwa jasiri na ukatambua kile unafanya, upo wakati Mungu atafungua ufahamu wako uone mazingira wanayopitia wenzako ambao wamebaki kujivunia udini/udhehebu. Ila ndani yao hawana Neno la Mungu, utaona ilivyo mbaya mtu kuwa mchanga wa kiroho, utaona ilivyo mbaya mtu kujivunia mkristo lakini kuna vitu vingi sana anavifanya vya kitoto.

Ninapokuambia SOMA NENO UKUE KIROHOusifikiri nakutania, ni kweli kabisa Neno la Mungu linakukuza kiroho. Na uzuri wa kukua kiroho kunakupelekea kukua kimwili pia, maana yake yale matokeo mazuri ya ndani ya mwamini ndio yanayozalisha matunda mema kwa mwonekano wa nje.

Huenda unajiuliza utatiwaje moyo kwa usomaji wako wa Neno la Mungu, hata hapa wakati unaendelea kujiuliza itakuwaje. Yupo mtu mmoja ametiwa moyo kupitia ujumbe huu unaosoma wewe hapa. Muhimu kwako ni kujua usomaji wako wa Neno la Mungu ni wa maana sana, hukufanyi tu uwe wa rohoni sana, unakufanya uwe wa tofauti na aliye mchanga wa kiroho.

Shida ya uchanga wa kiroho huwezi kuiona moja kwa moja kila eneo la maisha yako, ni mpaka pale utakapotoka hapo kwenye uchanga. Mnaweza kuwa mnajifariji na rafiki yako mpo vizuri, ila mmoja wapo akiamua kuweka bidii katika kulisoma Neno la Mungu na kulitafakari kila siku. Baada ya Muda atakuona wewe rafiki yake ni mchanga wa kiroho na una mambo fulani ambayo sio mfano wa kuigwa kama mtu aliyeokoka.

Bila shaka kuna kitu kizuri umekipata kupitia ujumbe huu, hebu kifanyie kazi na endelea kuweka bidii yako katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Yapo matunda mengi sana katika hili jambo la usomaji wa maandiko Matakatifu, huenda kwa sasa unaona hakuna chochote, nakwambia kuna siku utalia machozi ya furaha pale Mungu atakapofungua ufahamu/akili zako uone ulipokuwa zamani.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu. Kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kukua katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Imeandaliwa na Samson Ernest.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Website: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081