Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa matendo yake makuu kwetu.

Huwa tuna madai mengi sana katika maisha yetu, hasa hasa tukifika kwenye mambo ya msingi tunaanza kusingizia vitu vingine ambavyo havipo kabisa. Wakati tunafikiri upo wakati mwingine mzuri zaidi wa kuweka bidii katika mambo ya Mungu, tunajikuta hatufanyi bidii zozote kwa muda tulionao sasa.

Hata huo muda tunaofikiri ukifika tutafanya mengi mazuri, cha ajabu huo muda uliofikiri ni mzuri sana kwako kufanya mambo ya Mungu. Unafika ila unajikuta unakutana na changamoto zilezile zilizokukwamisha na wakati mwingine zinaongezeka zaidi ya mwanzo.

Kujidanganya ni rahisi sana, uvivu wa mtu huwezi kumfikisha viwango vya kiMungu ambavyo ukiwa kama mkristo unapaswa kuwa navyo. Ukristo wa kuunga unga ni mbaya sana, ule ukristo wa kulipuka kwa matukio na kuzima, ule ukristo wa kuhitaji msaada wa Mungu baada ya hapo unapotea kabisa. Hupaswi kuwa nao kabisa ukiwa kama mtu mwenye safari ya kwenda mbinguni.

Hebu fikiri lini umewahi kufikia hiyo siku uliyofikiri utapata muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu, bora ungesema muda niliokosa ni ule wa kushiriki Neno la Mungu na wenzangu tuliokubaliana kusoma biblia pamoja. Wewe kama wewe hata usipopata huo muda wa kusoma Neno la Mungu na kutafakari pamoja na wenzako, huwezi kujipa nusu saa ukapitia maandiko Matakatifu katika ule mpango wa kusoma sura hadi sura?

Haya mwingine alisema kwa sasa shule imenibana siwezi kupata muda wa kusoma Neno la Mungu, anamaliza hiyo shule. Lakini cha ajabu ndio anapotea zaidi, kipi ni bora kusubiri wakati fulani ndio uanze kumpa Mungu muda au mwenye muda ndio unapaswa kumpa muda wake?

Haya mwingine anakuambia kwa sasa nimebanwa sana na shughuli, sina kabisa muda wa kushika biblia nikasoma. Wakati huo smartphone/tablet yake ina App ya Biblia, kwa hiyo anamwambia Mungu hii kazi niliyokuwa nayo imechukua muda wako hata kusoma Neno lako siwezi. Kama ni hivyo mbona anapata muda wa kuchati kwenye mitandao ya kijamii, mbona anapata muda wa kulala, mbona anapata muda wa kula.

Haya wakati anadai kazi zilikuwa zinambana sana, sasa hiyo kazi hana yupo tu nyumbani, mbona bado hapati muda wa kusoma Neno la Mungu? Kipi kilikuwa kinamkwamisha, ni kazi au ni uvivu au ni kufikiri akifika muda fulani ndio atakuwa huru sana?

Nasikitika kukuambia wewe ambaye unafikiri upo wakati utakuwa huru sana, ambao huo uhuru utakufanya umpe Mungu muda wake aliokupa. Maisha haya yataendelea kubanana hivi hivi, hiyo changamoto unayoona imekubana leo mpaka kushindwa kumpa Mungu muda wa kusoma Neno lake. Kesho unaweza kuamka na changamoto nyingine mpya kabisa na bora zaidi ya ile ya jana, kwa hiyo unaweza kujikuta unamaliza miaka unafikiri upo wakati mwingine mzuri zaidi wa huo ulionao sasa.

Acha kujidanganya ndugu yangu, muda ulionao sasa ni wa thamani sana kwako, hiyo kesho unayoifikiria wewe hujui itaamka na nini. Inaweza kuamka na kipya zaidi ya kile unaona wewe kimekuwa kikwazo kwako, huenda hiyo changamoto inayokusumbua leo isingeonekana mzigo mzito kwako kama ungekuwa na Neno la Mungu moyoni mwako.

Usiifanye shida yako ndio kipaumbele chako cha kila siku kukosa muda wa kumpa Mungu, wengine mpaka ibada za pamoja kanisani wameacha kabisa. Wamebaki kuiabia jumapili moja moja tena hiyo jumapili yenyewe anaenda ilimradi tu. Hilo bomu unalojitengenezea Ndugu hatari sana katika maisha yako, maisha yako yanapaswa kutaliwa na kumcha Mungu.

Mungu hajakupa hizo pesa ili uache kutulia kwake, Mungu hajakupa hiyo kazi nzuri ili usiwe kabisa na muda wa kutulia kwake, Mungu hajakupa nafasi ya kwenda shule/chuoni ili uwe mbali naye, Mungu hajakupa zawadi ya mtoto ili ujitenge mbali kabisa na yeye, Mungu hajakupa mke/mume ili uwe mbali naye, na Mungu hajakupa huduma ya kuhudumia wengine ili uwe bize kiasi kwamba usiwe na muda wa kusoma Neno lake.

Ukiacha kumpa Mungu muda wako, unamaanisha hicho alichokupa hakukistahili kwako maana kinachukua nafasi yake. Na unajua kabisa Mungu anachukia sana vitu vyote vinavyochukua utukufu wake, ni hatari kupenda vitu vingine zaidi kuliko Mungu. Kumbuka mwenye vyote hivyo ni Mungu, iweje usimpe nafasi ya kutulia mbele zake kujua anakuelekeza nini kupitia Neno lake? Badilika.

Usishindwe akili na watu wa mataifa, hicho unachofikiri hakikupi uhuru wa kusoma Neno la Mungu, Mungu atakiondoa na bado hutokuwa na muda wa kusoma Neno la Mungu. Zaidi sana utazusha lingine tena la wakati huo mgumu unaopitia.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, naamini kuna kitu umejifunza kupitia ujumbe huu. Endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kukua katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Website: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.