Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, atupaye kushinda kila siku.
Upo uvivu mwingine tunajitakiaga wenyewe pasipo kujua madhara yake yapoje tusipoachana na huo uvivu, mtu anajikuta anakuwa mvivu wa jambo kwa sababu wengi hawafanyi vizuri kwa hicho anachotaka kufanya au anachokifanya wakati huo. Hii inatokana na kukaririshana kuwa kitu fulani ni kigumu sana kukifanya.
Mtu anauwezo kukesha na vitabu vya darasani, vya kozi anayosomea vyenye ujazo mkubwa kuzidi hata biblia, anavisoma vyote na mpaka anavimaliza. Lakini akija kwenye biblia anakwambia hawezi kusoma maneno mengi, yaani amejenga hiyo picha kwa sababu tu amesikia wengine wanasema biblia ni ngumu.
Ugonjwa huu umewashika wengi mpaka kwenye vitabu vingine vya maarifa mbalimbali katika maisha yetu ya kimwili, mtu anauwezo wa kusoma vitabu vya hadithi vyenye ujazo mkubwa wa karatasi. Ila akishika kitabu cha maarifa ya msingi anaona ni tabu kukisoma, hata hata hakijafisha kurasa 100.
Ugonjwa huu umeendelea zaidi mpaka kwa wasomaji wa makala zenye mafunzo ya kujenga tabia njema, mtu anasoma kichwa cha somo anaishia hapo. Ila ikiwa habari nyingine ya kutengeneza isiyo na msaada wowote kwake atasoma hadi nukta.
Uvivu mwingi tumeamua Kujitengenezea wenyewe kichwani pasipo sababu yeyote, hakuna ulazima wa kufikiri kusoma Neno la Mungu ni ngumu. Ikiwa ni hivyo ina maana gani wewe kuokoka? Roho Mtakatifu aliye ndani yako anakusaidia kufanya nini? Lazima ukae chini uanze kujifunza Neno la Mungu.
Hatuwezi kuwa wakristo wa jumla jumla, wakristo wa ndio tu, hata kama tunadanganywa tuwe tunaitikia tu. Sababu haswa ya hayo yote ni uvivu wa kushindwa kupitia Maandiko Matakatifu wenyewe, hata ile kuhakikisha hilo andiko kwenye biblia zetu tunaona ni tabu. Mwingine anaweza kuwa ameenda kabisa kanisani na biblia ila akiambiwa fungua kitabu fulani anaona shida kupitisha macho kuona kinachosomwa.
Ukisema nyumbani ndio kabisaa huwa hatuna muda kuyachunguza maandiko tuliyojifunza, kwa hali hii tutawezaje kukwepa mafundisho potofu? Kwa hali hii tutawezaje kuepuka kulishwa matango pori? Kwa hali hii tutawezaje kuwa na uwezo wa kujitegemea na kuweza kujisimamia wenyewe kiroho? Unafikiri tutaweza kumpendeza Mungu wetu ikiwa ndani yetu hatuna kabisa Neno la Mungu?
Biblia sio kitabu kigumu kiasi kwamba hakuna mkristo yeyote anaweza kukielewa isipokuwa mchungaji tu, hakuna sehemu iliyoandikwa waachieni wachungaji wasome biblia tu. Wote tuna jukumu la kutangaza habari za ukuu wa Yesu Kristo, tutakuwaje na ujasiri kumhubiri Kristo ikiwa hatuna neno lake ndani yetu? Wakati mwingine tumemzuia Roho Mtakatifu kufanya kazi yake kwa sababu hatuna maarifa ya kutosha ya Neno lake.
Amini huo uvivu ulionao sasa wa kushindwa kusoma Neno la Mungu unaendelea kuulea mwenyewe, sababu kubwa inayokufanya uone huo uvivu ni wa kawaida ni vile unaona wakristo wenzako hawana mpango wa kusoma Neno la Mungu. Hata ile ukimwambia kuhusu kusoma Neno la Mungu wala hashtuki na anaweza kukuongezea maneno ya kukuvunja moyo kabisa.
Unapenda kujua ahadi za Mungu kwako kama mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni, vyema ukajenga utaratibu wa kusoma Neno la Mungu. Muhimu ni wewe kuamua kutoka ndani ya moyo wako na kuweka nidhamu na bidii katika kusoma Neno la Mungu, mwanzo unaweza kuanza kwa shida shida ila kadri unavyozidi kujifunza ndivyo unavyozidi kufunguka zaidi.
Usipende maneno tu ya kuendelea kuwa mzembe, hakikisha unaichukia hali ya kushindwa kusoma Neno la Mungu. Hakikisha unatafuta njia ya kuweza kutoka kwenye huo uvivu kama unavyofanya bidii kwa mambo mengine.
Jitoe miongoni mwa kundi lisilopenda kusoma Neno la Mungu, jiunganishe/ ambatana na kundi linalopenda kusoma Neno la Mungu. Umeona usomaji wako ni hafifu, hakikisha huo uhafifu unauondoa kabisa kwako.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu. Kwa masomo mengine mazuri zaidi usiache kufuatilia humu humu Chapeo Ya Wokovu.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.