Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, tumshukuru Mungu kwa kutuchagua tena tuwepo siku ya leo. Kazi ya leo ni kurekebisha tulipokosea jana, na kutubu kwa yale yote tuliyomtenda Mungu dhambi, na kuanza upya na Bwana. Kisha kumzalia Bwana matunda yaliyo mema mbele zake, hatuwezi kumzalia matunda yakampendeza yeye huku tunaendelea kumtenda dhambi.
Uchukuliaji wako wa Neno la Mungu upo vipi mpaka sasa, bado unasoma ki kawaida na kufanya ilimradi siku imepita, au huwa unasoma kwa sababu kuna kitu unakihitaji ndani ya Neno la Mungu. Na hicho unachokipata kinakusaidia au bado unaendelea kusikia kama hadithi za wengine wakisema wametendewa mambo makuu kupitia Neno la Mungu.
Moyoni mwako una alama gani ambayo unaweza kusema Mungu amekutendea jambo, kipi unakumbukumbu nacho ambacho unaweza kusema Mungu amebadilisha maisha yako ya kiroho kupitia Neno lake. Hicho ulichokiona ndani yako, bado unaendelea kuona moyoni mwako unazidi kusogea hatua kwa hatua, au ulikuwa ni moto wa siku za nyuma. Ila sasa baada ya kukutana na changamoto za maisha, hata ule moto wa kumtafuta Mungu kwa bidii kupitia Neno lake umezimika.
Muhimu sana kujitafakari na kujihoji moyoni mwako, kama una vitu unavipata kupitia Neno la Mungu, vizuri ukajua tangu uanze kusoma Neno la Mungu, Mungu anaweza kusema nawe kwa mazingira husika kupitia Neno lake au huna kumbukumbu yeyote ya Neno la Mungu.
Umewahi kukutana na mazingira fulani alafu Neno la Mungu likakujia moyoni mwako, unaweza usikumbuke limeandikwa kitabu gani ila ukaona kabisa linakujia kwa nguvu jinsi lilivyo. Hiyo ndiyo ninaizungumza hapa, maana yake kuna kitu umekipanda moyoni mwako ambacho ukikutana na jambo linalohitaji kujibiwa na andiko, Neno la Mungu linakujia.
Changamoto inakuja pale unasoma Neno la Mungu kila siku alafu bado huna kumbukumbu yeyote moyoni mwako kuhusu Neno la Mungu. Inadhihirisha wazi kwamba huwa unasoma Neno la Mungu bila kutafakari kile umekisoma, wewe unachokifanya ni kutaka kumaliza biblia nzima ili ujenge historia ya kufanya hivyo. Ila sio kupata kitu cha kukusaidia katika safari yako ya wokovu.
Kusoma Neno la Mungu bila kutafakari ulichosoma, ni sawa na kumeza makande bila kutafuna, si unajua madhara ya kumeza makande bila kutafuna? Bila shaka unajua au umewahi kuona kwa mtoto wako au wa jirani yako. Kwa wewe usiyejua makande nini, ni chakula kinachotokana na mahindi.
Nakusihi sana, usisome Neno la Mungu ili uje ujivunie kwa watu au uonwe na watu, hiyo ni tabia ya asili kwa mwanadamu hasa hasa akiwa mchanga kiroho ambapo akishafanya kitu anapenda ajulikane, atambulike, aonekane. Sasa wewe uliyeanza kukomaa kiroho jikite kwenye kupata kitu cha kwako ambacho unaweza kujivunia ndani ya moyo wako hata bila mtu yeyote kukuona.
Neno la Mungu linagusa kila eneo la maisha yako, kama ni ufunguo wa kufuli/kitasa, tunaweza kusema unaingia kila kufuli/kitasa utakayokutana nayo mlangoni. Kama bado unasoma Neno la Mungu hupati ufunguo wa kufungua hata mlango wa kusamehe waliokukosea, jua bado hujamaanisha kuokoka na Roho Mtakatifu hayumo ndani yako.
Tembea na hili, je moyo wako unahifadhi yale unajifunza au huwa unaachia hapo hapo baada ya kumaliza kusoma? Ili kuondokana na hili, vyema ukajenga utulivu na nia ya kweli ya kutamani kupata kitu ndani ya Neno la Mungu. Kingine cha kuzingatia sana ni kuwa na muda wa kutafakari Neno la Mungu, kuna vitu vingi sana vinapatikana katika kutafakari Neno la Mungu.
Katika kutafakari Neno la Mungu utafunguka mambo mengi sana ambayo hukujua kama umefungwa nayo. Lakini ukiwa unasoma Neno la Mungu kwa kukimbiakimbia kila siku, nakwambia utafika kipindi utasema sasa basi. Maana hakuna unachokipata zaidi ya kusoma kama hadithi fulani, japo unayesoma Neno la Mungu huwezi kufanana kabisa na asiyesoma.
Nina imani ujumbe huu umekukumbusha jambo la kufanyia kazi, usiache kuchukua hatua kwa hilo uliloliona unapaswa kulirekebisha. Maana usipochukua hatua itakuwa haina manufaa yeyote kwako.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu. Kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kukua katika usomaji wako wa Neno la Mungu.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.