Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana, ametupa kibali cha kuiona.

Tumejifunza mara nyingi kujenga nidhamu ya kusoma Neno la Mungu kwa mtu binafsi bila kusukumwa na mtu yeyote, hili ni muhimu sana kuendelea kulizingatia. Maana usipojijengea nidhamu wewe binafsi, itakuwa ni ngumu sana kufanikiwa katika hili jambo la usomaji wa Neno la Mungu.

Hili jambo la kusoma Neno la Mungu, sio sheria ambayo anawekewa mtu aifuate kwa lazima hata kama hapendi. Bali mtu mwenyewe anapaswa kujitambua anachofanya hapaswi kusukumwa kwa nguvu, isipokuwa anapaswa kujisukuma mwenyewe kwa hiari.

Kwa kuwa binadamu huwa tuna tabia ya kuchoka na kuona tunachofanya hakuna anayetuona, na huku mioyoni mwetu tunatamani kuendelea na bidii yetu ya kusoma Neno la Mungu lakini tunakwamia njiani.

Wengi huwa tunakata tamaa wakati mwanzo tulianza vizuri sana katika hili zoezi la kusoma Neno la Mungu, ila inapofika kipindi fulani tunazoea na kuona ni jambo ambalo lipo na tunaweza kupumzika tukaja kuendelea siku nyingine.

Tunapojidanganya tunapumzika ili baada ya muda fulani tutakuja kuanza tena kusoma Neno la Mungu, tunajikuta tumeachana kabisa na utaratibu wetu wa kujifunza Neno la Mungu kila siku.

Unaweza kujipa moyo ukiwa peke yako kuwa unaweza kupata muda wa kusoma Neno la Mungu kila siku bila kuwa na kikundi chochote. Ila nakwambia ukienda sana miezi miwili, na hiyo miezi miwili utakuwa umekutana na changamoto kadhaa ambazo zinakuvunja moyo wa kutoendelea.

Kwanini ni muhimu sana kwako kuwa na kundi la wenzako ambao nia yao na yako ni kusoma Neno la Mungu?

Jambo la kwanza; inakuwa rahisi kwako kusukumwa hata pale unaposikia kuchoka na kuhitaji kupumzika. Kusukumwa ninayoizungumzia ni ule msukumo wa ndani pale unapoona wenzako wanafanya kile mlikubaliana kwa pamoja.

Jambo la Pili; ni kujisikia vibaya kuwaangusha wenzako kwa kushindwa kwako kushiriki Neno la Mungu, hii inakupa hamasa zaidi ya kufanya kile mlikubaliana. Hata kama umechoka sana, hutokubaliana na uchovu ule ukutawale sana, lazima utatafuta njia yeyote kutuliza akili yako usome Neno la Mungu.

Jambo la Tatu; ukifika hatua huelewi ulichosoma kuanzia mstari wa kwanza mpaka wa mwisho, una nafasi ya kujifunza kwa mwenzako aliyeelewa vizuri. Kutokuelewa unachosoma huwa inatokea sana pale unapokuwa unasoma Neno la Mungu halafu akili yako haipo pale, hii ipo sana kwa mtu anayepitia changamoto fulani katika maisha. Pia kutokuelewa inaweza kumtokea mtu ambaye mawazo yake hayatulii sehemu moja, sio kwamba ana kitu kinamsonga la hasha ni yeye kushindwa kujitawala mwenyewe na kujiweka sehemu moja.

Anapokutana na changamoto ya kutokuelewa alichosoma kutokana na hizo sababu nilizoeleza hapo juu, anapokuwa na wenzake ni rahisi sana kutiwa moyo kwa kusaidiwa na mwingine. Kusaidiwa kule kunaweza kuwa kwa kusoma/kusikiliza tafakari za wengine, ama kunaweza kuwa kwa kuwaona wengine wanavyofunguka kueleza kile mlichokuwa mnajifunza pamoja.

Jambo la Nne; unapokuwa unajifunza Neno la Mungu na wenzako, lazima kuna kanuni mtakuwa mmejiwekea za kuweza kukubana na kupewa adhabu pale unapokiuka hizo kanuni. Sasa unapofikiri adhabu itakayotolewa kwako kwa kushindwa kushiriki kusoma Neno la Mungu na wenzako, inakupa nguvu ya kuchukua hatua ya kuungana na wenzako.

Unajikuta ile kuepuka adhabu, inakufanya kuendelea kutoa muda wako kila siku kusoma Neno la Mungu, tofauti na ungekuwa peke yako ungesema hakuna anayeniona na wala hakuna atakayeniuliza kwanini sikusoma Neno la Mungu. Lakini unapokuwa kwenye kikundi, utaulizwa kwanini mwenzetu hukujumuika nasi katika mpango wetu tuliojiwekea.

Kuendelea kupambana usije ukavunja kanuni, taratibu unajikuta unajenga tabia ambayo hukuwa nayo hapo mwanzo. Na hii tabia inakuwa ni njema kwako, na msaada kwako na kwa wengine wanaokuzunguka.

Jambo la tano; inakujenga zaidi kujiamini pale unapoona vile umeelewa wewe ndivyo na wengine wameelewa vivyo hivyo. Unakuwa huna yale mashaka labda nimekosea au labda umeelewa tofauti na wenzako. Hali hiyo inakufanya kuendelea kujenga ujasiri ndani yako ambao ukisimama kumshuhudia mwingine, unakuwa huna mashaka yeyote.

Tunajua wote unapopokea kitu kipya kwenye ubongo wako, huwa kuna wasiwasi fulani unaoambatana na kutokuelewa vizuri. Ila anapotokea mwingine akakilezea vizuri kile ulichokuwa na wasiwasi nacho, unapata ujasiri na kukiamini zaidi.

Unaona ni jinsi gani ni muhimu sana kuwa na kikundi cha wenzako wanaopenda kusoma neno la Mungu, unapaswa kuambatana na wenzako wenye kiu ya Neno la Mungu. Hata pale unapojisikia kuchoka wenzako wanakuvuta kwa namna ambayo hutoelewa sana wakati huo. Ila utaelewa zaidi pale utapokuwa tayari umefanya na badala ya kuumia kwanini ulifanya, utajisikia furaha kwa kushinda uchovu/uvivu.

Hivi vikundi utavipata wapi? Swali zuri sana; tafuta marafiki zako mtaani kwako ambao mnaweza kukutana kila jioni kujisomea Neno la Mungu. Kuwa na utaratibu wa kusoma Neno la Mungu na familia yako kabla ya kulala, na njia nyingine nzuri zaidi na rahisi ambayo unaweza kuitumia popote pale ni kuwa kwenye group la whatsApp. Kuwa kwenye group la whatsApp itakufanya usome Neno la Mungu kiurahisi zaidi kuliko zile njia nilizokutajia mwanzo.

Kama hujajiunga na kundi la Chapeo Ya Wokovu, na unajiuliza hilo kundi utalipata wapi. Usipate shida kwa hilo, cha kufanya ni kunitumia ujumbe wako kwa njia ya whatsAppp kwenda namba 0759808081. Hakikisha tunawasiliana kwa njia ya whatsApp na sio kwa njia nyingine.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kila siku.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.